MARIAMU, MAMA WA KUWEKA MAMBO MOYONI.

by Nuru ya Upendo | 12 May 2026 08:46 pm05

Huu ni mfululizo wa masomo maalumu ya wanawake, ikiwa utapenda kupata madarasa mengine mengi ya nyuma wasiliana nasi kwa namba zilizo chini ya somo hili.

Mariam ni mwanamke ambaye Mungu alimchagua kipekee kuwa mfano bora wa kuigwa wa namna wanawake wa kikristo wanavyopaswa kuwa.

Mariamu alijitunza usichana wake, lakini pia sifa nyingi kubwa aliyokuwa nayo, hakuwa mtu wa kawaza ki-akili bali aliwaza kwa moyo. Kila jambo lililomfikia halikuishia akilini tu, kwamba ni hoja nzuri tu, au kwamba inaingia akilini, hapana bali alijifunza kulishusha mpaka moyoni, kulitafakari …Na hilo lilimsaidia sana kuwa mwanamke bora…

Embu tafakari haya matukio machache, mwitikio wake ulivyokuwa;

Luka 1:28-29

[28]Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. 

[29]Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? 

Luka 2:17-19

[17]Walipomwona wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. 

[18]Wote waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji. 

[19]Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake. 

Luka 2:48-51

[48]Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni. 

[49]Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? 

[50]Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia. 

[51]Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake. 

Hiyo ni kuonyesha ilikuwa ni desturi ya maisha yake, kufikiri kutoka kilindi mwake sio kwa akili zake…

Wazia zaidi, Mariamu aliposalimiwa alijiuliza salama hii, lengo lake ni nini? nyuma ya salamu kuna lengo gani, Mwisho wake ni upi.. hakupokea salamu, ilimradi salamu kisa inamtakia mema…aliivunja vunja kwanza..Na huko ndio kuwaza kwa moyo.

Mabinti wengi leo hii wanaingia kwenye mitego ya kulaghaiwa kwa kutowaza kutoka moyoni..hujiulizi iweje mtu usiyemjua aje kukupa tu salamu ya zawadi, akusifie, na wewe hufikiri salamu hii ni ya namna gani…

Hujiulizi huyu mtu nia yake ni nini? Anatarajia nini kwangu, kumbuka salamu sio lazima tu ije kwa maneno, yaweza kuja kwa kupewa lifti, kupewa nafasi ya upendeleo, kulipiwa manunuzi fulani, dada kuwa makini na salamu hizo, hata kama umeolewa kuwa makini sana. Ni kweli si zote ni mbaya lakini jiulize maudhui yake ni nini? Waza moyoni mwako, Nia ni nini?.

Kama mama yetu Hawa pale bustanini angejiuliza salamu za nyoka ni za namna gani, sote tusingekuwa kwenye matatizo tuliyonayo sasa.

Halidhalika Mariamu, hakuyaacha maneno yenye jumbe za Mungu yampite hivi hivi, mahali ambapo hajaelewa alihifadhi ndani yake akitumai upo wakati ataelewa vema kwa jinsi anavyozidi kutafakari…alihifadhi matukio yake yote moyoni..

Lakini wanawake wengi wa leo, wanahifadhi maneno yasiyo na maana, utaona moyoni mwao yamejaa maneno waliyosengenywa, waliyoaabishwa, waliodhalilishwa..hayo ndio yanawaganda lakini si maneno ya Mungu..

Wanatumia vibaya nafasi hizo, Na matokeo yake kinachotoka nje ya mioyo yao ni wivu, uchungu, hasira, chuki, masengenyo, badala ya mafunuo, upendo, hekima, na adabu.

Tumia moyo wako kwa lengo la kupambanua na kuhifadhi mambo mema…sio maovu.

Ifike wakati, unasema…lile hubiri lililohubiriwa mwaka juzi mpaka leo linanitafakarisha, lile ono Mungu alilonionyesha utotoni linanirudia rudia akilini, yale maonyo ya mhubiri tuliyokemewa kipindi kile yanazunguka ndani yangu hata sasa siwezi yasahau…

Hayo ndio mambo ya kubeba..

Geuka fikiri kama Mariamu.. 

Shalom

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

MAOMBI MAALUMU YA WA-WAMAMA / WANAWAKE WA KANISANI.

MAPAMBO YA WANAWAKE WALIOUKIRI UCHAJI WA MUNGU.

MASOMO MAALUMU KWA WANAWAKE.

WhatsApp
DOWNLOAD PDF

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2026/05/12/mariamu-mama-wa-kuweka-mambo-moyoni/