Nini maana ya ..“huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino (mwanzo 3:15)”

by Nuru ya Upendo | 31 July 2025 08:46 am07

Swali: Uzao wa mwanamke utampondaye kichwa nyoka, na nyoka ataupondanye mguu uzao wa mwanamke?


Jibu: Turejee..

Mwanzo 3:14 “Bwana Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako;

15 nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; HUO UTAKUPONDA KICHWA, NA WEWE UTAMPONDA KISIGINO”.

Andiko hili lina maana mbili (02) ya mwilini na rohoni.. tuzitazame zote.

      1. MWILINI

Kiumbe cha kwanza kinachoogopeka zaidi na mwanadamu ni nyoka vingine ni simba na mamba, lakini nyoka ndiye anayeshika namba moja..

Na mwanadamu anapokutana na nyoka mara nyingi anakimbilia kuponda kichwa!… hata pasipo kufundishwa na mtu, kichwa cha nyoka ni shabaha ya kwanza ya mtu, na hiyo haiji tu kwa bahati mbaya bali ni kwasababu tayari tangu mwanzo Mungu alishasema hayo.. “HUO UTAKUPONDA KICHWA”.

Lakini pia sehemu ya kwanza sehemu ya kwanza ya nyoka kuuma/kugonga ni mguu wa mtu/kisigino, kwasababu ndio sehemu ya chini kabisa ya mwili wa mwanadamu na ndio sehemu rahisi nyoka kuifikia kwasababu yeye mwenyewe anatambaa kwa tumbo..

Ni ngumu nyoka kukimbilia kung’ata mkono wa mtu au goti la mtu, lakini ni rahisi sana kisigino kwasababu ndio kipo chini na karibu sana na yeye.. Sasa hiyo ni maana ya kimwili, yenye uhalisia hebu tutazame maana ya pili ya kiroho.

    2. ROHONI.

Kiroho “Uzao wa mwanamke” ni  “Uzao wa YESU KRISTO”.. sasa si kwamba Yesu ni mwanamke la!. Bali kwasababu alizaliwa na mwanamke pasipo mbegu ya mwanaume kuhusika… Kwahiyo Yesu alikuwa na mama wa kibinadamu, lakini hakuwa na Baba wa kibinadamu (Isaya 7:14)..ndio maana anajulikana kama Uzao wa mwanamke.

Na wote wanaomwamini Yesu wanaingia katika uzao huo, (wa mwanamke).. Na uzao wa mwanamke una nguvu kwasababu ndio uzao wa MUNGU.

Sasa kama uzao wa mwanamke ni Yesu pamoja na wote wanaomwamini, vipi kuhusu uzao wa nyoka. Uzao wa nyoka ni wote ambao hawaitaki kweli, lakini wanamwabudu ibilisi.. kwanini wote wanaomwabudu ibilisi wanaitwa uzao wa nyoka?.

Ni kwasababu Biblia inamtaja “Nyoka” kama Ibilisi (Soma Ufunuo 20:2).. Na tena Bwana Yesu akasema “ninyi ni wa baba yenu ibilisi”.

Yohana  8:43 “Mbona hamyafahamu hayo niyasemayo? Ni kwa sababu ninyi hamwezi kulisikia neno langu.

44 Ninyi ni wa BABA YENU, IBILISI, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake”.

Hapo anasema “Ninyi ni wa BABA YENU, IBILISI” sasa badala ya kusema “ibilisi” weka “nyoka” kulingana na Ufunuo 20:2, kwahiyo ni sahihi kabisa kusema “nyinyi ni wa baba yenu joka/nyoka” hivyo wao ni uzao wa nyoka.

Ndio maana Yohana akawataja kama wazao wa nyoka..

Mathayo 3:7 “Hata alipoona wengi miongoni mwa Mafarisayo na Masadukayo wakiujia ubatizo wake, aliwaambia, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja?”

Soma tena Mathayo 12:34, Bwana Yesu anautaja uzao wa nyoka.. Kwahiyo kumbe tumejua! Mtu yeyote anayeikataa kweli na kumwabudu ibilisi ni uzao wa nyoka!..

Sasa hebu turejee pale maandiko yanaposema “uzao wa mwanamke utamponda kichwa uzao wa nyoka, na uzao wa nyoka utaponda kisigino uzao wa mwanamke.”

Hapa anazungumzia uwezo wa kimamlaka.. Kwamba uzao wa mwanamke (yaani watu walio ndani ya Imani ya Yesu Kristo) watakuwa na mamlaka juu ya uzao wa ibilisi, na hawa watakuwa na uadui, ndio maana utaona ijapokuwa watu wa MUNGU siku zote ni washindi lakini bado wanakutana na majaribu ya watu wanaomwabudu ibilisi, na wakati mwingine wanaumizwa nao.

Kwahiyo upo uadui wa asili kati ya watu wa Mungu (walio na imani ya YESU) na wale wanaomwabudu ibilisi.. Watu wa Mungu wanaponda vichwa (yaani Uongozi na mamlaka) za falme za watu wa ibilisi, ndivyo maandiko yanavyosema..

Habakuki 3:13 “Ukatokea kwa ajili ya wokovu wa watu wako, Kwa ajili ya wokovu wa masihi wako; UKAKIPONDA KICHWA CHA NYUMBA YA WAOVU, Ukiuweka wazi msingi hata mwambani”.

Na kinyume chake, watu wa ufalme wa giza (wa ibilisi) wanasumbua miguu (sehemu za mwisho mwisho) za watu wa Mungu… ndio maana utaona ijapokuwa Kristo aliziponda mamlaka za giza pale Kalvari kupitia kifo chake lakini miguu yake ilikuwa na alama za misumari, kutimiza unabii wa uzao wa nyoka kuponda miguu uzao wa mwanamke.

Na Ukitaka kuthibitisha zaidi kuwa “Uzao wa Nyoka” unaweza kuwakilisha watu Fulani.. rejea maandiko yafuatayo..

Mwanzo 49:17  “Dani atakuwa NYOKA barabarani, BAFE katika njia, Aumaye VISIGINO vya farasi, Hata apandaye ataanguka chali”.

Kwahiyo tunaona kuna faida kubwa ya kuwa upande wa Bwana zaidi ya ule wa ibilisi.. kwasababu upande wa ibilisi utapondwa kichwa na uzao wa mwanamke..Na hata sasa matukio ya nyoka kuuawa na mwanadamu ni mengi kuliko nyoka kuua wanadamu.. kiroho inatakangaza jambo hilo hilo, kuwa uzao wa Mungu una nguvu nyingi.

Je upo upande gani?.. je wewe ni uzao wa nyoka au wa mwanamke??.. Kama hujaokoka huna haja ya kutafuta kujua upo upande gani, ni moja kwa moja upo ule wa nyoka, “wa kupondwa kichwa” kwasababu ibilisi ni nyoka.. Mpokee leo YESU na ugeuzwe asili yako, kama bado hujampokea, na uwe mtu mwenye mamlaka ya kuponda vichwa vya majoka..

1Samweli 2:10 “Washindanao na Bwana watapondwa kabisa; Toka mbinguni yeye atawapigia radi; Bwana ataihukumu miisho ya dunia; Naye atampa mfalme wake nguvu, Na kuitukuza pembe ya masihi wake”.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Wale Nyoka wa Moto jangwani, walikuwa ni wa namna gani?

TUMEPEWA AMRI YA KUKANYAGA NGE NA NYOKA.

KUOTA NYOKA.

Wale Nyoka wa Moto jangwani, walikuwa ni wa namna gani?

TUMEPEWA AMRI YA KUKANYAGA NGE NA NYOKA.

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/07/31/nini-maana-ya-huo-utakuponda-kichwa-na-wewe-utamponda-kisigino-mwanzo-315/