BALI MTAKASENI KRISTO MIOYONI MWENU

by Nuru ya Upendo | 6 March 2026 08:46 pm03

Neno utakaso mara nyingi, tunalitazama katika jicho la Mungu kututakasa sisi(1Thes 5:23), lakini pia sisi kujitakasa wenyewe (1Petro 1:22), lakini tunasahau kuwa Kristo naye tunamtakasa… maandiko yanasema hivyo katika,

1 Petro 3:14

[14]Lakini mjapoteswa kwa sababu ya haki mna heri. Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike; bali mtakaseni Kristo Bwana mioyoni mwenu.

Kama Kristo anatakaswa? Swali ni je! Anatakaswaje wakati yeye ni mkamilifu?

Hapo anasema;

mtakaseni Kristo Bwana mioyoni mwenu’. 

Kumbe ni mioyoni mwetu, sio kwamba yeye mwenyewe tumtakase mahali alipo(hawezi kutakaswa kwasababu yeye ni msafi). Mioyo yetu ndio humfanya aonekane kivingine.

Kutakasa ni kukifanya kitu kiwe kisafi au kiwe kikamilifu tena, kurejee katika hadhi yake iliyopotezwa.

Sasa kumtakasa Yesu moyoni, ni sawa na kumfanya Yesu awe jasiri tena, ajae utukufu wake, ajawe na raha na fahari yote ndani ya mtu.

Haya ni mambo ambayo ukiyatenda/ kuyakubali basi unamtakasa sana Yesu moyoni mwako

1) Kukubali njia ya msalaba

Sawasawa na hilo andiko hapo juu anasema..

1 Petro 3:14

[14]Lakini mjapoteswa kwa sababu ya haki mna heri. Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike; bali mtakaseni Kristo Bwana mioyoni mwenu.

Zipo nyakati ambazo utachukiwa bure kwasababu umekataa uongo, au utafukuzwa kazi kwasababu umekataa rushwa, au utafungwa kwasababu unahubiri injili ,au utapigwa kwasababu unakemea dhambi..

Nyakati kama hizi wengine huzikwepa, na kuamua kusimama na maovu ili tu kuepusha madhara yatakawapata… hawajui kuwa wanamweka Kristo kando.

Matokeo yake Yesu anakosa kutukuzwa ndani yetu, kwasababu yeye naye alikubali kuteswa kwa kusimamia ukweli na haki, akapigwa, akasulubiwa kwa kifo cha aibu.. Hivyo atakapoona watu pia wanafuata Nyayo zake, hutakasika sana, hujitukuza sana ndani ya huyo mtu, hujithibitisha kuwa kazi yake kamilifu huendelea kumulika gizani.

Hivyo usikwepe mapito yenye gharama, wala usihuzunishwe nayo maadamu ni haki unayoisimamia. Mtakase Kristo.

Lakini pia..

2) Kwa Kumsifu, kwasababu ya neema yake.

Waefeso 1:6-7

[6]Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa.

[7]Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.

Kwa jinsi unavyoitambua kazi ya Kristo aliyoitenda kwa ajili yako pale msalabani kwamba kwa kupigwa kwake umepokea neema na ukombozi kupitia msamaha wa dhambi ndivyo unavyomtakasa Kristo moyoni mwako.

Tumia muda mwingi kutafakari juu ya neema ya wokovu, kisha msifu na kumtukuza na kumshukuru juu ya hilo. Kristo anapoona umeithamini kazi yake, huinuka sana moyoni mwako.

3) Jitoe kwa vyovyote kwa ajili yake.

Utakumbuka yule mwanamke kahaba na Miriamu ndugu yake Martha walivunja vibweta vya marhamu vyenye thamani nyingi, wakampaka Yesu kichwani na miguuni, mpaka wengine wakasema ni upotevu mkubwa sana..lakini Yesu alipoona alisema wametenda kazi njema juu yake, (Marko 14:3-9, Luka 7:36-50).

Jifunze kumtolea Kristo sadaka zaidi hata kipimo chako cha sikuzote, sio kwamba unamshawishi Yesu kwa vitu, (yeye hashawishi na hivyo)..Lakini anapendezwa sana, na watoaji, anatakasika sana pale unapofanya kitu cha ziada kwa ajili ya Mungu wako. Jifunze kutoa sana sadaka.

4) Omba naye.

Yesu anajaa utukufu na waombaji…utakumbuka alikuwa na mitume kumi na wawili…lakini waliokuwa tayari kudumu naye katika masafa ya ndani ya kimaombi walikuwa ni watatu; yaani Petro Yohana na Yakobo.

Na wakati ule alipopanda juu ya ule mlima mrefu(Mathayo 17), ghafla walimwona katika utukufu mwingine wa ajabu, nguo zake zilikuwa zikimeta-meta kwa weupe mkuu.. wakashangaa na kuingiwa na hofu..

Lakini Yesu asingeweza kubadilika mbele yao, kama wangekuwa mbali na yeye katika maombi.

Hivyo unapozama sana katika uombaji, ndivyo unavyomtakasa Kristo ndani yako. Anajiona safi na mkamilifu.

Kwa hitimisho ni kuwa, unapokubali mateso pamoja na Yesu, unapo msifu sana kwa kazi yake ya msalaba, unapotoa sadaka zako nyingi na unapokuwa mwombaji.

Moyoni unahesabika kuwa unamtakasa Bwana wako sana.

Shalom, Mungu akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

WALAWI WALIKUWA WENYE MIOYO YA ADILI KWA KUJITAKASA KULIKO MAKUHANI.

Kanisa kama sehemu ya maisha ya mwamini mpya.

SHUGHULIKA NA HASIRA INAYOKAA KIFUANI


 

WhatsApp
DOWNLOAD PDF

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2026/03/06/bali-mtakaseni-kristo-mioyoni-mwenu/