JIBU: Neno hilo halimaanishi kuwa hatupaswi kabisa kumwita mtu yeyote baba duniani hata wazazi wetu, hapana kama ni hivyo basi Mungu angekuwa anapingana na Neno lake pale aliposema “Waheshimu baba yako na mama yako (Kutoka 20:12)”
unaona?. Lakini tunapaswa kufahamu maneno hayo Bwana aliwalenga watu wa namna gani, ukisoma mistari hiyo kuanzia juu utaona kuwa aliwalenga wale mafarisayo na masadukayo ambao wao, walipenda kuchukua nafasi ya Mungu duniani kwa kila kitu, walitaka watu wawaone kama pasipo uwepo wao, hawawezi kumjua Mungu, pasipo watu kuongozwa na wao hawawezi kumfikia Mungu, yaani kwa ufupi walikuwa wanachukua nafasi ya Kristo duniani. Na ndio maana tukisoma tangu juu tunaona Bwana akiwaambia maneno haya..
Mathayo 23:1 “Kisha Yesu akawaambia makutano na wanafunzi wake, akasema,
2 Waandishi na Mafarisayo WAMEKETI KATIKA KITI CHA MUSA;
3 basi, yo yote watakayowaambia, myashike na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi.
4 Wao hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani mwao; wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole chao.
5 Tena matendo yao yote huyatenda ILI KUTAZAMWA NA WATU; kwa kuwa hupanua hirizi zao, huongeza matamvua yao;
6 hupenda viti vya mbele katika karamu, na kuketi mbele katika masinagogi,
7 na kusalimiwa masokoni, na kuitwa na watu, Rabi.
8 Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu.
9 WALA MSIMWITE MTU BABA DUNIANI; MAANA BABA YENU NI MMOJA, ALIYE WA MBINGUNI.
10 WALA MSIITWE VIONGOZI; MAANA KIONGOZI WENU NI MMOJA, NAYE NDIYE KRISTO”.
Mambo hayo hayo ndio tunayoweza kuyaona leo hii katika Kanisa la kirumi (Katoliki), ofisi ya kiPapa inajulikana kama “ofisi ya baba mtakatifu” na watu humweshimu yeye kama mpatanishi wa dhambi zao, na anaonekana kama ni mtu aliye na kibali cha karibu zaidi kwa Mungu zaidi ya watu wengine wote, hivyo amepewa heshima ya kipekee, anaketi mbele katika masinagogi (Katika umoja wa makanisa) ili atazamwe na ulimwengu wote kuwa yeye ni baba mtakatifu. Sasa Heshima kama hizo ambazo zinazohusianishwa na uhusiano na vyeo mbele za Mungu kwamba mtu Fulani ni mwenye cheo Fulani cha kipekee mbele za Mungu zaidi na wengine, ndizo Kristo alizokuwa anazikemea, kwamba tusimwite mtu yeyote Baba kwa namna hiyo, au kiongozi, au Rabi. Kwasababu sisi sote ni ndugu na hakuna aliye juu ya mwenziwe.
Pale Mtume Paulo alipomwita Timotheo na Tito wanae, alikuwa anaonyesha uhusiano aliokuwa nao kama mtumishi wa Mungu aliyewazaa katika injili, na kuwalea, kwa mfano wa Baba kwa mwanawe, lakini hakuwa na maana kuwa yeye yupo juu ya mwenzake, wala hakutanua hirizi zake wala kuongeza matamvua yeye, kiasi cha kukaa masokoni kupewa heshima na watu, kwamba ni sharti aanze yeye mbele za Mungu kisha wao, na kwamba pasipo yeye hawawezi kumfikia Mungu, Hapana na hakuna mahali popote Paulo alisisitiza yeye aitwa aitwe Baba.
Utaona nyaraka zake zote Mtume Paulo, alianza na “Mimi Paulo, mfungwa na Mtumwa wa Yesu, sehemu nyingine anasema mimi Paulo mtume wa Yesu Kristo”..Lakini hutaona sehemu yoyote anaanza kwa kusema “Mimi Paulo, Baba Mtakatifu wa kanisa takatifu korintho”..hapana hutaona hicho kitu.
Lakini inasikitisha zaidi kusikia leo hii watu wanagombania kuitwa baba, na wengine kwa nguvu, hata kama huyo mtu hana mahusiano yeyote ya kiiamani na yeye anayetaka amwite, bado atataka aitwe tu baba, hayo ndiyo Kristo aliyoyakataa, hiyo ni roho ya mpinga-kristo.
Lakini ikiwa ubaba wowote hautahusianishwa na kuchukua nafasi yoyote ya Kristo, huo hauna shida yoyote, ni kama tu vile unavyomwita mzazi wako baba au mama, hiyo haikuchukui nafasi yeyote linapokuja suala la kumwabudu Mungu, kwasababu unajua Baba yako aliye mbinguni ndiye anayestahili kupewa heshima zote za ibada na za kiungu.
Vivyo hivyo ikiwa utatoa heshima yako kwa kiongozi wako yeyote, au mwalimu wako, kanisani, hakikisha kuwa hilo halichukui nafasi ya Kristo, mnapokuja kwenye suala la kumwabudu Mungu basi sisi wote ni ndugu na tunapaswa kupeleka heshima zote, shukrani zote, na maombi yote kwa Mungu na sio kwa mwanadamu yeyote kama kanisa katoliki lifanyavyo kwa mapadre wao na Papa, na baadhi ya makanisa ya kiroho ambayo yanamfanya mtu mmoja kama ndio kila kitu kwao, huku wakimwita baba na pasipo yeye wanajihisi hawawezi kumwabudu Mungu. Hizo ni ibada za sanamu.
Ubarikiwe sana.
Mada Nyinginezo:
KWANINI YESU ALIMUITA BABA YAKE “ABA”?
MAANDALIZI YA UJENZI WA HEKALU LA TATU YAPO TAYARI.
MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA KITABU CHA RUTHU:
WALIPO WAWILI AU WATATU KWA JINA LANGU
MADHARA YA KUKOSA MAJI YA UZIMA BAADA YA KIFO.
About the author