ZABURI 91, NI ZABURI YENYE NGUVU NYINGI.

ZABURI 91, NI ZABURI YENYE NGUVU NYINGI.

Zaburi 91, Ni Zaburi iliyo ya kipekee sana yenye nguvu, Na shetani analijua hilo, ukitaka kuamini jiulize, ni kwanini Shetani aliitumia Zaburi hii kumjaribu Bwana,? Kiasi kwamba mtego wake ungekubali basi Zaburi hii ndio ingekuwa silaha ya kumwangushia Bwana.

Ni kwanini ainukuu Zaburi 91? Shetani aliijua nguvu na ulinzi Mungu aliouweka juu ya wampendao..Lakini wengi wetu hatuifahamu…Alimwambia hivi Bwana..

Mathayo 4:6 “akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.

7 Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako”.

Unaona, alijua kuwa mtu yeyote aliyempendeza Mungu, huwa anaachiliwa ulinzi wa kipekee, Mungu anamuagizia mpaka malaika zake, wamlinde, asijikwae,..

Hivyo kama wewe umeokoka  na umesimama vizuri basi fahamu Zaburi 91, Ni salaha yako madhubuti ya kummaliza shetani na vitisho vyake, na majeshi yake..Isipokuwa tu usiitumie hiyo kwa lengo la kumjaribu Mungu, vinginevyo utampa shetani nafasi ya kukuangusha kama alivyojaribu kufanya kwa Bwana Yesu.

Embu tuisome,

ZABURI 91

1 Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi.

2 Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini.

3 Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo.

Bwana anasema, atakuepusha na mitego ya mwindaji(Shetani), na tauni iharibuyo..akiwa na maana atakulinda na magonjwa hatari mfano wa Tauni kama Corona..Unaona ikiwa wewe ni mtakatifu, huna haja ya kuwa na hofu.

Anaendelea kusema…

Zaburi 91:4 Kwa manyoya yake atakufunika, Chini ya mbawa zake utapata kimbilio; Uaminifu wake ni ngao na kigao.

5 Hutaogopa hofu ya usiku, Wala mshale urukao mchana,

6 Wala tauni ipitayo gizani, Wala uele uharibuo adhuhuri,

Ndugu uliyeokoka, Bwana atakulinda tu, huna haja ya kuogopa, iwe ni mchana au usiku atakuwa na wewe kukulinda na mikono ya magonjwa na maadui.

Zaburi 91:7 Ijapo watu elfu waanguka ubavuni pako. Naam, kumi elfu mkono wako wa kuume! Hata hivyo hautakukaribia wewe.

8 Ila kwa macho yako utatazama, Na kuyaona malipo ya wasio haki.

9 Kwa kuwa Wewe Bwana ndiwe kimbilio langu; Umemfanya Aliye juu kuwa makao yako.

10 Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako.

Haijalishi utaona ni wangapi, wanadondoka, au wanashindwa pembeni yako, wameanguka, lakini wewe Bwana atakuwa na wewe wakati wote kuhakikisha hushindwi wala hupatwi na mabaya hayo yote, hata kama utaonekana kama unashindwa,lakini mwisho wa siku ushindi utakuwa ni wako tu,

Zaburi 91:11 Kwa kuwa atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote.

12 Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.

13 Utawakanyaga simba na nyoka, Mwana-simba na joka utawaseta kwa miguu.

Unaona zaidi ya hiyo, Malaika wa Bwana watakuwa na wewe kukulinda kila wakati, usijikwae, na mabaya..Na hiyo yote ni kwasababu gani? Ni kwasababu, umempenda Mungu na umemtafuta kwa bidii, umemfanya yeye kuwa tegemeo lako, na ndio maaana anasema..

Zaburi 91:14 Kwa kuwa amekaza kunipenda Nitamwokoa; na kumweka palipo juu, Kwa kuwa amenijua Jina langu.

15 Ataniita nami nitamwitikia; Nitakuwa pamoja naye taabuni, Nitamwokoa na kumtukuza;

16 Kwa siku nyingi nitamshibisha, Nami nitamwonyesha wokovu wangu.

Maneno ya faraja sana na yanayotia nguvu, lakini  mpaka Mungu kukutamkia hivyo ujue ni lazima kwanza uwe ni mwana wake mpendwa, vinginevyo, hakuna ulinzi wowote, utaokao kwake utakufikia..

Ili Mungu akulinde na tauni (Corona) isikuue, au magonjwa mengine ya kutisha yaliyozuka duniani leo hii, ni lazima uwe mwana wake mpendwa, ili Mungu akulinde na maadui (mapepo na wachawi), Ili Mungu akuagizie malaika zake watembee na wewe kila wakati kama alivyofanya kwa Elisha..basi ni lazima kwanza ufanyike mwana wake.

Ndipo hapo nawe utakapoitamka Zaburi 91 kwa ujasiri wote, na iwe kweli na maana kwako. Kumbuka  Zaburi hii ilimwingia sana shetani kichwani, na ndio maandiko pekee aliyoyatamka kwa kinywa katika biblia nzima, hiyo ni kuonyesha kuwa ni jinsi gani anaona wivu, kuona watoto wa Mungu wanapokea ulinzi wa kipekee kutoka kwa Mungu.

Maana yake ni kuwa ukimkosa leo Kristo, basi huwezi mshinda shetani, kwasababu ulinzi wa Mungu haupo juu yako.. Hivyo kama upo tayari leo kumpa Yesu maisha yako, basi uamuzi utakaofanya ni mzuri na wa busara sana..Kama ni hivyo fungua hapa kwa ajili ya maelekezo juu ya sala ya Toba.>>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Tafadhali Share na wengine,

Whatsapp: +255789001312

Mada Nyinginezo:

TAZAMA, NASIMAMA MLANGONI.

AGANO LAKO LINABEBWA NA NANI?.

WEWE NI BWANA UNIPONYAYE.

KIAMA KINATISHA.

JIFUNZE KUJITOA KWA MUNGU NA KUWA MKARIBISHAJI.

UNYAKUO.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments