JE! UMEFIKIA VIGEZO VYA KUWA BABA ROHONI?

by Nuru ya Upendo | 19 November 2025 08:46 am11

Kitabu cha Waraka wa kwanza wa Yohana ni kitabu ambacho kilielekezwa mahususi kwa makundi matatu (3) ya watu, Watoto, vijana, na Wababa.  Sasa sio Watoto au vijana au wababa kimwili, Hapana, bali alikuwa anazungumzia ngazi hizo katika roho, yaani Kundi la Watoto kiroho, vijana kiroho na wababa kiroho.

1Yohana 2:12-14

12 Nawaandikia ninyi, watoto wadogo, kwa sababu mmesamehewa dhambi zenu, kwa ajili ya jina lake.
13 Nawaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nawaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mmemshinda yule mwovu. Nimewaandikia ninyi, watoto, kwa sababu mmemjua Baba.
14 Nimewaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nimewaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu.

WATOTO:

Na kila mmoja wao ameelezwa sifa zao, zinazowafanya wawe vile. Kwamfano Watoto kiroho, anasema  ni kwasababu wamesahewa dhambi, lakini pia wamemjua Baba, tafsiri yake ni nini? Kwa mtu ambaye ni mchanga kiroho, anapokuja kwa Kristo, jambo la kwanza, ambalo atalipitia kwenye maisha yake, ni kutuliwa mizigo, mizito ambayo alikuwa anasumbuka nayo, ambayo asili yake ni dhambi. Ndio hapo ataanza kujiona mwepesi, anapokuja kwa Kristo, anajiona huru, katika kifungoni, anajiona na amani ambayo hajui chanzo chake ni nini, anajiona anapendwa,..Na ndivyo ilivyo upendo wa Mungu kwa huyu mtu unakuwa wa kipekee sana, ndio sababu kwanini anasema nimewaandikia nyinyi Watoto wadogo kwasababu mmesamehewa dhambi zenu, na mmemjua Baba. Hayo ni mambo mawili ambayo walio wa changa kiroho hujapitia.

VIJANA:

Lakini kwa vijana, anasema nimewaandikia kwasababu mmemshinda yule mwovu. Hatua hii ya ujana ni ya kipindi cha ukuaji kiroho, hapa mara nyingi mwamini hukutana sana na majaribu ya shetani, mapingamizi makubwa, vita vya kiimani, misukosuko kwa sababu ya Kristo. Kiroho mtu kama huyu huitwa kijana, kwasababu wakati huu, ijapokuwa atasongwa lakini huwa haachi kumng’ang’ania Mungu, moto wake hauzimiki, hata kidogo, kama ni maombi, kasi huwa ni ile ile,usomaji Neno haupungui,  hata akiumwa haiwi vyepesi kumwacha Mungu, kwasababu ni wakati wa Nguvu za Mungu nyingi Kutenda kazi ndani yake, na kumshinda mwovu kotekote.

WABABA:

Lakini Wababa kiroho, sifa yao pia ni tofauti na hao wengine, Sifa yao ni kuwa “ wamemjua yeye aliye tangu mwanzo”.

Maana yake ni nini? Kwanini hasemi kwasababu mmehubiri sana?, au kwasababu mmedumu sana ndani ya Kristo? Bali kwasababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo?

Kumfahamu Mungu, tangu mbali, ni kigezo kikuu sana cha ukomavu rohoni. Mpaka mitume kuitwa baba zetu, ni kwasababu walipewa kumwona Mungu kutokea mbali, tofauti na waandishi na makuhani..Ndio maana waraka tu huu ulipoanza anasema..

1Yohana 1:1 Lile lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono yetu ikalipapasa, kwa habari ya Neno la uzima;

Hili lilikuja kudhihirika pale Yesu alipoanza kuwaeleza mambo yake mwenyewe aliyoandikiwa tangu, Torati ya Musa, Zaburi na Manabii, jinsi alivyokuwepo na watu wake, jangwani, kupitia ule mwamba, Mana, nyoka wa shaba, jinsi alivyo mtokea Ibrahimu kama Melkizedeki, jinsi alivyojidhihirisha kwao kwa namna mbalimbali kupitia tumbo la Samaki kwa Yona n.k. lakini hawakumwelewa.

Luka 24:44

44 Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii na Zaburi.
45 Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko.

Sasa, mtu akishamwona Mungu kwa namna hiyo, basi Mungu kwake hawi wa “matukio” bali wa wakati wote. Yaani alikuwa nasi jana, yupo nasi leo, na atakuwa nasi hata milele.. Watoto wachanga kiroho, hawawezi kumwona Mungu jana, wenyewe Mungu wao, ni wa matukio ya leo.

Maeneo matatu ambayo macho yako yanapaswa yafunguke kuhusu, kumjua Mungu tangu mwanzo.

  1. Maandiko: Ili uwe Baba kiroho, ni sharti umwone Kristo tangu mwanzo wa uumbaji wote kama alivyowafundisha mitume (Luka 24:44).
  2. Maisha: Ni lazima umtambue Mungu madhihirisho yake tangu mwanzo wa maisha yako (Siku ulipozaliwa), Daudi mpaka kufanywa mchungaji wa Israeli, ni kwasababu alimwona Mungu tangu akiwa machungani, wakati ule alipokutana na dubu na Simba, aligundua kuwa ni Mungu ndiye aliyemsaidia (1Samweli 17:37)..Vivyo hivyo na mtu aliyekomaa kiroho, ataweza kumtambua Mungu, katika matukio mengi ya maisha yake, hata kabla hajaokoka, Na kujifunza Sauti yake
  3. Baada Ya kuokoka: Baada ya wokovu, mtu huwa anaanza maisha mapya, Na sasa ameshakaa muda Fulani mrefu, ni lazima ujifunze kumtambua Mungu katika nyakati mbalimbali alizokupitisha na uijie tabia yake kwako. Nyakati za taabu, za shida, za kufanikiwa na kupungukiwa..umwona Mungu, Jifunze kumjua yeye.. tangu mwanzo.. Ili usiwe tena mtoto mchanga.

Hivyo ile uwe Baba, ni lazima umjue Mungu aliyekuwepo tangu Mwanzo, usiwe mtu wa matukio ya leo leo, kama mtu uliyeokoka jana, Kaa chini, tafakari sana, hatua moja baada ya nyingine ya maisha yako, anzia kwenye maandiko uone jinsi Mungu alivyokuwa na watu wake tangu zamani, ambao wengine kwa kukosa kumjua wakawa wanalalamika tu, wanaishi kiwepesi wepesi, na hatimaye kumsulibisha, lakini wale waliomjua waligeuzwa na kuwa mitume wake,

Kuwa baba rohoni.

Mungu akubariki.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Je umewaonea utungu watoto wako?

Kwa jina lake Ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa.

LAKINI SISI HATUKUIPOKEA ROHO YA DUNIA.

WhatsApp
DOWNLOAD PDF

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/11/19/je-umefikia-vigezo-vya-kuwa-baba-rohoni/