UAMSHO MKUU UMEKARIBIA!!

by Admin | 17 July 2018 08:46 am07

UAMSHO MKUU UMEKARIBIA!!

Yoeli 2:28-32″ Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono;

29 tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu.

30 Nami nitaonyesha MAMBO YA AJABU KATIKA MBINGU na KATIKA DUNIA, DAMU, na MOTO, na MINARA YA MOSHI.

31 JUA LITAGEUZWA KUWA GIZA, na MWEZI KUWA DAMU, kabla haijaja hiyo siku ya Bwana iliyo kuu na itishayo.

32 Na itakuwa ya kwamba mtu awaye yote atakayeliita jina la Bwana ataponywa; kwa kuwa katika mlima Sayuni na katika Yerusalemu watakuwako watu watakaookoka, kama Bwana alivyosema; na katika mabaki, hao awaitao Bwana.

UVUVIO MKUBWA UNAKUJA DUNIANI:

Tukisoma mistari hiyo Nabii Yoeli alionyeshwa maono ya uvuvio mkubwa wa Roho ya Mungu ambao ungekuja katika siku za mwisho,  Na ni dhahiri kabisa kwa wasomaji wa biblia wanafahamu sehemu ya huo unabii ulitimia wakati wa PENTEKOSTE, pale Roho wa Mungu alipowashukia wale watu 120 kwa mara ya kwanza, na kuwapa vipawa vikubwa na vya ajabu, ishara na miujiza mingi ikifanywa na mitume na wale wote waliojazwa Roho Mtakatifu.

Mvua hii ya Roho Mtakatifu Mungu aliyoiachilia kwa mara ya kwanza  pale Pentekoste inajulikana kama “MVUA YA AWALI/MASIKA” ( kwa kiingereza former Rain). Lakini pia Mungu aliahidi kuileta mvua nyingine tena ambayo ni “MVUA YA BAADAYE/ VULI” ( kwa kiingereza Latter Rain). Kwa ufafanuzi wa maelezo haya tusome;    

Yoeli 2:23 “Furahini, basi, enyi wana wa Sayuni, mkamfurahie Bwana, Mungu wenu; kwa kuwa yeye huwapa ninyi MVUA YA MASIKA, kwa kipimo cha haki, naye huwanyeshea mvua, MVUA YA MASIKA, na MVUA YA VULI, kama kwanza.” 

Kwahiyo hii mvua ya pili (MVUA YA VULI) mbali na ile ya kwanza iliyotokea wakati wa Pentekoste, Tukisoma katika historia ya ukristo Bwana aliishusha tena mwaka 1906, kwenye uamsho uliotokea mtaa wa AZUSA, huko Calfornia Marekani ambapo Bwana alimwaga ROHO wake na kushusha vile vipawa tena  vya Roho Mtakatifu kama ilivyokuwa katika Pentekoste ya kwanza baada ya kanisa la Kristo kukaa muda mrefu bila uamsho kwa muda wa karne nyingi, lakini kuanzia huu mwaka 1906 tunaona vipawa vyote vilirejeshwa watu wakaanza kunena kwa lugha, kutabiri, kuponya magonjwa, ishara na miujiza, unabii n.k. vitu ambavyo havikuwahi kutenda tangu wakati wa kanisa la kwanza.

Hivyo basi Mungu alimtuma mjumbe wake William Branham kama mjumbe wa kanisa la mwisho LAODIKIA, ufunuo 3, Mungu alimtumia kwa ishara nyingi na miujiza ya ajabu ambayo haikuwahi kufanyika hapo kabla ikiwemo na utambuzi wa siri za mioyo ya watu, tafsiri za ndoto kama ilivyokuwa kwa Nabii Danieli, na ishara zilizoweza kuonekana wazi na kunaswa katika picha za kimagnetiki, n.k.

Ndipo Mungu akaendeleza kuimwaga hiyo roho kwa watumishi wake wengi waaminifu duniani kote kwa mfano wa William Branham kama oral Robert, Billy Granham, TL Osborn, nk.. 

UAMSHO MKUU UMEKARIBIA!!  Yoeli 2:28-32" Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono;

( tazama ushuhuda mfupi juu ya huduma na maisha ya William Branham,)

Mvua hii ya mwisho itatimizwa katika huu wakati wa mwisho Bwana aliahidi sehemu hii ya maandiko itaenda kutimia

Yoeli 2:29 “tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu.

30 Nami nitaonyesha mambo ya ajabu katika mbingu na katika dunia, damu, na moto, na minara ya moshi.

31 Jua litageuzwa kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla haijaja hiyo siku ya Bwana iliyo kuu na itishayo. 

Kumbuka katika mvua iliyoachiliwa mara ya kwanza, tuliona unabii, lugha, maono, ndoto, ishara, n.k. lakini hatukuona mambo ya ajabu katika dunia na katika mbingu kama jua kutiwa giza, mwezi kuwa damu, moto, minara ya moshi, n.k. tumezoelea kuona unabii na uponyaji, lakini haya mambo mengine yaliyosalia  yanaenda kutimilika katika hii mvua ya mwisho na yatakuja na hukumu sio kwa kuwaburudisha watu, Tunaona mfano uliotokea kwa mapigo ya Musa na Eliya. Ni mambo ya kutisha yanakuja. Na ishara ambazo hata hazijawahi kurekodiwa wala kufanywa mahali popote pale katika historia ya dunia.

Kumbuka hakuna ishara isiyokuwa na  ujumbe nyuma yake. Hivyo hizi ishara zitakuja na ujumbe, na ujumbe wake utakuwa ni wa kipekee, ukisoma kitabu cha ufunuo 10:4-11″ Inaelezea zile NGURUMO SABA ambazo Yohana aliambiwa asiziandike, ni siri zilizofichwa tangu zamani nazo hazijaandikwa mahali popote katika biblia.

Zipo siri nyingi ambazo hazijulikani  kwamfano “Tutakapofika kwenye utawala wa miaka 1000 ni shughuli gani zitakuwa zinaendelea , na tukienda mbinguni tutakuwa tunafanya nini huko, siri za kwenda kwenye unyakuo na siri za kurudi kwa pili kwa Yesu, kuanguka kwa shetani, na mambo yaliyokuwa yanatendeka kabla ya Adamu kuumbwa nk,(huu ni mfano tu, zinaweza zikawa nyingine tofauti ya hizo au zaidi ya hizo ) .Siri hizi zitakuja kufunuliwa katika wakati huu ambao upo karibu katika mvua hii inayokuja kunyesha.

Ndugu William Branham kabla ya kufariki kwake alionyeshwa na Bwana huu uvuvio mkubwa jinsi utakavyokuja kuwa kiasi kilichomfanya yeye mwenyewe atamani kuwepo katika huo uamsho. Katika hilo ono alionyeshwa uponyaji wa kiungu wa ajabu ukitendeka watu wengi walikuwa wakiponywa kabisa kabisa.

lakini tukisoma

Mathayo 24:14″Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.”

Mstari huu unaelezea jambo litakalofanyika kwanza kabla ya Bwana YESU kurudi, Huu uamsho unaokuja ndio utakaokuwa wa mwisho na utapita duniani kote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote, kwasababu mambo dhahiri na ishara za ajabu zitaonekana kwa watu wote na bibi-arusi naye atakusanyika pamoja kwa ajili ya unyakuo na ndipo ule mwisho utakapokuja.

Ndugu hizi siku zipo karibu, wakati huo utakapofika kama leo haujajiweka tayari kule hautaweza kwasababu zitakuja na hukumu kutoka kwa Bwana, utaishia kupinga na kusema ni vya shetani, kwasababu utasikia mambo ambayo pengine hayajarekodiwa mahali popote kwenye biblia, na hautapata uhakiki wa mambo hayo sehemu yeyote kama hauna ROHO MTAKATIFU kwasababu ni mambo mapya kabisa na hautaweza kupambanua utabakia kuwa mtu wa nia mbili kama unyasi utikiswao na upepo hutajua wapi usimame, ikiwa leo tu huwezi kumtambua yupi nabii wa kweli na yupi nabii wa uongo, utawezaje kuelewa yatakayokuja huko mbele ambapo mambo mapya yatakuja kuhubiriwa??.

Tafakari ndugu tunaishi katika siku za mwisho, ijue kalenda ya Mungu katika maisha yako na wakati tuliopo, usije ukafanana na wale wanawali wapumbavu ambao hawakuwa na mafuta ya ziada katika taa zao. Maana ya yale mafuta ya ziada ni roho ya mafunuo ambayo mkristo wa dini tu hawezi kuwa nayo.

Ndugu kaa ukifahamu Huu uamsho utaanza duniani kote hivi karibuni, na mambo ya ajabu yataenda kutendeka na kuhubiriwa, kwa waovu itakuwa ni hukumu bali kwa wenye haki itakuwa ni kwa kuandaliwa kwa ajili ya unyakuo. Maandalizi ni sasa.

  “Tumeandika makala hii kuwakumbusha bibi arusi wa Kristo wote popote walipo kuwa kuna uamsho mkuu unakuja mbeleni na kuna baadhi ya watumishi wa Mungu waaminifu wachache wamekwisha anza kuonyeshwa katika maono na Bwana Yesu, jinsi utakavyokuwa. Tazama chini shuhuda chache za watu hawa;”

 USHUHUDA WA STEPHEN POWELL’S 

Stephen Powell’s ni muhubiri wa kimarekani hivi karibuni tarehe 21 April 2017. Bwana alimwonyesha maono yafutayo na haya ni maneno yake yaliyonukuliwa;

NEMBO YA VITA ALIYOKUWA NAYO WILLIAM BRANHAM INAACHILIWA TENA.

Kulingana na historia, “NEMBO” (Coat of Arms) ni ishara muhimu ya utaratibu wa urithishaji uliotumika katika zama za kati huko Ulaya, Ilitumika mahususi kama utambulisho katika vita, Nembo zilianzishwa kuashiria ukoo wa familia fulani, urithi, umoja, umiliki, na pia katika taaluma fulani .

Bwana kwasasa anaenda kupitisha NEMBO hii ya thamani sana kwa kizazi chenye utukufu anachokinyanyua  leo duniani!, Mungu anaenda kuachilia uhalali fulani, ujuzi fulani, na urithishwaji katika roho!. Nisikilize kwa makini kitu ninachokwenda kusema sasa…

Hivi karibuni katika mfululizo wa maono niliyopewa, nilichukuliwa mbinguni nikaonyeshwa vitu vingi. Mara ya mwisho nilijikuta nimerudi katika hali yangu ya kawaida nikiwa na akili zangu  juu ya kitanda changu katika hotel moja huko west Virginia. Na nilipokuwa nimelala pale nilisikia BWANA akisema ” NINARUDISHA TENA NEMBO YA VITA ALIYOKUWA AMEIVAA WILLIAM BRANHAM “. Kisha nikaona ono Bwana akishika bega la askari mmoja ambaye kwenye nguo yake kulikuwa na kitu kama NEMBO hivi ingawa sikuweza kuikariri jinsi ilivyokuwa. Kisha  Bwana akaniambia ataenda kuachia vipawa vya miujiza katika mikono ya wana wake na binti zake katika hichi kipindi, kama ilivyokuwa kwa William Branham alivyopewa sio tu kuona maono bali pia kipawa katika viganja vyake.

KIZAZI KIPYA CHA WATENDA-MIUJIZA KATIKA MWENDELEZO WA WILLIAM BRANHAM.

Katika vita askari huwa wanavaa vazi fulani la nje (surcoat) kuzuia dirii isipate kutu. Hichi ndicho nilichokiona usiku ule, na ninaamini NENO la Bwana kuwa ni hili: Bwana anaenda kuendeleza haya katika roho mwaka huu  hapa Marekani na itakuwa ni kwa mwendelezo wa William Branham. Dirii ya huyu mtu haitaendelea kushika kutu itatokea tena kwa mara nyingine Marekani katika huu mwaka, wamekwisha vikwa hawa matenda miujiza wapya ambao wataanza kutenda kazi mwaka huu.

Kama vile Mungu alivyoweka fimbo katika mkono wa  Musa na kumwambia aende kufanya miujiza kule Misri, vivyo hivyo Mungu ataenda kufanya miujiza kupitia mikono ya hawa mashujaa ambao watatokea katika mwendelezo wa William Branham.

Branham alipewa maagizo mwaka 1946, Mungu alimwambia “miujiza itafanyika kupitia mikono yake”. Moja ya hii miujiza ilifanya kazi katika mkono wake wa kushoto na akapewa uwezo wa kupambanua roho hata kuweza kugundua uwepo wa magonjwa ya kipepo au udhaifu. Ishara ya pili aliyopewa ni kipawa cha ajabu cha maono aliweza kutambua siri za mioyo ya watu kwenye mimbari na kuwasaidia watu kuishinda roho ya kutokuamini (kitu ambacho kinazuia miujiza mingi isitendeke hapa Marekani). Mungu aliyafanya haya yote kupitia maisha ya huyu mtu na huduma yake, Hata hapa Marekani Mungu anaenda tena kufanya haya katika wakati wetu. Anaendeleza Nembo iliyokuwa kwa William Branham.

ONYO KWA VIONGOZI WA MAKANISA

Bwana alisema msiwe na mitazamo hafifu juu ya uvuvio unaokuja wa Mungu, kwasababu ikiwa haupo katika sehemu ya huo uamsho, ni rahisi wewe kuingia  katika hatari ya kumruhusu shetani aufanye moyo wako kuwa mgumu kama hautakuwa makini.

“Kuweni makini sana katika huu wakati mchunge laana mnazotoa katika midomo yenu juu ya huo uamsho unaokuja na kuuita kazi ya Mungu kuwa ni ya shetani. Kwasababu hata mafarisayo  walisema maneno hayo hayo japo walikuwa wanauona uwepo dhahiri wa Mungu ukitembea katika dunia. Sio mara zote ni rahisi kufahamu kipi kinatoka kwa Mungu na kipi kinatoka kwa shetani kwahiyo usiwe mwepesi kuhukumu kimakosa huo uvuvi unaokuja. Jinyenyekezeni viongozi wangu, ” Bwana anasema ” Na kwa utulivu hukumuni kazi ya Mungu hichi kipindi kinachokuja, sana sana kama katika kazi za kanisa”

“Kwasababu mimi BWANA nitaijaribu mioyo ya viongozi wangu katika huu uvuvio unaokuja; kwasababu uvivio unaokuja unahitaji kuujaribu uongozi. Mimi BWANA nitafichua siri za mioyo yenu, na kuyakemea mawazo yenu kwa vitu ambavyo hamjawahi kusikia wala msivyovielewa. Lakini kama mkijinyenyekeza  na kuwa wavumilivu  katika hukumu zenu katika hichi kipindi, Mimi Bwana nitawafunulia kazi zangu ni zipi na za shetani ni zipi.

“Mimi Bwana nitawafanya mtambue tofauti kati ya mwanga na giza. Lakini hawatapewa ujuzi huo viongozi wote wenye majigambo na wenye kujikweza na kujidhani kuwa wana mamlaka yote. Hawatapewa watu wanaojiona wanajua vitu vya Mungu. Siri za Mungu hawatapewa watu wale waliowepesi kuhukumu bali wale wanyenyekevu ndio watakaopewa kuzijua hizi siri.

Katika huu uamsho unaokuja kutafunuliwa vitu vya ajabu, siri zilizojificha, na vitu ambavyo huwezi kuvitegemea, Mimi Bwana nitaleta watenda miujiza na sio tu waponyaji, hawa watafanya miujiza ambayo hamjawahi kusikia wala kuona. Lakini msiogope kwa hivyo vitu msivyovielewa, Kwa kuwa mimi Bwana nitakuwa pamoja nanyi nami nitawapa uwezo wa kutambua. Nitaenda kuwasaidia, viongozi wangu, Mitume wangu, Manabii wangu, Wachungaji wangu, lakini muwe wanyenyekevu na msiwe wepesi kuhukumu. Hili ndilo Neno nalowapeni leo kuwaanda ninyi katika huo uvuvio unaokuja.

Love & Blessings,

Stephen Powell,

Lion of Light Ministries.

USHUHUDA WA SADHU SUNDAR SELVARAJ:

Hivi karibuni ndugu Sadhu ambaye ni nabii mwenye asili ya India Bwana amekuwa akimtumia kutoa nabii nyingi na kuja kutimia ikiwemo ushindi wa Obama 2008 na Donald Trump 2016 , mafuriko na matetemeko ya ardhi, mengi pamoja na tetemeko litakalokuja kutokea Calfornia Marekani hivi karibuni,  Alionyeshwa na Bwana Yesu Katika maono kwamba nguvu ya uvuvio iliyokuwepo juu ya nabii William Branham itarejeshwa tena ikiwa na nguvu mara saba”, kwa vijana wadogo ambao Mungu ataenda kuwanyanyua. Bwana alimwonyesha katika maono mengine mengi kuwa nguvu ambayo itaenda kuachiliwa katika huu wakati ukifika itakuwa ni kubwa sana na miujiza isiyokuwa ya kawaida itatendeka alisema. bofya hapa kutazama video .

 Na kuna manabii wengi wameonyeshwa uamsho huo utakao kuja duniani, baadhi yao ni Rick jonyer, Kenneth Hagin, Neville JohnsonVincent selvakumar n.k.

Kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno litathibitika. Katika neema tulionayo sasa hivi umejiwekaje tayari umepokea Roho Mtakatifu?. Jitahidi utubu ndugu injili zinazokuja huko mbele sio za kuwafanya watu watubu tena bali ni kwa ajili ya hukumu na ushuhuda kwa watu tu , wakati wa kutubu ndio sasa, wakati wa kupita katika mlango ulio mwembamba ndio sasa, Tafuta mahusiano yako binafsi na Mungu epuka kamba za madhehebu uwe tayari maana Bwana yupo mlangoni kurudi. Ndugu huu ni wakati wa kukaa chini na kumtafuta muumba wako, kalenda ya Mungu isikupite usilemewe na mambo ya ulimwengu huu, Bwana Yesu alisema tukeshe ili siku hiyo isitujie kama mwivi maana ndivyo itakavyoujia ulimwengu mzima. Kukesha sio kujizuia kulala bali ni kuwa macho rohoni, ujumbe wa Mungu unapokushukia uufahamu. 

Luka 13:23-28″ Mtu mmoja akamwuliza, Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache? Akawaambia, 

24 Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze. 

25 Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana, tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako; 

26 ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu.

 27 Naye atasema, Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu.

 28 Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje”. 

Mungu akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Kwa mawasiliano/Ushauri/kuokoka/Whatsapp. Namba zetu ni hizi

+255693036618/+255789001312


Mada Nyinginezo:

HATUA ZA ROHO MTAKATIFU KATIKA KUTUONGOZA

ACHENI MJUE YA KUWA MIMI NI MUNGU.

NINI MAANA YA HUU MSTARI “NIMEVIPIGA VITA VILIVYO VIZURI, MWENDO NIMEUMALIZA, IMANI NIMEILINDA”?

HISTORIA YA WILLIAM BRANHAM


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2018/07/17/uamsho-mkuu-umekaribia/