by Nuru ya Upendo | 5 December 2025 08:46 am12
Biblia inatufundisha kumfahamu sana MWANA WA MUNGU (YESU KRISTO)..
Waefeso 4:13 “hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na KUMFAHAMU SANA MWANA WA MUNGU, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo”
Tukimjua vizuri mwana wa Mungu tutaweza kutembea naye vema, tutaweza kumpendeza vema na vile vile tutaweza kumheshimu zaidi.
Leo tutazame jinsi MWANA WA MUNGU (YESU KRISTO) alivyojitambulisha mwenyewe mara saba (07) kama “MIMI NDIMI”.
1. MIMI NDIMI MKATE WA UZIMA.
Yohana 6:35 “Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe”.
Maneno haya ameyarudia tena katika mstari wa 48 na 51 ya mlango huo huo wa sita (06).. Ikiwa na maana kuwa tukimpata YESU maishani ni zaidi ya chakula cha damu na nyama.. chakula cha damu na nyama kinatoa uzima wa masaa machache tu, au siku chache tu, na baadaye mtu atasikia tena njaa, na asipokula anakufa, lakini YESU ndiye chakula cha UZIMA, ambacho mtu akila hatasikia tena njaa.. bali atakuwa na uzima wa milele.
2. MIMI NDIMI NURU YA ULIMWENGU.
Yohana 8:12 “Basi Yesu akawaambia tena akasema, MIMI NDIMI NURU YA ULIMWENGU, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima”.
Kwa kumwamini YESU na kuyaishi maneno yake, maisha yetu yatakuwa na Mwanga, kila mahali tutakapokwenda na kila tutakachofanya kitakuwa na mwelekeo kama vile mtu anavyotembea katika Nuru..
3. MIMI NDIMI MLANGO WA KONDOO
Yohana 10:7 “Basi Yesu aliwaambia tena, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo”.
Yeye ndiye mchungaji mwema, na kama vile Mchungaji anavyowahesabu kondoo wake wanaoingia na kutoka zizini, na kwamba hakuna hata mmoja atakayepotea mkononi mwake, kadhalika na YESU ndiye Mchungaji wetu, atulindaye na kutuongoza zizini, kuingia kwetu na kutoka kwetu, wala mkononi mwake hatutapote.
4. MIMI NDIMI MCHUNGAJI MWEMA.
Yohana 10:11 “Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo”.
Mchungaji mwema ni Yule anayejitoa hata uhai wake kwaajili ya kondoo, na Kristo aliutoa uhai wake kwaajili yetu, kuonesha upendo wake mkuu kwetu.
5. MIMI NDIMI UFUFUO NA UZIMA.
Yohana 11:25 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi”
Kwa kumwamini YESU tunalo tumaini la kufufuliwa siku ya mwisho, hakuna mwanadamu yoyote wala malaika aliyewahi kumwahidia mwanadamu yoyote ahadi kama hii inayotoa tumaini baada ya kifo.
6. MIMI NDIMI NJIA, KWELI NA UZIMA.
Yohana 14:6 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi”.
Hakuna njia ya mkato ya kufika mbinguni, isipokuwa kupitia YESU KRISTO, tukilijua hili tutamwangalia kwa bidii ili tuwe warithi wa uzima wa milele.
7. MIMI NDIMI MZABIBU WA KWELI.
Yohana 15:1 “Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima”.
Tunapokaa ndani ya YESU ni kama matawi katika shina la mzabibu, ambalo linazaa sana, na sisi tutazaa sana kama tukikaa ndani ya YESU KRISTO.
Je umemkaribisha huyu YESU (Mkuu wa Uzima) maishani mwako?.. au bado unatanga-tanga na dunia tu!.. badilisha uelekeo leo, anza kutembea na YESU aliyejaa heshima.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
MANENO SABA YA YESU MSALABANI.
MFANYE BWANA YESU MWENYEJI MAISHANI MWAKO.
ZIFAHAMU ALAMA KUU NNE ZA KRISTO NDANI YAKO.
JITIE NGUVU KWA BWANA MUNGU WAKO.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/12/05/mimi-ndimi-saba/
Copyright ©2025 Wingu la Mashahidi unless otherwise noted.