UMEITWA KWANZA KUWA SHAHIDI, SIO MHUBIRI

by Nuru ya Upendo | 16 September 2025 08:46 am09

Matendo 1:8

Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.

Ipo tofauti kati Mhubiri na Shahidi

Kwa lugha rahisi kuna tofauti ya kuhubiri na kushuhudia.
Yesu alituita tuwe mashahidi duniani.. Na hiyo ni kazi ya kila mmoja, Wito wa kumtangaza Yesu, sio wa kimahubiri, bali ni wa kiushuhudiaji.

Mhubiri ni nani?

Mhubiri ni mtu anayesimama na biblia, anayefundisha maandiko, anayefafanua, hadithi mbalimbali na mafunzo katika biblia kisha kutarajia watu kugeuka kwa mafundisho hayo. Huyu anaweza akawa mchungaji, mwinjilisti, mtume, Askofu, shemasi n..k

Shahidi ni nani?

Lakini shahidi ni mtu aliyeona ukweli wa jambo Fulani, kisha akasimama kama mteteaji au mthibitishaji wa ukweli huo.
Ndio kazi tuliyopewa sisi sote kufanya kuhusu Kristo, kuwa mashahidi wake ulimwenguni kote. Wa yale yote aliyotutendea sisi katika maisha yetu. Yaani yale aliyoyasema tukayathibitisha sisi wenyewe kuwa ni kweli katika maisha yetu.

Kwamfano pale aliposema njoni kwangu ninyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha (Mathayo 11:28). Ulipokwenda kwake ukaona mzigo huo umetuliwa, Hivyo tukio hilo huna budi kusimama na kulithibitisha kwa wengine, na wao pia waamini, ili watendewe jambo hilo hilo.

Pale Yesu aliposema tukiamini tukabatizwa, tutapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.(Matendo 2:38) Na wewe sasa umepokea Roho Mtakatifu, umejua ni ukweli, sasa hapo ndipo unapokwenda kuwashuhudia kwa wengine ukweli huo.

Pale ulipoponywa, ulipofunguliwa, ulipoonyeshwa ishara, ulipopewa nguvu ya kushinda dhambi fulani.. Hapo ndipo unapopashuhudia..Na kwa kupitia ushuhuda huo, mwingine atajengwa Imani na kumwamini Yesu kama wewe ulivyoamini hatimaye kuokoka.

Ushuhuda hauhitaji theolojia

Sasa kazi hii haihitaji theolojia ya biblia, haihitaji ukomavu wa kiroho, haihitaji mifungo na maombi, inahitaji tu kufungua kinywa chako na kuanza kueleza uzuri ulioupata ndani ya Kristo, na kwa njia hiyo ndio Mungu atamshawishi mtu na kuokoka.

Mfano wa Paulo – Matendo 9

Ukiwa kama mkristo umeokoka labda tuseme leo, Kumbuka tayari una deni la kuanza kushuhudia uzuri wa Kristo kwa maneno hayo hayo machache uliyonayo kinywani mwako.. Ndicho alichokifanya Paulo baada tu ya kubatizwa..

Matendo 9:
17 Anania akaenda zake, akaingia mle nyumbani; akamwekea mikono akisema, Ndugu Sauli, Bwana amenituma, Yesu, yeye aliyekutokea katika njia uliyoijia, upate kuona tena, ukajazwe Roho Mtakatifu.
Mara vikaanguka machoni pake vitu kama magamba, akapata kuona, akasimama, akabatizwa;
19 akala chakula, na kupata nguvu. Akawa huko siku kadha wa kadha pamoja na wanafunzi walioko Dameski.
20 Mara akamhubiri Yesu katika masinagogi, kwamba yeye ni Mwana wa Mungu.
21 Na wote waliosikia wakashangaa, wakasema, Siye huyu aliyewaharibu walioliitia Jina hili huko Yerusalemu? Na hapa alikuwa amekuja kwa kusudi hilo, awafunge na kuwapeleka kwa wakuu wa makuhani?
22 Sauli akazidi kuwa hodari, akawatia fadhaa Wayahudi waliokaa Dameski, akithibitisha ya kuwa huyu ndiye Kristo.
23 Hata siku nyingi zilipopita, Wayahudi wakafanya shauri ili wamwue.

Tatizo la kimtazamo juu ya kazi ya injili

Tatizo linatokea pale ambao tunaona kazi ya injili ni ya watu maalumu na ni nzito . Hapana, kumbuka anayeshawishi watu mioyo ni Mungu, sio kwa wingi wa vifungu vya maandiko au kwa uzoefu wa kuhubiri, bali kwa Roho Mtakatifu tu. Maneno mawili, tu yenye kumshuhudia Yesu, yana nguvu ya kugeuza mtu zaidi hata ya maneno elfu ya vifungu vya biblia.

Unapokwenda kushuhudia usifikiri fikiri ni nini utasema, wewe anzia pale ambapo ulitendewa na Yesu ikawa sababu ya wewe kuokoka.. muhadhithie huyo mtu Habari hiyo kwa taratibu. Utashangaa tu, huko huko Katikati Mungu anakupa hekima na kinywa cha kumhubiria mpaka utashangaa hekima hiyo umeitolea wapi. Pengine mtu atakuuliza swali umsaidie, lile jibu linalokuja kwenye kinywa chako liseme, wala usijidharau au usiogope, anayemshawi mtu ni Mungu, yeye kuelewa au kutokuelewa hiyo sio kazi yako ni ya Mungu, uwe tu na ujasiri, kwasababu hakuna Habari yoyote yenye maudhui ya Kristo ndani yake haina matokeo.

Anza sasa kumshuhudia Yesu, Na kwa Pamoja tuujenge ufalme wa Kristo. Anza na marafiki zako, familia, wafanyakazi wenzako, majirani zako kabla ya Kwenda hata mwisho wa nchi.

Mungu akubariki

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

JINSI YA KUSIMAMA NA KUFUNDISHA/ KUHUBIRI

YESU KATIKA KUCHOKA KWAKE.

Enendeni ulimwenguni mwote

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/09/16/umeitwa-kwanza-kuwa-shahidi-sio-mhubiri/