SADAKA ILIYOKUBALIKA.

by Admin | 5 December 2018 08:46 am12

 

SADAKA ni moja ya maagizo muhimu sana, na yanayobeba Baraka nyingi sana kwa Mtu, kama ikitolewa kulingana na Neno na kwa Hiari ya mtu pasipo kulazimishwa au kusukumwa na mazingira Fulani. Lakini sadaka hiyo hiyo isipotolewa jinsi inavyopaswa inaweza ikaleta LAANA kubwa sana, badala ya Baraka. Kwasababu biblia inasema katika..Mithali 15:8 “Sadaka ya mtu mbaya ni CHUKIZO KWA BWANA; Bali maombi ya mtu mnyofu ni furaha yake”.

Biblia inaposema mtu mbaya ina maana gani?

Mtu yeyote Yule ambaye haishi kulingana na Neno la Mungu, mtu huyo ni mbaya mbele za Mungu. Mtu yeyote anayejua kuwa kufanya jambo Fulani ni dhambi na bado analifanya mtu huyo ni mbaya mbele za Mungu. Mtu yoyote anayejua uasherati ni dhambi na bado anaufanya, mtu yeyote anayejua rushwa ni dhambi na bado anatoa au anapokea, mtu yeyote anayejua usengenyaji ni dhambi na bado anasengenya, mtu yoyote anayejua kuwa matusi ni dhambi na bado anatukana mtu huyo mbele za Mungu ni mtu Mbaya,

Mtu yoyote anayejua ulevi, anasa, wizi ni mbaya na bado anafanya mambo hayo mtu huyo ni mbaya mbele za Mungu, Na hivyo sadaka zake ni MACHUKIZO MAKUBWA MBELE ZA MUNGU. Apatapo chochote kwa njia hizo na kuzipeleka Madhabahuni kwa Bwana sadaka yake mtu huyo ni MACHUKIZO, na hivyo atakuwa ameenda kujitafutia laana badala ya Baraka. Kwahiyo kwake linakuwa ni chukizo litakalomletea Uharibifu wake mwenyewe. Biblia inasema katika..

Kumbukumbu 23: 17 “PASIWE NA KAHABA KATIKA BINTI ZA ISRAELI, wala pasiwe na HANITHI katika wana wa Israeli wanaume.

18 USILETE UJIRA WA KAHABA, wala mshahara wa mbwa, katika nyumba ya Bwana, Mungu wako, kwa ajili ya nadhiri yo yote; KWANI HAYA NI MACHUKIZO KWA BWANA, MUNGU WAKO, YOTE MAWILI”.

Unaona hapo! Bwana alikataza sadaka zozote, zitokanazo na njia zilizo nje ya Neno lake, zisifike kabisa nyumbani mwake.

Watu wanapokosa shabaha ni kufikiri kuwa Ukristo ni kwenda kanisani na kutoa sadaka, basi au kusaidia wajane na mayatima…Hawajui kuwa Ukristo ni zaidi ya hapo. Kumpendeza Mungu sio kumpa yeye sehemu ya mali yako na kuishi maisha unayotaka..Hapana Mungu sio mfanya biashara kwamba anakutafuta wewe ili apate kitu kwako, wala sio mwana-Hisa kwamba anawekeza kwetu ili baadaye apate kitu kutoka kwetu. Yeye mwenyewe anasema Dunia yote ni yake, sasa ana haja na kitu gani? Bwana Yesu alisema maneno haya..

Mathayo 9: 13 “Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, NATAKA REHEMA, WALA SI SADAKA;”

Na pia anasema katika Waebrania 10:6

“Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo;

7 Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) NIYAFANYE MAPENZI YAKO, MUNGU.”

Unaona hapo? Bwana anachotaka kutoka kwetu ni REHEMA, yaani anataka mtu atubu, asafishike na kuwa msafi kweli kweli anayekubaliwa na Mungu, atende mapenzi ya Mungu…Hiyo ndio sadaka inayompenda Mungu.

Wakati Fulani Mfalme Sauli alipewa maagizo kutoka kwa Bwana akawaangamize jamii ya watu Fulani, aangamize na mifugo yao yote na kila kitu, ili kutimiza kisasi cha Bwana juu ya hao watu, lakini Sauli hakufanya vile, hakuitii sauti ya Mungu kwa kuangamiza kila kitu, na badala yake akamuacha mfalme wao hai, na akachukua wale ng’ombe walionona ili akamtolee Mungu wa Israeli sadaka zile mambo ambayo Mungu alimkataza asiyafanye.. Kwa mawazo yake alijua Mungu atamheshimu na kumpenda kwasababu amemletea sehemu zilizonona za nyara za Maadui zao. Lakini mambo yalimbadilikia mbeleni alipokutana na Samweli nabii wa BWANA…

1 Samweli 15: 20 “Sauli akamwambia Samweli, Hakika mimi nimeitii sauti ya Bwana, nami nimemleta Agagi, mfalme wa Waamaleki, tena nimewaangamiza Waamaleki kabisa.

21 Ila watu waliteka nyara, kondoo na ng’ombe walio wazuri, katika vitu vilivyowekwa wakfu, KUSUDI WAVITOE DHABIHU KWA BWANA, MUNGU WAKO, huko Gilgali.

22 Naye Samweli akasema, JE! BWANA HUZIPENDA SADAKA ZA KUTEKETEZWA NA DHABIHU SAWASAWA NA KUITII SAUTI YA BWANA? Angalia, KUTII NI BORA KULIKO DHABIHU, NA KUSIKIA KULIKO MAFUTA YA BEBERU.

23 Kwani KUASI NI KAMA DHAMBI YA UCHAWI, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme”.

Kwa kosa hilo moja tu! Sauli alipoteza ufalme wake, na Mungu alimwacha tangu siku ile. Kwasababu hakuwa mtii mbele za Mungu na badala yake akadhani kuwa uhusiano wake yeye na Mungu haujalishi sana, bali kinachojalisha ni kiasi gani cha sadaka anachomtolea.

Mahali pengine Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake..

Mathayo 5: 23 “Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, NA HUKU UKIKUMBUKA YA KUWA NDUGU YAKO ANA NENO JUU YAKO,

24 Iache Sadaka Yako Mbele Ya Madhabahu, Uende Zako, Upatane Kwanza Na Ndugu Yako, Kisha Urudi Uitoe Sadaka Yako”.

Unaona! Unaweza ukawa tayari umeshajiandaa kutoa sadaka yako kwenye madhabahu ya Mungu, lakini ndani ya moyo wako kuna mtu mmegombana, au kuna mtu umemkosea, au kuna mtu umemsengenya au kitu kilicho kibaya umekifanya, Bwana Yesu anatuonya Nenda kwanza kapatane na ndugu yako kisha ndipo uje utoe ile sadaka,.. Lakini tusipofanya hivyo na kuitoa ile sadaka.. yatakukuta kama yaliyomkuta Mfalme Sauli. Badala ya kupokea Baraka unapokea Laana. Badala ya kuinuliwa unashushwa.

Hivyo maisha yetu matakatifu ndio sadaka ya kwanza Mungu anayoitaka katika maisha yetu, ukiwa mwasherati tubia kwanza uasherati wako kwa kumaanisha kuuacha kwasababu maana ya kutubu sio kuomba msamaha tu! Bali ni KUGEUKA ndipo ukamtolee Mungu sadaka yako, ukiwa mlevi tubia kwanza ulevi wako kwa kumaanisha kuuacha kabisa ndipo ukamtolee Bwana sadaka zako, na vivyo hivyo mambo mengine yote yaliyo nje na Neno lake unayoyafanya. Yaache kwanza ndipo ufikirie suala la Sadaka..

Isaya 1: 11 “Huu wingi wa sadaka zenu mnazonitolea UNA FAIDA GANI? Asema Bwana. Nimejaa mafuta ya kafara za kondoo waume, na mafuta ya wanyama walionona; nami siifurahii damu ya ng’ombe wala ya wana-kondoo wala ya mbuzi waume.

12 Mjapo ili kuonekana mbele zangu, ni nani aliyetaka neno hili mikononi mwenu, kuzikanyaga nyua zangu?

13 MSILETE TENA MATOLEO YA UBATILI; uvumba ni chukizo kwangu; mwezi mpya na sabato, kuita makutano; SIYAWEZI MAOVU HAYO NA MAKUTANO YA IBADA.

14 Sikukuu zenu za mwezi mpya na karamu zenu zilizoamriwa, NAFSI YANGU YAZICHUKIA; MAMBO HAYO YANILEMEA; NIMECHOKA KUYACHUKUA.

15 Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu nisiwaone; naam, mwombapo maombi mengi, sitasikia; mikono yenu imejaa damu.

16 JIOSHENI, JITAKASENI; ONDOENI UOVU WA MATENDO YENU USIWE MBELE ZA MACHO YANGU; ACHENI KUTENDA MABAYA;

17 JIFUNZENI KUTENDA MEMA; TAKENI HUKUMU NA HAKI; WASAIDIENI WALIOONEWA; MPATIENI YATIMA HAKI YAKE; MTETEENI MJANE.”

Neema ya Bwana Yesu Kristo izidi kuwa nawe.

Ubarikiwe sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2018/12/05/sadaka-iliyokubalika/