MAUMIVU YA DHAMBI

by Nuru ya Upendo | 27 April 2026 08:46 am04

Tambua Dhambi inaua chini kwa chini..

Je unajua ni kwa namna gani?….

Hebu fikiri kama mwili wako usingewekewa hisia ya maumivu kabisa, maana yake ukijikata na kisu hauhisi maumivu, ukipigwa husikii maumivu, ukinywa kitu chenye kudhuru husikii maumivu yoyote ya tumbo, ukiwa na vidonda vya tumbo husikii maumivu yoyote..

Unadhani ni nini kingetokea baada ya muda fulani?..bila shaka ni “kifo cha ghafla”.. kwanini? Kwasababu ungepata majeraha ambayo yangeendelea kukuharibu ndani kwa ndani, na usingekujua kama kuna tatizo kwasababu hakuna hisia yoyote ya maumivu utakayokupa taarifa ya tatizo mahali fulani, hali kadhalika usingekuwa mtu wa kujijali, kwani maumivu yanasaidia kujijali na kujihadhari.

Sasa dhambi iko hivo hivyo…haina hisia yoyote ya maumivu katika mwili, kiasi kwamba mtu anapoifanya anaweza kudhani hajaingiza madhara yoyote katika maisha yake, lakini mwisho wake ni kifo cha ghafla.

Hiyo ndio saababu ya Bwana MUNGU kumwambia Adamu pale bustanini kuwa asile  yale matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, kwani atakufa, agizo hilo halikuwa kwa faida ya MUNGU bali kwa faida ya  ADAMU na kizazi chake, ili waishi na wasife.

Mwanzo 2:17 “walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika”.

Na vinyo hivyo maandiko yanasema kuwa mshahara wa dhambi ni “MAUTI”

Warumi 6:23 “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu”.

Ndugu, dhambi haina maumivu mwilini, hautasikia maumivu yoyote mwilini ukishamaliza kuzini, au ukishafanya anasa, ukitukana, ukiishi maisha ya dhambi, n.k lakini madhara yake yanakuja ghafla utaona amani uliyokuwa ndani yako inakufa ghafla, furaha yako inakufa ghafla, Baraka zako zinazima ghafla, na mwisho kifo cha mwili kinahitimisha ikiwa mabadiliko hayatafanyika mapema.

Lakini habari njema na nzuri ni kwamba kwa YESU hata kama mambo baadhi yameshakufa kutokana na dhambi, ipo ahadi ya ufufuo wa mambo hayo endapo mtu atamkimbilia YESU kwa njia ya kutubu na kujinyenyekeza mbele zake, ile amani iliyokufa inarudi mara dufu, ile furaha iliyokufa inafufuka, ule ushindi ulioupoteza unarudi, ile afya iliyopotea inarudi na mambo mengine mazuri..

Je ni wewe leo ambaye dhambi imekuulia mambo yako mazuri, na ni ghafla?.. na hujui nini cha kufanya?.. hakuna atakayekutoa hapo, hata upate pesa kiasi gani bado shida itakuwepo, hata dunia nzima ije upande wako na kukufariji bado utaona kuna kupungukiwa mahali fulani..

Suluhisho lipo kwa mmoja tu, nakuambia ukweli.

Na huyo si mwingine zaidi ya YESU MNAZARETI,  huyo atakugeuzia ukurasa wa maisha na kukupa uzima wa hapa duniani na ule wa milele ujao (uzima tele).

Yohana 10:10 “Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.

11 Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo”.

Unachopaswa kufanya ni kukiri kuwa wewe ni mkosaji, na dhamiria kuacha dhambi, yeye atashughulika kukuongezea nguvu ya kushinda dhambi, na pia tafuta ubatizo sahihi wa maji mengi kwa jina la Bwana YESU KRISTO, (Matendo 2:38), hapo utakuwa umekamilisha hatua zako za wokovu, kwani yule Roho Mtakatifu ataingia ndani yako, na kukufanyia miujiza ambayo hata ukihadhithia huwezi kueleweka.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

UVUKISHE MIPAKA UPENDO WAKO.

JINSI YA KUACHA DHAMBI INAYOKUTESA.

SHUGHULIKA NA HASIRA INAYOKAA KIFUANI

SAFARI YA KUUONA USO WA MUNGU.

MKATAE MWAJIRI HUYU MBAYA.

WhatsApp
DOWNLOAD PDF

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2026/04/27/maumivu-ya-dhambi/