by Admin | 17 July 2018 08:46 am07
Kuna tofauti kati ya MAMLAKA(CHEO) na UTAJIRI. Unaweza ukawa tajiri lakini usiwe na mamlaka au cheo na pia unaweza ukawa na CHEO na usiwe tajiri au unaweza ukawa na vyote viwili kwa pamoja. Kwamfano viongozi wenye vyeo kama wakuu wa mikoa, madiwani, mawaziri na mameya, wana nguvu na usemi juu ya watu wote pamoja na matajiri huko huko, haijalishi matajiri wana fedha kiasi gani, hiyo haiwapi wao mamlaka ya kuiamrisha nchi. Kiongozi akisema ndiyo ni ndiyo na hapana ni hapana japokuwa hao viongozi wanaweza wasiwe na mali na utajiri wowote wa kuwazidi hao matajiri wa nchi lakini wamepewa mamlaka makuu juu ya wote yaani matajiri na wasio matajiri. Lakini matajiri hawawezi wakawa na mamlaka juu ya wakuu wa nchi (Viongozi).
Vivyo hivyo katika ukristo, kuna UKUU na UTAJIRI. tutazame utajiri ni upi na ukuu ni upi;
UTAJIRI KATIKA UFALME WA MBINGUNI:
Kama tunavyofahamu utajiri unakuja kwa bidii na juhudi za mtu, kwa jinsi unavyofanya kazi sana, na kujiwekea hazina ndivyo utajiri wake unavyokuja. Na ndivyo ilivyo hata kwa Mungu utajiri katika Kristo unakuja unapokuwa mwaminifu katika kazi ya Mungu. bidii yako kuitumia karama uliyopewa katika kuhubiri, kuwavuta watu kwa Kristo, kutumika katika kanisa, kutenda wema na ukarimu, kutoa sadaka, kusaidia yatima na wajane pamoja na maskini n.k, kiufupi kazi zote njema zinazotokana na Mungu. Yote haya ni HAZINA unayojiwekea mbinguni ambao ndio huo UTAJIRI wako,
Luka 12:33 “Viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo haharibu.Kwa kuwa HAZINA YENU ILIPO, ndipo itakapokuwapo na mioyo yenu. “
Unaona jinsi utoavyo sadaka ndivyo utajiri wako unavyoongezeka mbinguni.
Marko 12:41 “Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi.
42 Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa.
43 Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini AMETIA ZAIDI kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina;
44 maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake AMETIA VYOTE ALIVYOKUWA NAVYO, ndiyo riziki yake yote pia. ”
Unaona tena hapo kitu cha pekee alichokuwa nacho yule mwanamke ni pale alipotoa vyote alivyo navyo kwa ajili ya BWANA, ikamfanya aonekane mbinguni kuwa mwenye utajiri mkubwa kuliko wote, nasi pia tunafundishwa tufanye hivyo sio tu pale tunapozidiwa na mali tumtolee Mungu, bali hata katika hali ya upungufu tuliyopo tumtolee Mungu vyote ili UTAJIRI wetu mbinguni uwe mkubwa.
UKUU KATIKA UFALME WA MBINGUNI:
Tukisoma..
Mathayo 18:1 “Saa ile wanafunzi wakamwendea Yesu wakisema,
2 Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni? Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao,
3 akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa KAMA VITOTO, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.
4 Basi, YE YOTE AJINYENYEKESHAYE MWENYEWE KAMA MTOTO HUYU, huyo ndiye aliye MKUU katika ufalme wa mbinguni.”
Wengi wanadhani unapohubiri injili, au unapotoa sadaka sana, au unapotumika kanisani sana kunakufanya wewe kuwa MKUU mbinguni hapana huko kote ni kukuongezea utajiri(HAZINA) yako mbinguni lakini sio kukupa wewe UKUU au MAMLAKA, Kama tulivyotangulia kusema mtu anaweza akawa na mamlaka na asiwe tajiri, au anaweza akawa na vyote kwa pamoja na ndivyo ilivyo hata kwa Mungu, UKUU au UKUBWA, au MAMLAKA unakuja kwa njia moja tu. Biblia inaiita “KUJINYENYEKEZA NA KUWA MDOGO KULIKO WOTE KATIKA KRISTO” Kwa mfano wa mtoto mdogo Hilo tu!.
Na kujinyenyekeza huku kunakuja kwa namna mbili..
1.Unyenyekevu kwa MUNGU.
Bwana Yesu alituambia tuwatazame watoto wadogo, kwasababu watoto wadogo siku zote wanaweka tegemeo lao lote kwa Baba zao kwa kila kitu kwa chakula,afya,malazi,mavazi n.k., wao ni kama kondoo pasipo wazazi wao hawawezi kufanya lolote, wanapoadhibiwa ni wepesi kubadilika na hawana kinyongo, kichwa cha mtoto mdogo ni chepesi kujifunza kuliko cha mtu mzima kwasababu yupo tayari siku zote kukubali kusikia, mtoto mdogo ni mtii, na anaamini lolote atakaloambiwa na wakubwa zake bila kushukushuku, Na ndivyo Bwana Yesu alivyokuwa kwa BABA yake tunasoma kila mahali alikuwa anamtaja BABA, BABA, BABA,ikiashiria pasipo BABA yake hawezi kufanya lolote soma Yohana 5:19″Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile vile. “..Unaona hapo jinsi YESU alivyojinyenyekesha chini ya mapenzi ya baba yake na kuwa mtii hata MUNGU akamfanya kuwa mkubwa kuliko vitu vyote vya mbinguni na duniani.
Wafilipi 2:8 “tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, ALIJINYENYEKEZA AKAWA MTII HATA MAUTI, naam, mauti ya msalaba.
9 Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina;
10 ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi;
11 na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba. “
Na sisi vivyo hivyo tunapaswa tujinyenyekeze chini ya BABA yetu wa mbinguni mfano wa MTOTO-na-BABA yake. mapenzi yetu yafe lakini ya Mungu yatimizwe maishani mwetu.Hii ndiyo sadaka ya kwanza mtu anaweza akamtolea Mungu yenye kumpendeza. Kumbuka BWANA YESU alishuhudiwa na BABA kwanza kuwa AMEMPENDEZA kabla hata hajaanza kuhubiri injili au kufanya kazi ya Mungu.(mathayo 4). Hii ni namna ya kwanza na ya pili ni;
2.Kujinyenyekeza chini ya ndugu (wakristo).
Bwana Yesu aliwaeleza wanafunzi wake,atakayetaka kuwa mkubwa kati yenu na awe mdogo kuliko wote, kama yeye alivyokuwa mdogo kuliko wote. YESU alimnyenyekea BABA pamoja na wanadamu Vivyo hivyo na sisi pia sio tu kumtii Mungu halafi tunawadharau ndugu zetu, na kujifanya sisi ni KITU fulani cha kipekee zaidi ya wao. tunapaswa tujishushe tuwatumikie wenzetu mfano ule ule wa YESU KRISTO hata kufikia kiwango cha kuona nafsi ya ndugu yako ni bora kuliko ya kwako. Tusome..
Marko 10:42 “Yesu akawaita, akawaambia, Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha.
43 Lakini haitakuwa hivyo kwenu; BALI MTU ATAKAYETAKA KUWA MKUBWA KWENU, ATAKUWA MTUMISHI WENU,
44 NA MTU ANAYETAKA KUWA WA KWANZA WENU, ATAKUWA MTUMWA WA WOTE.45 Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, NA KUTOA NAFSI YAKE IWE FIDIA YA WENGI.”
Mahali pengine Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake.
Mathayo 11:11 ” Amin, nawaambieni, Hajaondokea mtu katika wazao wa wanawake aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji; walakini ALIYE MDOGO KATIKA UFALME WA MBINGUNI ni MKUU kuliko yeye. “
Hii ikiwa na maana kuwa yule ANAYEJINYENYEKEZA (KWA MUNGU na KWA WANADAMU) na KUWA MDOGO, Huyo ndiye aliye MKUU kuliko Yohana mbatizaji,.Unaweza ukaona ni faida gani aliyonayo mtu yule ajishushaye kama mtoto mdogo halafu anakuwa mkubwa kuliko hata manabii mfano wa Yohana Mbatizaji na wote waliomtangulia kabla yake.
Katika utawala unaokuja huko mbele wa milele, Kristo akiwa kama MFALME WA WAFALME, atatwaa wafalme wengine hao ndio watakaoitawala dunia wakati huo milele, sasa hizi nafasi za wafalme hawatapewa wale MATAJIRI WA ROHO bali wale WAKUU WA ROHO. Hawa wakuu watakuwa na amri, na usemi kwa kila kitu na kila kiumbe duniani kitakuwa chini yao kwasababu watakuwa wamepewa hayo na MKUU WA WAKUU (YESU KRISTO), Biblia inasema wataichunga dunia kwa fimbo ya chuma,(Ufunuo 2:26 Na yeye ashindaye, na kuyatunza matendo yangu hata mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa, naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, kama vyombo vya mfinyanzi vipondwavyo, kama mimi nami nilivyopokea kwa Baba yangu. Nami nitampa ile nyota ya asubuhi. )… watakuwa wenye mataji mengi kama leo hii tu huwezi kuwakaribia hawa wafalme wa dunia ambao sio kitu itakuwaje kwa wale?? watakuwa ni miale ya moto kama BWANA MWENYEWE.
Vivyo hivyo na MATAJIRI watapewa heshima yao, watamiliki hazina nyingi, watakuwa na HESHIMA katika ulimwengu kama tu vile matajiri wa ulimwengu huu wanavyoheshimika sasa, chochote watakachotaka watapata, kwasababu walijiwekea HAZINA nyingi mbinguni, kuna viwango vya umiliki watafikia wewe usiye na kitu hutaweza kufika.
Bwana mwenye haki atamlipa kila mtu kwa kadri ya alichokipanda ulimwenguni. Kumbuka wapo pia watakaokuwa MATAJIRI NA WAKUU kwa pamoja. Hao ndio wale waliojinyenyekeza na kumtumikia Mungu kwa bidii na kwa moyo, waliitangaza injili, walikuwa watumishi kati ya ndugu, watakatifu, waaminifu katika karama walizopewa, walikuwa kama vitoto vidogo mbele za MUNGU, walikuwa na mapenzi yao wenyewe lakini wakayakataa na kuyakubali mapenzi ya MUNGU maishani mwao, katika mapito yao yote hawakumnung’unikia, walitii na kumwamini pasipo majadiliano kama tu mtoto na baba yake mfano wa BWANA WETU YESU KRISTO.
Kwahiyo ndugu tuutafute UKUU na UTAJIRI WA MBINGUNI. lakini zaidi UKUU ambao kwa huo tu ndio utakaokuleta karibu na Mungu.
Ufunuo 3:19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.
20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.
21 Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi. “
Mungu akubariki.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2018/07/17/aliye-mkuu-katika-ufalme-wa-mbinguni/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.