ITAMBUE KARAMA YA MUNGU.

by Admin | 27 October 2018 08:46 pm10

Bwana Mungu wetu kaumba vitu vyote vya mwilini, kufunua vitu vya rohoni, aliumba milima, kufundisha kuwa kuna milima ya rohoni, aliumba maji kuonyesha kwamba kuna maji ya rohoni, aliruhusu mauti iwepo kufunua kwamba kuna mauti ya kiroho,aliruhusu vyakula viwepo ili kufunua kwamba kuna vyakula vya rohoni, kwasababu mwanadamu ameumbwa katika pande mbili, rohoni na mwilini. Na ndio maana alisema kwenye Neno lake Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu (Mathayo 4:4)”.

Hivyo kama kuna mauti ya mwilini, ni wazi kuwa ipo pia mauti ya rohoni. Na kama vile, mauti ya mwilini ilivyo na nguvu leo, kiasi kwamba kila nafsi lazime ipitie, vivyo hivyo mauti ya rohoni ina nguvu ile ile ambayo inalazimisha kila kiumbe kife kwa namna ya roho. Na hii mauti ya rohoni iliingia pale Edeni, Adamu na Hawa walipoasi. Na kama tunavyojua leo hii hakuna dawa ya kifo cha mwilini, Kifo ni kifo tu! Vivyo hivyo na dawa ya Kifo cha rohoni haikuwepo mpaka njia ya mti wa uzima YESU KRISTO ALIPOFUNULIWA. Ndio tiba ya kifo ikapatikana vinginevyo hakungekuwa na uzima wa milele kwa kiumbe chochote kile.

Kwahiyo mara nyingi Bwana anapenda kutufundisha kwa kutumia mifano ya mwilini, kufunua vitu vya rohoni, kwamfano tunamwona yule mwanamke msamaria siku moja alipokwenda kisimani kuteka maji akakutana na Bwana, na Bwana akamwomba maji, na yule mwanamke alipotaka kuanza maandalizi ya kumpatia maji kutoka katika kisima kile, kwa kumuuliza baadhi ya maswali,Bwana alimkatisha palepale na kumwambia… “ kama ungaliijua KARAMA YA MUNGU, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, UNGALIMWOMBA YEYE, NAYE ANGALIKUPA MAJI YALIYO HAI (Yohana 4:10)”

Na palepale yule mwanamke alidhani Bwana anazungumzia habari za maji yale ya mwilini ya kwenye kwenye visima, akafurahi akatamani apewe yale maji. Tunaweza kuona mistari hiyo tuone jambo..

“11 Yule mwanamke akamwambia, Bwana, huna kitu cha kutekea, na kisima ni kirefu; basi umeyapata wapi hayo maji yaliyo hai.

12 Je! Wewe u mkubwa kuliko baba yetu, Yakobo, aliyetupa kisima hiki, naye mwenyewe akanywa maji yake, na wanawe pia, na wanyama wake?

13 YESU AKAJIBU, AKAMWAMBIA, KILA ANYWAYE MAJI HAYA ATAONA KIU TENA;

14 walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi HATAONA KIU MILELE; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, YAKIBUBUJIKIA UZIMA WA MILELE.

15 Yule mwanamke akamwambia, Bwana, unipe maji hayo, nisione kiu, wala nisije hapa kuteka”

Unaona hapo, Bwana anazidi kumtoa yule mwanamke Msamaria kwenye mawazo ya maji ya mwilini na kumpeleka kwenye mawazo ya maji ya rohoni, lakini bado alikuwa hajamwelewa. Alijaribu kutumia mfano wa maji ya mwilini ili kumwonyesha umuhimu wa maji ya rohoni lakini bado hakumwelewa vizuri mpaka baadaye kidogo. Alijaribu kumfunulia KARAMA YA MUNGU lakini bado ilimuwia ngumu kumuelewa kwa wakati ule kwasababu ya mapokeo ya kibinadamu aliyokuwa nayo. Bwana alichotaka kwa yule mwanamke ni KUTUBU, NA KUACHA DHAMBI ALIZOKUWA ANAZIFANYA, NA KUMGEUKIA MUNGU kwa moyo wake wote! Na kuishi maisha mapya yanayompendeza Mungu Hicho tu! ndio Bwana alichokuwa anatafuta kwa yule mwanamke. Hiyo ndiyo KARAMA YA MUNGU aliyokuwa anataka kumpa yule mwanamke…ili asife kwa kukosa maji ya uzima akaukosa uzima wa milele..Na ndio maana biblia inasema katika..

Warumi 6:23 “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; BALI KARAMA YA MUNGU ni UZIMA WA MILELE katika Kristo Yesu Bwana wetu”.

Na baada ya Bwana kumfunulia siri ya moyo wake kwamba anao waume watano na yule aliyenaye sasa si wake, ndipo alipotambua kwamba yeye ni mwenye dhambi, na kwamba Bwana alikuwa hazungumzii maji ya mwilini bali ya roho yake, yatakayompa uzima wa milele.

Tunaweza tukajifunza tena mfano mwingine katika maandiko wa Mtu aliyeielewa haraka KARAMA YA MUNGU pasipo Bwana kutumia nguvu nyingi kumfafanulia, na huyu si mwingine zaidi ya Petro. Wakati Fulani Bwana alimwendea Petro kwa mara ya kwanza kama alivyomwendea yule mwanamke Msamaria, akamkuta anaosha nyavu, kwasababu wamefanya kazi ya kuchosha usiku mzima bila kupata kitu, Na Petro alipomwona Bwana alidhani ni muhubiri tu wa kawaida, mwalimu wa torati kama walimu wengine, hivyo kwa heshima yake akaona bora amtii tu, Tunasoma hayo katika..

Luka 5: 4 “Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki.

5 Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.

6 Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika;

7 wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama.

8 Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, ONDOKA KWANGU, KWA KUWA MIMI NI MTU MWENYE DHAMBI, BWANA.

9 Maana alishikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi wa samaki walioupata”;

Unaweza ukaona hapo, Petro baada ya kuiona ile ishara ya kupata samaki wengi namna ile, akatambua KARAMA YA MUNGU nyuma ya ile ishara, akatambua kuwa mtu aliyesimama mbele yake ni MKUU WA UZIMA, na yeye ni mtakatifu na hachangamani na uchafu, akaogopa akamwangukia chini akamwambia “ONDOKA KWANGU, KWA KUWA MIMI NI MTU MWENYE DHAMBI, BWANA” alitambua Bwana Yesu hakuja kumpa yeye VIKAPU VYA SAMAKI, hakumfanyia ile ishara ili kumfanya yeye kuwa milionea, bali aliifanya ile ishara ili kumwonyesha Petro kwamba yeye ni mwenye dhambi kiasi gani na kwamba anahitaji UZIMA WA MILELE. Bwana hakumfanyia ile ishara Petro kwasababu anavutiwa sana na ile kazi aliyokuwa anaifanya ya kuvua samaki, hapana alimfanyia Petro ile ishara kwasababu aliona dhambi ndani ya Petro na hakutaka Petro apotee, Na Petro alilitambua hilo akatubu mbele zake.

Na jambo hili hili linaendelea leo, Bwana Yesu anakutembelea kwenye mambo yako unayoyafanya, labda shughuli Fulani ya kujipatia kipato, au labda elimu, au mali, au afya…Inatokea umepitia au ulipitia hali Fulani ulikuwa unaugua sana na Bwana akakuponya kimiujiza, na ndani ya moyo wako ukashuhudiwa kuwa ungestahili kufa lakini umepona… Sasa huu si wakati wa kuanza kutazama mambo ya mwilini, kwamba sasa umepata afya ndio wakati wa kusaka fedha kwa nguvu uwe tajiri kwasababu Mungu kakunyanyua tena, au ukadhani kwamba Bwana alikuponya kwasababu alikuhurumia sana ulipokuwa unateseka na maumivu ya magonjwa yako,

Nataka nikwambie ndugu Bwana hakukuhurumia kwasababu ulikuwa unateseka na maumivu ya ugonjwa bali alikuhurumia akakuponya kwasababu alikuhurumia usije ukafa na dhambi ulizo nazo ndani yako na ukaingia kwenye lile ziwa la moto hivyo ni muhimu sana kuielewa KARAMA YA MUNGU juu maisha yako? Bwana alikuponya kimiujiza ili UKATUBU, ukaache uasherati, ukaache anasa, ukaache usengenyaji, ukaaache rushwa,ukaache kuishi na mume au mke ambaye hamjafunga ndoa, ukaache kuiba, ukaache pombe, alikuponya magonjwa ya zinaa ili ukaache uasherati na uzinzi n.k

Bwana hakukufanikisha kwenye kazi yako ya kujipatia kipato, kwasababu anataka sadaka au fungu la kumi kutoka kwako, au kwasababu alikuhurumia sana ulikuwa maskini kwa muda mrefu na ulikuwa unateseka hapana!! Bwana alikufanikisha kwenye shughuli zako kwasababu anaona maisha yako kuna sehemu pengine hayajakamilika mbele zake, anakufanyia ishara kubwa namna hiyo kama alivyomfanyia Petro, anataka UANGUKE CHINI utambue kwamba, Jicho la Mungu linakutazama kuliko unavyodhani, mambo yako na dhambi zako za siri anayoana kuliko unavyofikiri, ziko wazi mbele zake, anataka uone kwamba MTAKATIFU WA WATAKATIFU AMEKUSOGELEA, Anataka uone kwamba hatua moja mbele yako kasimama mtu asiyechangamana na dhambi. Na anataka akupatie uzima wa milele!

Biblia inasema mtu asipozaliwa mara ya pili hawezi kuuona ufalme wa mbinguni, (Yohana 3:3). HIYO NDIYO KARAMA YA MUNGU KWAKO.

Bwana Azidi kukubariki sana, Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

KARAMA ILIYO KUU.

MOYO ULIOELEKEA KWA MUNGU.

MTUME PAULO ALIKUWA NA MAANA GANI KUSEMA NIKAKUFA KILA SIKU??

MBONA MUNGU ANARUHUSU WATU WAPATE SHIDA, ILHALI ANA UWEZO WA KUTUEPUSHA?


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2018/10/27/itambue-karama-ya-mungu/