JIBU: Wakati ule Mtume Petro alipokuwa kule Yafa katika nyumba ya Yule mtu mtengenezaji ngozi, siku moja aliumwa na njaa sana, na alipotaka kwenda kuandaa chakula biblia inasema alizimia na kuona maono, na ndani ya maono yale aliona kitu kama nguo kubwa ikishuka kutoka juu na ndani yake imebeba viumbe vya aina zote duniani, wanyama wa kila namna. Na Bwana akamwambia Petro aende kuwachinja ale. Lakini kama tunavyosoma Petro alimjibu Mungu na kumwambia tangu azaliwe hajawahi kula vitu vilivyo najisi. Na ndipo hapo Mungu akamwambia nilivyovitakasa mimi usiviite wewe najisi.(Matendo 10).
Sasa pale ni jambo gani BWANA alikuwa anataka kumwonyesha Petro, Tukisoma ile habari, kuanzia mwanzo utaona kuwa kulikuwa na mtu mmoja mcha Mungu aliyeitwa Kornelio, Ni mtu ambaye hakuwa myahudi, wala hakujua sheria zozote za kiyahudi, Ni Mtu wa mataifa, lakini kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu alipewa neema ya kuwa mmojawapo wa wateule wa Mungu. Sasa kumbuka kabla ya hapo watu wa mataifa kule Israeli walijulikana kama najisi, hivyo hawakuruhusiwa kuchangamana na wayahudi kwa namna yoyote ile ya ibada. Lakini Mungu alimwambia Petro nilivyovitakasa mimi usiviite wewe najisi najisi, Ondoke uende katika nyumba ya Kornelio akawahubirie injili, akawabatize na wao pia wapokee habari njema za Yesu Kristo waokoke. Hivyo vile viumbe vya aina tofauti tofauti alivyoviona Petro, najisi, na visivyo najisi, vitambaavyo, virukavyo, vyenye miguu minne, nguruwe, bundi, popo, mbuzi, pweza,karungu-yeye, kivunja-chungu n.k.
Vilikuwa vinawakilisha jamii tofauti tofauti za watu waliopo duniani. Na ndio maana baada ya Petro kupata ufunuo huo ndio utaona kuanzia huo wakati nao pia wakaanza kuhubiri injili kwa watu wa mataifa pia, jambo ambalo hapo kabla walikuwa hawafanyi, walikuwa wakihubiri wa wayahudi tu peke yao. Japo YESU alishatangulia kuwapa maagizo hayo kabla lakini hawakumwelewa. Sasa ndio tukirudi kwenye huo mstari ambao Bwana aliwaambia mitume wake siku ile aliyokuwa anapaa kwenda mbinguni akisema “Enendeni ulimwenguni mwote,MKAIHUBIRI INJILI KWA KILA KIUMBE.” Alimaanisha waende wakahubiri injili kwa kila jamii ya watu waliopo ulimwenguni bila kuchagua hawa ni wayahudi, hawa si wayahudi, bila kujali rangi, dini zao, utamaduni wao, taifa lao, lugha zao n.k. Ilimradi ni mwanadamu basi injili ni lazima imfikie. Lakini Bwana hakumaanisha tukawahubirie kuku, na panya, na mijusi, na konokono injili.
Ubarikiwe.
Mada zinazoendana:
AGIZO LA UTUME.
INARUHUSIWA KULA NYAMA YA NGURUWE KWA MKRISTO WA KWELI?
MWILI NA DAMU YA YESU KRISTO.
WALIPO WAWILI AU WATATU KWA JINA LANGU
MPAKA UTIMILIFU WA MATAIFA UTAKAPOWASILI.
MZEITUNI HALISI UTAKAPOPACHIKWA.
Rudi Nyumbani:
Print this post