USIINGIE MKATABA NA DHAMBI.

USIINGIE MKATABA NA DHAMBI.

Laiti Yuda angefahamu yatakayokwenda kumpata Bwana ni makubwa kiasi kile, asingedhubutu hata kidogo kumsaliti, Yeye alijua tu watakwenda kumchukua na kumkemea asiwafundishe makutano mahubiri yake, na kumtishia kidogo na kisha kumwachia aende…Lakini mambo kule yalienda kuwa makubwa kuliko alivyotegemea…Kwani walikwenda kumpiga, na kumdhihaki, na kufikia hatua mpaka ya kumwua Bwana tena kwa kifo cha aibu na mateso…

Kwasababu ya tamaa ya fedha hakujua tayari ametumika kulitimiza kusudi la shetani…Pasipo kuwa na macho ya kuona mbali alijikuta kawa chombo maalumu cha shetani. Moto mdogo aliouwasha akidhani utateketeza karatasi tu, sasa umeteketeza msitu mkubwa…Ndio maana mwishoni aliishia kujuta kwa aliyoyafanya, alipoona kwamba ni busu lake dogo tu limemfikisha Bwana msalabani, alipoona vipande 30 tu vya fedha vimemwaibisha vile na kumtesa kiasi kile…alipojua atafikishwa salama na kutoka salama lakini mwisho wake anaishia kuvuliwa nguo na kuvishwa taji ya miiba kichwani…ni Dhahiri kuwa ilikuwa ni nje ya mapatano yao..

Marko 14:44 “Na yule anayemsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni, MKAMCHUKUE SALAMA.

45 Basi alipokuja, mara akamwendea, akasema, Rabi, akambusu.

46 Wakanyosha mikono yao wakamkamata”.

Mstari wa 44 hapo unasema “mkamchukue salama”…Lakini kule alipokwenda walikwenda kumtesa na kumwaibisha na kumuua, kinyume na mapatano yao. Na hiyo yote ni kutokana na kuingia mkataba na dhambi.

Na mwisho Yuda anasema maneno haya…

Mathayo 27: 3 “Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, alipoona ya kuwa amekwisha kuhukumiwa, alijuta, akawarudishia wakuu wa makuhani na wazee vile vipande thelathini vya fedha, akasema, Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia.

4 Wakasema, Basi, haya yatupasani sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe.

5 Akavitupa vile vipande vya fedha katika hekalu, akaondoka; akaenda, akajinyonga”

Mambo machache tunaweza kujifunza hapo…unaweza kuuza wokovu wako kwa kitu kidogo..lakini mwishoni usijue kama kitakuletea au kitaleta madhara makubwa mbeleni…Umemwamini Yesu tayari, lakini unaingia tamaa ya kufanya zinaa..hivyo unatoka na kumwona mwanamke na kumtamani, na kusema nitatubu tu…siku unakutana naye kumbe kuna mwingine amewaona na kuwafuatilia mpaka nyumba mnayokwenda, na huko mnakuja kufumaniwa..na picha zinapigwa na kuwekwa kwenye mitandao..mtumishi fulani au mpendwa fulani afumaniwa na mke wa mtu…utajisikiaje siku hiyo?..Wewe ulidhani ni moto mdogo tu umewasha kumbe hujui utakwenda kuwa mkubwa wa kushtusha mji mzima, na hivyo hivyo na dhambi nyingine zote, tunaweza kuziona zina madhara madogo hapa tu..lakini baada ya kuzitenda ndio tutaona ukubwa wake..

Kwahiyo tunapaswa kuzidi kuwa makini kwa kila kitu, Mfano wa Yuda ni somo tosha kwetu…Tujichunge yasijikute na sisi, shetani akatudangaya tukajikuta tunamsulubisha Kristo mara ya pili kwa aibu na mateso. Na mwisho wa siku tukashindwa hata kurudi kule tulipokuacha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

MADHARA YA DHAMBI YA UASHERATI.

Je Mtu anaweza kusema uongo, Na Mungu akambariki?

NAMI NINAZO FUNGUO ZA MAUTI, NA ZA KUZIMU.

JE NI DHAMBI KUWA NA MAHUSIANO KABLA YA NDOA?

Kwanini wanawake wengi huwa wanalipuka mapepo?

MAMBO 5 AMBAYO KILA MKRISTO ANAPASWA KUFAHAMU.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
2 years ago

Ubarikiwe sana mtumish wa Mungu