VIGEZO VYA KUWA KARIBU NA YESU KRISTO KATIKA ULIMWENGU UJAO.

by Admin | 5 October 2018 08:46 pm10

Wakati raisi wa Marekani Barack Obama alipokuja Tanzania mwaka 2013, japo wengi walifahamu kuwa ni ngumu kuketi meza moja naye au kumpa mkono lakini pamoja na hayo wengi waliona pia itakuwa ni bahati walau wakiuona msafara wake ukipita barabarani, Hilo tu lingewatosha watu kujiona kuwa ni wenye bahati sana kushuhudua tendo kama lile ambalo watu wachache sana wanaweza kuliona. Na mara nyingine unaweza ukafikiria wale watu wanaoongozana naye kila mahali ni watu ambao wamebahatika kuliko watu wote duniani. Kwasababu kiongozi ambaye ni mkubwa na anayeheshimika duniani kote mahali popote atakapokuwepo yupo nao. Kadhalika wewe nawe ungekuwa katika nafasi ile ungejiona kuwa ni mtu uliyebahatika sana (tunazungumza kwa namna ya kidunia).

Lakini biblia inatuambia YESU KRISTO, Ndiye Mfalme ambaye atakuja kuubatilisha ufalme wote wa hii dunia na kisha atauweka UFALME mpya wa milele usioasika, Biblia inasema yeye atakuwa ni MFALME WA WAFALME, na BWANA WA MABWANA. Ataitawala dunia yote kwa fimbo ya chuma, pale dunia wakati huo itakaporejeshwa katika hali yake ya mwanzo ya uzuri, basi chini yake kutakuwa na wafalme wengi na makuhani wengi, na mabwana wengi sana. Kumbuka wakati huo bahari haitakuwepo, kwani tunajua bahari imechukua asilimia 75% ya dunia, sasa bahari ikiondolewa unaweza ukaona kama ni mabara duniani yatakuwa mangapi?, kadhalika majangwa nayo hayatokuwepo, na wala hakutakuwa na sehemu yoyote ya dunia itakayokuwa ukiwa, sehemu zote zitakuwa zimejaa utukufu wa Mungu na wanadamu.

Kama biblia inavyosema Mfalme wetu YESU KRISTO atatawala na watakatifu wake kwa kipindi cha miaka 1000, kabla ya ule umilele kuanza. Unafahamu sasahivi Kristo ameketi katika kiti cha neema kama mkombozi lakini atakaporudi mara ya pili, sura yake itabadilika hatakuwa tena kama Yesu mwokozi bali YESU MFALME?. Na kama ni mfalme basi na tabia zile zote za kifalme ni lazima ziambatane naye. Na Ndio maana Mungu aliruhusu kwanza tupitie kuziona falme za ulimwengu huu, walau kwa sehemu tupate picha juu ya ule ufalme usiokuwa na mwisho utakavyokuja kuwa huko mbeleni.

Wengi wetu tunadhani, tukienda mbinguni basi watu wote watakuwa sawa kisha tutakuwa usiku na mchana tunamwimbia tu Mungu kama vile malaika. Lakini hiyo sio kweli, huko tunapokwenda biblia inatuambia kuna UFALME, na kuna MBINGU mpya na NCHI mpya. Ikiwa ni Ufalme basi kuna kutawala na kutawaliwa. Na kama vile watu wa ulimwengu huu wanavyoupigania ufalme mpaka waupate, kadhalika na ufalme wa mbinguni unapiganiwa, vinginevyo nguvu yako ikiwa ni ndogo kule hutatawala bali utatawaliwa (hapa tunawazungumzia waliookolewa, na sio watu wote, hao wenye dhambi wakati huo watakuwa katika ziwa la moto).. Na ndio maana Bwana YESU alisema.

Mathayo 11: 12 “Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka”.

Unaona hapo?. Kuwa na uhakika wa kwenda mbinguni tu hautoshi, bali nafasi utakayokwenda kuwa nayo huko, na aina gani?

Na tena sasa baada ya wanafunzi wake kulisikia hilo, wakijua ya kuwa Kristo ndiye atakayekuwa mmilika wa ufalme wa Mungu, wawili kati ya wanafunzi wake walimwendea kwa siri na kumwomba wafanyiwe jambo kama tunavyosoma katika..

Marko 10: 35 “Na Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, wakamwendea, wakamwambia, Mwalimu, twataka utufanyie lo lote tutakalokuomba.

36 Akawaambia, Mwataka niwafanyie nini?

37 Wakamwambia, Utujalie sisi tuketi, mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika utukufu wako.

38 Yesu akawaambia, Hamjui mnaloliomba. Mwaweza kunywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi?

39 Wakamwambia, Twaweza. Yesu akawaambia, Kikombe ninyweacho mimi mtakinywea, na ubatizo nibatizwao mimi mtabatizwa;

40 lakini habari ya kuketi mkono wangu wa kuume au mkono wangu wa kushoto si langu kuwapa, ila wao watapewa waliowekewa tayari.

41 Hata wale kumi waliposikia wakaanza kuwakasirikia Yakobo na Yohana”.

Unaona hapo, mfano tu leo hii raisi wa hii nchi angekuwa na rafiki zake wawili ambao tangu zamani walijua kuwa atakuja kuwa raisi, ni wazi kuwa wangemwomba mmojawao awe makamu wake na mwingine waziri mkuu, lakini Raisi asingeweza kuwaambia neno “sawa” kirahisi rahisi tu, ni wazi kuwa yapo masharti yangepaswa wayafuate kutoka kwa raisi tangu kipindi kile kile ambacho kabla hajawa hata Raisi, pengine angewaambia, mkiwa na mimi katika kampeni zangu zote na kunipigia debe, ndipo nitawafanya wote kuwa hivyo, au wahakikishe siku zote wanamletea taarifa zote za maadui zake, kadhalika kwenye shida zote zitakazojitokeza wawe pamoja naye na zaidi ya yote wawe na angalau na ujuzi Fulani au maarifa Fulani kuhusiana na hayo mambo ya uongozi…Hivyo wakishinda hivyo vigezo, ule wakati ukifika basi atawafanya kuwa viongozi..

Kadhalika na kwa Bwana wetu Yesu Kristo, tunaona wanafunzi wake wawili walimfuata na kumwomba jambo gumu kama lile, kwamba katika ufalme wake awajalie mmoja aketi mkono wake wa kuume na mwingine wa kushoto, lakini yeye akawaambia je! KIKOMBE nikinyeacho mtakinywea?, kadhalika UBATIZO nibatizwao mtabatizwa??.

Hilo ni swali tunauliza hata sisi tunaotamani siku ile YESU KRISTO akiwa kama MFALME atatumbue kama watu wake wa karibu sana wenye heshima kubwa katikati ya wingi wa watakatifu na malaika watakaokuwepo siku zile atakapokuja kutawala dunia…JE! KIKOMBE nikinyeacho mtakinywea?, JE! UBATIZO nibatizwao mtabatizwa??.

Kwa maneno mepesi ni wazi kuwa kila mtu atatamka, Ndio nitaweza! Kama vile wale Yakobo na Yohana walivyotamka,,..Lakini Bwana kwa kuwa alikuwa anajua waliombalo akawaambia ni kweli mnaweza kufanya hivyo lakini yeye hawezi kutamka kuwa mtaketi naye isipokuwa wale Baba aliowaweka tayari..Kuna lugha nyepesi tunaweza kusema “wale ambao Mungu atawapa neema kunywea kukombe kama cha kwake, na kubatizwa ubatizo kama wa kwake hao ndio watakaoketi pamoja naye katika ufalme wake.”.

Swali Kikombe ni nini? Na Ubatizo ni upi?

Kikombe, kama wengi tunavyojua ni mateso kwa ajili ya ushuhuda ulionao, kama tunavyomwona Bwana wetu Yesu alivyopitia yale mateso Makali kama yale mpaka kufikia kufa, kwa kuliona lile kwa uchungu mwingi akatamani hata mateso yale yamwepuke, lakini Mungu alimpa nguvu ya kuyashinda…

Mathayo 26: 39 “Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe”.

Lakini UBATIZO ule unaozungumziwa pale haukuwa ubatizo wa maji tena hapana, kwani alikuwa ameshabatizwa wakati huo aliokuwa anazungumza hayo maneno.

Luka 12: 49 “Nimekuja kutupa moto duniani; na ukiwa umekwisha washwa, ni nini nitakalo zaidi?

50 LAKINI NINA UBATIZO UNIPASAO KUBATIZIWA, nami nina dhiki kama nini hata utimizwe! “

Kama tunavyofahamu neno Kubatizwa ni kuzamwishwa/kuzikwa, tunapobatizwa ni ishara ya kuwa tunakufa na kufufuka na Kristo katika ubatizo wake. Na ndio maana tunasoma katika

Warumi 6: 3 “Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake?

4 Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.”

Kwahiyo kama tunavyoona hapo ubatizo  Yesu Kristo aliokuwa anauzungumzia hapo ni kile kitendo cha KUFA, KUZIKWA, na KUFUFUKA. Huo ndio ubatizo aliokuwa anaungojea.

Lakini leo hii tunaona wengi tunapenda kumfuata Yesu lakini kuingia gharama hatutaki, Bwana Yesu alisema mtu hawezi kuwa mwanafunzi wangu kama asipoacha vitu vyote na kubeba msalaba wako na kunifuata, na pia kama yeye alivyoutoa uhai wake kwa ajili yetu, na sisi pia imetupasa kutoa uhai wetu kwa ajili ya Kristo , na pia maandiko yanasema hatujapewa kumwamini tu, bali hata kuteswa kwa ajili yake. Njia hiyo hiyo ya msalaba ya kudharauliwa ndiyo iliyowafanya Bwana wetu Yesu Kristo kuwa MFALME,

Waebrania 12: 2 “tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake ALIUSTAHIMILI MSALABA NA KUIDHARAU AIBU, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.

3 Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu”.

kadhalika pale itupasapo kupitia hayo, basi tujue kuwa Mungu ametuchagua kumkaribia yeye katika ufalme wake, ili siku ile na sisi tuwe na jina mbele zake. Kwanini mitume hawakuona ni kitu kuuliwa kwa ajili ya Kristo ni kwasababu walitamani kumkaribia Kristo katika ufalme wake.

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2018/10/05/vigezo-vya-kuwa-karibu-na-yesu-kristo-katika-ulimwengu-ujao/