MFANYE BWANA YESU MWENYEJI MAISHANI MWAKO.

MFANYE BWANA YESU MWENYEJI MAISHANI MWAKO.

Ipo tabia moja  ya kipekee ya wageni waliostaarabika. Kikawaida wageni walio wastaarabu huwa wanaonyesha tabia fulani baadhi ambazo wenyeji wanapaswa wazijue ili waweze kuchukuliana nao na kuendana nao.

Kikawaida mgeni sio mtu wa kuonyesha moja kwa moja kwamba anajitaji jambo fulani kutoka kwa mwenyeji, mgeni akija kukutembelea bila shaka hawezi kukuomba chakula hata kama ana njaa sana, utaona atakaa na wewe kimya, na  tena utakapofika wakati wa kuondoka, utaona anaondoka bila hata kukukumbusha suala la chakula, tena utaona anaondoka kwa furaha sana, na wakati mwingine hata kwa kukupa asante nyingi. Lakini moyoni, hajafurahishwa sana!.

Hivyo ni wajibu wako wewe kupambanua ni nini mgeni anahitaji kwa wakati huo. Kama ni chakula, au makazi au malazi.. Ili ajisikie yupo nyumbani kadhalika awe huru kuzungumza nawe zaidi..

Ukiona mgeni kakutembelea asubuhi jua kuna kitu anakihitaji kwako kwa asubuhi hiyo usimfanye akae mpaka jioni, wala usijifanye huelewi, ukiona mgeni kafika kwako mchana wakati wa kupata riziki, ujue ana nafasi pia katika hicho chakula, ukiona anashinda kwako mpaka jioni, ujue pengine anahitaji kulala kwako, mwekee mazingira ya kulala kwasababu pengine kuna jambo na atakapoona umemwelewa hali yake na umemruhusu ale chakula chako, au alale kwako, basi ni rahisi zaidi kusikia mengi kutoka kwake, au kukufunulia mengi.

Lakini ukimnyima riziki, au makazi, au malazi.. utafikiri kweli umemkomoa lakini hutasikia mengi, ambayo angetaka kukuambia..

Kadhalika Kristo naye kuna wakati anakuja kwetu kama Mgeni, au anatukaribia kama mgeni, na anakuwa anaonyesha tabia zote kama za mgeni. Atakuwa ana njaa, lakini atajifanya kama hana njaa, atakuwa anatamani kuja kulala na sisi lakini atajifanya kama anapita tu!. Ndicho kilichowatokea wale watu wawili waliokuwa wanakwenda Emau.

Hebu tuisome habari hiyo vizuri katika kitabu cha Luka.

Luka 24:13 “Na tazama, siku ile ile watu wawili miongoni mwao walikuwa wakienda kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili.

14 Nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotukia.

15 Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao.

16 Macho yao yakafumbwa wasimtambue.

17 Akawaambia, Ni maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea? Wakasimama wamekunja nyuso zao.

18 Akajibu mmoja wao, jina lake Kleopa, akamwambia, Je! Wewe peke yako u mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui yaliyotukia humo siku hizi?

19 Akawauliza, Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote;

20 tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha.

21 Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu yalipotendeka mambo hayo;……………..

25 Akawaambia, Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii!

26 Je! Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake?

27 Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe.

28 Wakakikaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, NAYE ALIFANYA KAMA ANATAKA KUENDELEA MBELE.

29 Wakamshawishi wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukaa nao”.

Hapo katika mstari wa 29 maandiko yanasema.. “NAYE ALIFANYA KAMA ANATAKA KUENDELEA MBELE.” Yaani baada ya kuzungumza nao muda wote huo, umefika wakati wa kuingia ndani, yeye anajifanya kama anataka kuendelea na safari!.. Hebu jiulize endapo wale watu wangekuwa wachoyo, na kusema kile chakula chetu kule ndani kinatutosha tu sisi wawili, huyu mtu mwache aendelee zake, je wangekosa mangapi?..au wangesema kile kitanda chetu kule ndani kinatutosha tu sisi wawili na si mwingine watatu, wangekosa mangapi?..Lakini tunaona walielewa hali ya mgeni kwamba kamwe hawezi kusema naomba jambo fulani kama anaona wenyeji hawana huo moyo.. Sasa hebu tuone wangekosa nini endapo wangemruhusu Bwana aende zake.. Tuendelee mbele kidogo katika mistari hiyo…

Luka 24:29 “Wakamshawishi wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukaa nao.

30 Ikawa alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa.

31 Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; KISHA AKATOWEKA MBELE YAO.

32 Wakaambiana, Je! Mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia maandiko?

33 Wakaondoka saa ile ile, wakarejea Yerusalemu, wakawakuta wale kumi na mmoja wamekutanika, wao na wale waliokuwa pamoja nao”,

Umeona, kumbe sio kila mgeni ni mgeni wa kawaida tu!, si kila anayekuomba ni kwasababu anashida, si kila anayetaka kuja kukaa na wewe ni kwasababu yake yeye, wengine wanataka kuja kwako kwa faida yako wewe, wengine wanataka kula chakula chako kwa faida yako wewe… Unyonge wa Kristo kwako ni kwasababu anataka wewe upate faida.

Hivyo hata leo hii, Kristo anakuja mioyoni mwetu kama mgeni, hivyo hatuna budi tumpe nafasi.

Jambo moja wengi wasilolijua ni kwamba Kristo sio dikteta, kwamba tunapompokea basi ataanza kututumikisha kama maroboti, siku zote anakuwa kama mgeni..maana yake unapompa nafasi zaidi ndivyo anavyojifunua kwako zaidi, unapomkataa anakuacha na kukupita..wala hakulazimishi, ingawa atakuonyesha kila dalili za kutamani kuendelea kukaa na wewe…

Na sio tu katika hatua ya kumpokea yeye, bali hata baada  ya kumpokea Yeye, endapo tukijitenga naye..na kujikuta tumezama kwenye mateso au majaribu hatakuja kutulazimisha atusaidie, atasogea karibu na sisi, kuonyesha ishara ya kutaka kutusaidia, lakini kama hatutampa basi hatatupa msaada..

Utasema hilo tunalithibitisha vipi kimaandiko…Hebu tusome kile kisa cha Bwana kutembea juu ya maji ni nini kiliwatokea mitume, na kwa jinsi gani Bwana aliwasaidia.

Marko 6:48 “Akawaona WAKITAABIKA kwa kuvuta makasia, kwa maana upepo ulikuwa wa mbisho; hata ilipopata kama zamu ya nne ya usiku akawaendea, akitembea juu ya bahari; AKATAKA KUWAPITA.

49 Nao walipomwona anatembea juu ya bahari, walidhani ya kuwa ni kivuli, wakapiga yowe,

50 kwa kuwa wote walimwona, wakafadhaika. Mara akasema nao, akawaambia, Changamkeni; ni mimi, msiogope”.

Ukisoma habari hiyo sehemu nyingine utaona, Baada ya Bwana kuingia chomboni, ule upepo ulikoma!.

Lakini nataka tuone hapo kwenye mstari wa 48, maandiko yanasema “AKATAKA KUWAPITA”.. Umewahi kujiuliza kwanini alikuwa anataka kuwapita?.. Ni kwasababu bado alikuwa hajaona kibali cha yeye kutoa msaada…ndio maana akataka kuendelea mbele

Sasa kama Kristo aliweza kufanya hivyo kwa wanafunzi wake!, ambaye aliwachagua yeye mwenyewe, atashindwaje kufanya kwangu na kwako?.

Huu ni wakati wa kumpa Kristo nafasi na kumfanya mwenyeji ndani yetu…

Unajua kabisa huelewi maandiko unapoyasoma, lakini bado humpi Yesu nafasi katika maisha yako, bado kwako ni mgeni mnyonge!.. Kwenda kanisani kwako ni jambo la kusukumwa na kulazimishwa!, kujikana nafsi kwako ni jambo zito.. ukiambiwa uache kuvaa suruali tu! Ni shida, uache vimini na mavazi yasiyo na heshima ni shida.. Kristo atajifunuaje kwako!.. Hawezi kwasababu akiangalia huku na huko anaona milango kila mahali imefungwa!… Unapitia tabu lakini hata kumtolea Mungu huwezi, zaidi sana unapinga matoleo, pasipo kujua kuwa wakati mwingine ni kwa faida yako si ya Kristo.

Je! Kristo ni mgeni au mwenyeji kwako?

Bwana Yesu anasema..

Mathayo 25:41“Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake;

42 kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula; nalikuwa na kiu, msininyweshe;

43 nalikuwa mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi, msinivike; nalikuwa mgonjwa, na kifungoni, msije kunitazama”.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya ya kila siku kwa njia ya Whatsapp  basi waweza kujiunga kwa kubofya hapa >>> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

YESU NI MFALME WA AINA GANI KWAKO? 

Je! mwanadamu wa kwanza kuumbwa ni yupi?

Kama tunaokolewa kwa neema kwanini wokovu tuupate kwa nguvu?

“Si watu wa kutumia mvinyo sana”, je tunaruhusiwa kutumia mvingo kidogo?(1Timotheo 3:8).

Hapana hata mmoja aliyethubutu kuambatana nao;

Tarshishi ni mji gani kwasasa?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
2 years ago

Amen.