NI KIZAZI KIPI WEWE UPO?

NI KIZAZI KIPI WEWE UPO?

Kibiblia  Kizazi ni kundi la watu linalozuka ghafla lenye tabia zinazofanana, linaweza kuzuka aidha kutokana na mabadiliko ya nyakati, au mabadiliko ya mazingira. Kwamfano, Wana wa Israeli walipokuwa Misri, chini ya Yusufu, waliishi kwa raha sana, Lakini Yusufu alipokufa pamoja na Yule Farao, kilinyanyuka kizazi kingine kisichokumbuka wema wa Yusufu, na hapo ndipo utumwa mgumu ulipoanza.

Vilevile, Wana wa Israeli walipofika katika nchi yao ya  Ahadi, mwanzoni waliishi maisha ya kumcha Mungu sana, lakini wakati ulipopita mrefu kilinyanyuka kizazi kingine kisichomjali Yehova, hapo ndipo Israeli ilipoanza kuingia katika matatizo mengi sana.(Waamuzi 2:10)

Na katika hichi kipindi cha Siku za mwisho, tunapaswa tuwe makini sana, Zipo tabia ambazo utaziona kwa watu wengi sana, lakini kiuhalisia hazikuwepo huko nyuma. Hivyo ni vizuri ukafahamu aina ya vizazi vilivyopo duniani sasa hivi  kulingana na biblia ili ujue wewe upo wapi na jinsi gani unapaswa ujiupeshe navyo.

  1. Kizazi cha uzinzi na zinaa:

 Bwana Yesu alisema..

Mathayo 12:39 “Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona”.

Ni kizazi cha watu kinachozuka kinapenda tu usherati na uzinzi kuliko kitu kingine chochote ulimwenguni. Leo hii tazama  mawazo ya vijana wengi yalivyo, sikiliza mazungumzo yao,  mambo wanayoyafanya kwa siri,vitu wanavyotazama mitandaoni, video za ngono, ni jambo la kawaida kwao, na kibaya zaidi sio tu vijana, hadi wazee na watoto wamo katika kundi hili. Jambo ambalo hapo zamani halikuwepo. Hiyo ni kuthibitisha kuwa ni hiki ni kizazi kingine kimezuka, ambacho ni hatari sana.

Bwana Yesu alisema..

Marko 8:38 “Maana kila mtu atakayenionea haya mimi, na maneno yangu, katika KIZAZI HIKI CHA UZINZI na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu”.

Ndugu, jiupeshe, na mkondo huu, si lazima uishe kama ulimwengu unavyotaka, kizazi hiki kimeshahukumiwa na Mungu.

     2) Kizazi cha nyoka:

Kipo kizazi cha Nyoka.

Mathayo 3:7 “Hata alipoona wengi miongoni mwa Mafarisayo na Masadukayo wakiujia ubatizo wake, aliwaambia, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja?

8 Basi zaeni matunda yapasayo toba;

9 wala msiwaze mioyoni mwenu kwamba, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba Mungu aweza katika mawe haya kumwinulia Ibrahimu watoto”.

10 Na shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.

Soma pia..Mathayo 12:34

Nyoka, alikuwa mwerevu sana kuliko wanyama wote mwituni, lakini alikubali kuwa chombo teule cha shetani. Uzao wake, ndio uliendelea mpaka kwa Kaini, na ndio maana watu wale walikuwa hodari sana , wagunduzi na wavumbuzi wakubwa, lakini waovu waliopindukia (Mwanzo 6:4). Ni watu ambao walikuwa hawana muda na Mungu, lakini kwa upande wa pili uzao wa Mungu, ulikuwa ni mnyenyekevu unaomtafuta Mungu usiku na mchana, vilevile na usio na masumbufu mengi ambao ulipitia kwa Sethi. (Mwanzo 4:26).

Inafunua hadi sasa, kwamba kizazi hiki kipo, Angalia dunia ya sasa, imestaarabika kuliko ile ya zamani, watu wanaelimu kubwa sana, wanagundua mambo makubwa  sana, wamekwenda mpaka mwezini, lakini ukiwagusia habari za Mungu, wanakuambia  hayo ni mawazo yako tu, hakuna Mungu,dini imetengenezwa na watu, wamejikita katika mambo ya mwilini, tu, elimu, utajiri, uvumbuzi basi, Mungu hayupo.

Ndugu, ikiwa na wewe upo katika jopo hili la watu, jiangue haraka sana, hichi ni kizazi, ambacho kipo ulimwenguni sasa.

   3) Kizazi cha watu wasiowatii wazazi wao.

Mithali 30:11 “Kuna kizazi cha watu wamlaanio baba yao; Wala hawambariki mama yao”.

Kuporomoka kwa maadili na nidhamu unakokuona leo, hakukuwepo huko nyuma. Leo utasikia mtoto anajibizana na mzazi wake, mwingine anampiga, mwingine anamzungumzia vibaya, wengine wametengeneza mpaka uadui na wazazi wao.. Kesi hizi ni nyingi sana sikuhizi..Wewe kama mtoto, wewe kama kijana, kuwa makini sana, kizazi hiki kimezuka ulimwenguni sasa. Unapoona, wenzako hawawaheshimu wazazi wao, na wewe usiwe mmojawapo.

Katika agano la kale mtu aliyejaribu kuonyesha utomvu wa nidhani kwa mzazi wake, sheria yake ilikuwa ni kifo. Jitathmini unawatii wazazi wako, Unawapenda?, unawabariki? Unawanenea mema? Unawaombea?.. Hata kama mzazi anakuudhi, huna ruhusu ya kurudisha baya kwa baya kwake. Vinginevyo upo chini ya laana ya kizazi hiki.

4) Kizazi cha watu wanaojiona siku zote wapo sawa:

Mithali 30:12 “Kuna kizazi cha watu walio safi machoni pao wenyewe; Ambao hawakuoshwa uchafu wao”.

Hili kundi ni kubwa sana, Mtamuhubiria mtu na kumwambia pasipo kumwamini Kristo, huwezi kuokolewa, yeye atakuambia, mimi naamini matendo yangu ni safi, ninaamini Mungu hiyo inatosha, siwezi kuhukumiwa. Atakuwa radhi, kujihesabia haki, hata kama ni mzinzi, au mlevi..Haoni hatia yoyote kwa anayoyafanya. Yeye anachoamini ni kuwa Mungu hawezi kumchoma motoni milele,.Nimeshakutana na watu wa namna hii wengi sana. Wanaodhani kuwa kwa kile wanachokiamini, ndio tiketi ya Mungu kuwaokoa siku ile.

Ndugu kama upo katika hili kundi jiepushe nalo, Ikiwa bado hujaokoka, mkimbilie Yesu, yeye pekee ndiye mwenye uwezo wa kukusafisha dhambi zako, na sio kile unachokiamini.

 5) Kizazi cha watu wenye kiburi:

Mithali 30:13 “Kuna kizazi cha watu ambao macho yao yameinuka kama nini! Na kope zao zimeinuka sana”.

Wapo watu ambao, kujishusha hakupo ndani yao. Wanajiona kuwa hakuna chochote kinachoweza kuwa msaada kwao, Mungu si kitu kwao, kwanini wakaombe, kwanini waende ibadani. Wapo radhi hata kuutukana wokovu, au kazi ya Mungu. Wanatumaini, mali zao, au ujuzi wao.

Kama tabia hizo zimeanza kuonekana ndani yako, geuka upesi.

  6) Kizazi wa watu wasio na huruma.

Mithali 30:14 “Kuna kizazi cha watu ambao meno yao ni panga; Na vigego vyao ni kama visu. Ili kuwala maskini waondolewe katika nchi, Na wahitaji katika wanadamu”.

Utu umeondoka duniani, Yupo radhi kufanya biashara haramu, bila kujali kinaleta madhara mangapi kwa jamii, anauza madawa ya kulevya, anauza bidhaa zilizoisha ubora, wanadhulumu haki za wajane na mayatima kwa faida zao wenyewe. Anaua, ili apate mali, n.k.

Tunayoyaona, hayakuwepo zamani, tusiwe watu wenye tamaa ya mali.

  7) Kizazi cha wenye adili:

Lakini pamoja na kuwepo kwa vizazi hivi vyote, vya watu waovu.. Biblia inasema pia, kitakuwepo kizazi cha watu wenye adili, wanaomcha Mungu, wanaotenda mapenzi yake.

Zaburi 112:1 “Haleluya. Heri mtu yule amchaye Bwana, Apendezwaye sana na maagizo yake.

2 Wazao wake watakuwa hodari duniani; Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa”.

Na ndio maana unaona pia wapo watakatifu wa Mungu leo duniani. Hawa ndio Bwana anaowatazama, na siku moja itafika Kristo atawahamisha kutoka katika huu ulimwengu kwa tukio la UNYAKUO na kuwapeleka mbinguni. Swali ni je wewe upo katika kizazi kipi?

Matendo 2:40 “Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi”.

Jibu unalo moyoni mwako.

Kumbuka Unyakuo upo karibu sana, dalili zote zimeshatimia, huna haja ya kuendelea kutangatanga na huu ulimwengu tena. Mgeukie Kristo akuokoe, ili uwe mmojawapo wa kizazi cha watu waadilifu.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp yanayotumwa kila siku basi bofya hapa >>>  WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita..

BADO UPO YERUSALEMU TU..GALILAYA HUTAKI KWENDA?

Nini maana ya msiwe waalimu wengi (Yakobo 1:3)?

FANYIKA SIPORA WA KRISTO, UNYAKUO UPO KARIBU.

Marago ni nini? ( Waamuzi 10:18)

Rushwa inapofushaje macho?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments