by Admin | 10 July 2018 08:46 am07
Bwana wetu YESU KRISTO atukuzwe.
Tunamshukuru Mungu kwa kutupa neema hii mpya ya kujifunza Neno lake. Leo tukiwa ukingoni kabisa wa kitabu cha Yona ile sura ya nne. Kama tulivyojifunza katika sura zilizotangulia, Nabii Yona anawakilisha kundi la wakristo pamoja na wahubiri walio vuguvugu wa Imani biblia inawaita wanawali wapumbavu, ambao walipaswa kuingia na Bwana wao katika karamu lakini kwasababu Taa zao hazikuwa na mafuta ya ziada wakaachwa. Kwasababu walikisia tu kwamba yale mafuta yaliyokuwa katika taa zao yangewatosha mpaka wakati wa Bwana wao kuja (Mathayo 25). Ni Mfano dhahiri wa wakristo wa kanisa hili la mwisho la Laodikia.
Na kiini cha sura hii ya mwisho tunaona ni Yona kutoa SABABU YA YEYE KUTOKWENDA NINAWI. Na haya yote tunayaona ni baada ya Bwana kughahiri mabaya yote aliyokuwa ameyakusudia kuyaleta juu ya Mji wa Ninawi, baada ya kuona kuwa matendo yao yamebadilika na kutubu, Tunasoma:
Yona 4
“1 Lakini jambo hili lilimchukiza Yona sana, naye akakasirika.
2 Akamwomba Bwana, akasema, Nakuomba, Ee Bwana; sivyo hivyo nilivyosema, hapo nilipokuwa katika nchi yangu? HII NDIYO SABABU NALIFANYA HARAKA KUKIMBILIA TARSHISHI; KWA MAANA NALIJUA YA KUWA WEWE U MUNGU MWENYE NEEMA, UMEJAA HURUMA, SI MWEPESI WA HASIRA, U MWINGI WA REHEMA, NAWE WAGHAHIRI MABAYA.
3 Basi, sasa, Ee Bwana, nakuomba, uniondolee uhai wangu; maana ni afadhali nife mimi kuliko kuishi.
4 Naye Bwana akasema, Je! Unatenda vema kukasirika?
5 Ndipo Yona akatoka mjini, akaketi upande wa mashariki wa mji, akajifanyia kibanda huko, akakaa chini yake uvulini, hata aone mji ule utakuwaje.
6 Na Bwana Mungu aliweka tayari mtango, akaufanya ukue juu ya Yona, ili uwe kivuli juu ya kichwa chake, na kumponya katika hali yake mbaya. Basi Yona akafurahi sana kwa sababu ya ule mtango.
7 Lakini siku ya pili kulipopambazuka, Mungu akaweka tayari buu, nalo likautafuna ule mtango, ukakatika.
8 Basi ikawa, jua lilipopanda juu, Mungu akaweka tayari upepo wa mashariki, wenye hari nyingi; jua likampiga Yona kichwani, hata akazimia, naye akajitakia kufa, akasema, Ni afadhali nife mimi kuliko kuishi.
9 Mungu akamwambia Yona, Je! Unatenda vema kukasirika kwa ajili ya mtango? Naye akasema, Ndiyo, natenda vema kukasirika hata kufa.
10 Bwana akamwambia, Wewe umeuhurumia mtango, ambao hukuufanyia kazi, wala kuuotesha; uliomea katika usiku mmoja, na kuangamia katika usiku mmoja;
11 na mimi, je! Haikunipasa kuuhurumia Ninawi, mji ule mkubwa; ambao ndani yake wamo watu zaidi ya mia na ishirini elfu, wasioweza kupambanua katika mkono wao wa kulia na mkono wao wa kushoto; tena wamo wanyama wa kufugwa wengi sana?”
Kama tunavyosoma maandiko hapo juu, sababu pekee iliyomfanya YONA akaidi njia za Mungu, ni kumkadiria Mungu kwamba yeye anaweza yote, Yona alimsoma Mungu kwa muda mrefu akaona jinsi alivyokuwa analirehemu taifa la Israeli pindi walipokuwa wanamuudhi sana Mungu, na kutaka kuangamizwa lakini Mungu alikuwa akighahiri mabaya yote. Hata wakati Yona alipokuwa anaishi katika Taifa lake, uovu wa wana wa Israeli ulikuwa ni mwingi sana, lakini Bwana alikuwa akiwahurumia kwa kuwatumia manabii wake kuwaonya watubu. Hivyo Yona kwa kuyajua hayo yote, Neno la Mungu lilipomjia na kuambiwa aende Ninawi kawahubiria watu watubu vinginevyo wataangamizwa, yeye akajisema ndani ya moyo wake, ..’aa Mungu najua siku zote ni wa rehema, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa huruma, huwa anaghahiri mabaya, ni mwema, anatupenda sana. mwisho wa siku atasamehe tu!.Yona hakuona sababu ya kwenda kuwapa watu presha, wakati mwisho wa siku anajua wataponywa tu! Mungu ni mwingi wa rehema. Hivyo Yona kwa kulijua hilo akalifanya lile Neno kuwa jepesi sana, na kuendelea na mambo yake mwenyewe, na kama tunavyosoma habari yakamkuta mabaya yale pale alipopitia dhiki isiyokuwa ya kawaida tumboni mwa samaki siku tatu usiku na mchana….
Ndivyo ilivyo kwa wahubiri wa leo na wakristo walio vuguvugu, Wahubiri wengi mwanzoni walitumwa na Mungu kweli wawahubirie watu habari za TOBA, na kwamba wamgeukie Mungu na kuacha njia zao mbaya kwasababu hukumu ya Mungu inakuja. Lakini wengi wamegeuka sasa wanawahubiria watu mahubiri ya faraja angali wanajua kabisa Hakuna amani kwa mtu ambaye hajatubu kwa kumaanisha kuziacha dhambi zake na kujazwa Roho Mtakatifu, Mahubiri yao siku zote ni …”Mungu ni wa rehema”…”Yote ni mema, “Haijalishi”..”Mungu ni Mungu wa upendo” “Hawezi kuteketeza dunia leo wala kesho,… tunaishi chini ya neema”..”Mungu haangalii mavazi, anaangalia moyo”n.k.
Wahubiri hawa kiini cha mafundisho yao ni faraja na mafanikio ya ulimwengu huu tu!..TOBA inatupiliwa nyuma kama kitu kisichokuwa na umuhimu sana. kwamba kwao laana kubwa ni mtu ambaye hajafanikiwa kimaisha, na sio mtu ambaye hajatubu dhambi zake. Lakini hawakusoma kwamba Neno la kwanza Yohana mbatizaji alilohubiri katika huduma yake ni TOBA, pia Hubiri la kwanza lililotoka katika kinywa cha Bwana wetu YESU KRISTO ni TUBUNI! kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. Lakini wao neno lao la kwanza ni NJOO UPOKEE!!.. Na kundi kubwa la wakristo limeungana na hawa watu hawajui kuwa wote kwa pamoja wanaelekea Tarshishi kwa NJIA YA BAHARI ambapo humo yumo yule mnyama atokaye baharini mwenye vichwa 7 na pembe 10 (Ufunuo 13&17) aliyewekwa tayari kuwameza, katika kile kipindi cha dhiki kuu. Wakati huo unyakuo wa Bibi-arusi wa kweli wa Kristo utakuwa umeshapita.
Lakini ni kwasababu gani watayapata hayo yote?. Ni kwasababu walikisia kuwa Mungu ni Mungu wa rehema, si mwepesi wa hasira, kwani kuna watoto wasiojua mema na mabaya, kuna wanyama, kuna mimea, n.k. Bwana hawezi kuangamiza vyote hivyo. Lakini ndugu nataka nikuambie Bwana anaweza kama alifanya kwa wakati wa Nuhu, na wakati wa Luthu atafanya pia katika siku za mwisho kama watu wasipotubu.
Kuna wakati kilele cha maovu ya Israeli kilifika na Bwana akakusudia Yuda kuchukuliwa utumwani (BABELI). Na Bwana alimtumia nabii Yeremia kutoa unabii huo kwa mfalme wa Israeli na wakuu wake, na kuwaambia baada ya siku ambazo si nyingi watachukuliwa mateka waende Babeli, lakini alizuka nabii mmoja anayeitwa HANANIA yeye alinyanyuka na kutabiri kuwa Bwana ameghahiri mabaya hawataenda tena utumwani zaidi ya yote vile vitu vyao vilivyochukuliwa kabla vitarudishwa. Hivyo Israeli wote wakafurahi na kustarehe na kufarijika sana, wakijua ni habari njema, kumbe hawajui Hanania hakutumwa na Mungu ni nabii wa uongo. Na baada ya miezi 2 Mungu alimuua kwa kuwatumainisha watu uongo.
Yeremia 28: 15 ” Kisha nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania, Sikia sasa, Ee Hanania; Bwana hakukutuma; lakini UNAWATUMAINISHA WATU HAWA MANENO YA UONGO.
16 Basi Bwana asema hivi, Tazama, nakutuma uende zako toka juu ya uso wa nchi; mwaka huu utakufa, kwa sababu umenena maneno ya uasi juu ya Bwana.
17 Basi nabii Hanania akafa, mwaka uo huo, mwezi wa saba.”
Hivyo ndugu usidanganyike na Injili za matumaini kana kwamba hakuna hukumu inayokuja mbeleni. Tunaishi katika siku za mwisho hizi, Bwana Yesu yupo mlangoni kurudi, wakati umeenda sana, ishi maisha ya TOBA, na utakatifu, jiepushe na ibada za sanamu, uasherati, ulevi, anasa, mavazi ya kikahaba, rushwa, usengenyaji n.k.(Waebrania 12:14) ubatizwe katika ubatizo sahihi kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako, ujazwe na Roho wa Mungu. Huko ndiko kufanikiwa kwa kwanza kwa mkristo ndipo mafanikio mengine ya mwilini yafuate.
Mungu akubariki sana.
Kwa maombezi/ Ushauri/ Ratiba za Ibada/Maswali/ Whatsapp/ Piga namba hizi: +255693036618/ +255789001312
Tafadhali share ujumbe huu kwa wengine na Mungu atakubariki!.
Mada Nyinginezo:
ALIYE MKUU KATIKA UFALME WA MBINGUNI.
NINI TOFAUTI KATI YA MATENDO YA SHERIA NA MATENDO YA IMANI?
BWANA ALIPOSEMA “SIKUJA KUTANGUA TORATI BALI KUITIMILIZA” ALIKUWA ANAMAANISHA NINI?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2018/07/10/yona-mlango-wa-4/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.