NJIA YA BWANA INATENGENEZWA WAPI?

by Admin | 1 January 2019 08:46 pm01

Kabla Bwana YESU kuanza huduma yake ya wokovu hapa duniani, Ilimpendeza Mungu amtangulizie kwanza mtu atakayemwandalia mazingira mazuri ya yeye kufanyia huduma yake, mtu atakayemtengenezea njia ya kupendeza iliyonyooka ili apate kupita juu yake. Mungu hakuona vema mwanawe mpendwa afanye kazi katika mazingira ambayo hayajaandaliwa kwa namna yoyote, hivyo kwa hekima zake nyingi akaona ni vema amtangulize kwanza mtu atakayeanza kuzungumzia habari za kuja kwake kabla ya yeye kufika, kusudi kwamba atakapofika watu wawe tayari kumpokea kwa furaha, kadhalika awe mtu atakayeigusia habari ya injili ambayo yeye atayaokuja kuihubiri mbeleni na ndio hapo tunakuja kumuona Yohana mbatizaji akihubiri habari za ubatizo na toba pamoja na ufalme wa mbinguni mambo ambayo hayakujulikana na wayahudi hapo mwanzo.

Na injili hiyo hiyo ya ufalme wa mbinguni ndiyo YESU aliyoanzana nayo katika huduma yake. Jambo lililomfanya Yohana kuonekana mtu MKUU sana katika ufalme wa mbinguni kuliko hata wote waliomtangulia katika agano la kale. Kwasababu yeye pekee ndiye aliyefanikiwa kumtengenezea Mungu NJIA ya kutembelea hapa duniani hakukuwa na mwingine yeyote aliyefanikiwa kufanya vile au kufikia viwango vile kabla yake.

Marko 1: 1 “Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.

2 Kama ilivyoandikwa katika nabii Isaya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, ATAKAYEITENGENEZA NJIA YAKO.

3 Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake.

4 Yohana alitokea, akibatiza nyikani, na kuuhubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi.

5 Wakamwendea nchi yote ya Uyahudi, nao wa Yerusalemu wote, wakabatizwa katika mto wa Yordani, wakiziungama dhambi zao.

6 Na Yohana alikuwa amevaa singa za ngamia na mshipi wa ngozi kiunoni mwake, akala nzige na asali ya mwitu”.

Lakini swali la kujiuliza hapo ni kwanini Yohana alionekana kuwa ni mtu azungumzaye kutoka NYIKANI. Tunapaswa tujue maana ya maisha yake ya nyikani na jangwani, ili kwamba tufahamu ni kitu gani kilichompelekea awe mtu wa namna ile, kumbuka Mungu huwatumia manabii wake kuwa ISHARA kwa ajili ya Neno lake ili kufunua mambo ya rohoni. Sasa kama tukisoma Isaya 40:3 inasema..

Isaya 40:3 “Sikiliza, ni sauti ya mtu aliaye, ITENGENEZENI NYIKANI njia ya Bwana; NYOSHENI JANGWANI njia kuu kwa Mungu wetu.

4 Kila bonde litainuliwa, Na kila mlima na kilima kitashushwa; Palipopotoka patakuwa pamenyoka, Na palipoparuza patasawazishwa;

5 NA UTUKUFU WA BWANA UTAFUNULIWA, Na wote wenye mwili watauona pamoja; Kwa kuwa kinywa cha Bwana kimenena haya.”

Unaona hapo?. Isaya anasema NJIA YA BWANA haitengenezwi mahali pengine popote isipokuwa nyikani, kadhalika NJIA KUU YAKE hainyooshwi mahali pengine popote isipokuwa jangwani..Hivyo JANGWANI na NYIKANI ni mahali ambapo njia ya Bwana inapotengenezewa..

Na ndio maana tunaomwona mtu kama Yohana Mungu alimtumia kama ishara ya wazi kuwa mtu wa majangwani na nyikani kuonyesha kuwa huko ndiko Njia ya Mungu inapotengenezewa..Yeye aliufahamu ujumbe huo ambao nabii Isaya aliuhubiri kwa miaka zaidi ya 700 iliyopita, akajua hilo Neno si la mtu Fulani pekee tu, bali ni kwa yeyote atakayeliishi, na hilo Neno linaishi kwa kila kizazi na ndio maana utamwona japo Yohana alikuwa ndiye mtu aliyemtengenezea Bwana njia lakini bado aliwahubiria watu na makutano kuwa wao nao WAMTENGENEZEE BWANA NJIA YA KUSHUKIA..

Ukiendelea kusoma hapo katika Isaya utaona inasema:

“4 Kila bonde litainuliwa, Na kila mlima na kilima kitashushwa; Palipopotoka patakuwa pamenyoka, Na palipoparuza patasawazishwa;

5 NA UTUKUFU WA BWANA UTAFUNULIWA, Na wote wenye mwili watauona pamoja; Kwa kuwa kinywa cha Bwana kimenena haya.”

Sasa mabonde yanayozungumziwa hapo ni mabonde yote yanayoweza kukwamisha kusudi la Mungu lisifunuliwe kwa watu wake kupitia wewe, hayo yote yataondolewa si pengine zaidi ya jangwani na nyikani, milima yote, na makando kando yote yanayoweza kukwamisha utukufu wa Mungu usifunuliwe juu ya watu wote yataondolewa pale tu mtu atakapokubali kuipitia njia ya nyikani na jangwani.

Kumbuka wana wa Israeli wasingeweza kumjua Mungu wa Yakobo ni nani na anataka nini katika maisha yako kama ingekuwa ni kutoka tu Misri na moja kwa moja kufika Kaanani, japo waliuona kweli mkono wa Mungu ukiwapigania na kuwashindania dhidi ya maadui zao, kwa ishara nyingi na miujiza mingi lakini bado wangefika nchi ya ahadi pasipo kumjua Mungu wanayemtumikia. Iliwapasa kwanza wapitie njia ya JANGWA NA NYIKA muda mrefu ili Mungu awape amri zake na sheria zake. Iliwapasa wapitie kule ili Mungu aondoe vinyago vilivyokuwa ndani ya mioyo yao. Walikaa nyikani mbali na mataifa mengine kwa muda mrefu wakilishwa tu mana siku zote walizokuwa kule jangwani. Mungu hakuwaruhusu wafanye biashara yoyote na mataifa ya pembeni, wala shughuli zozote za kimaisha, yeye pekee ndiye aliyekuwa anawalisha mana. Aliwatenga mbali sana na tamaa za ulimwengu na macho mahali ambapo ukiangalia mkono wa kulia huoni miji wala majengo mazuri isipokuwa milima na mabonde tu kwa muda wa miaka mingi, mahali pakame sana, walisahau anasa na vitu vitamaniwavyo vya ulimwengu huu, Mungu aliwaua kwa habari ya dunia, aliwanyenyekeza kiasi kwamba vile viburi walivyotoka navyo Misri hawakuingia navyo Kaanani.

Na huko ndiko walipotoka na sheria na kanuni za kutembea na Mungu katika hiyo nchi waliyokuwa wanaiendea. Huko ndipo walipomtengenezea Mungu NJIA KUU ya kutembelea kwa utukufu wake.

Milima yote ya kiburi ilishushwa kule jangwani, mabonde yote ya ouvu yalisafishwa walipokuwa kule jangwani. Walipokuwa wanasua sua kwa kutokumwamini Mungu walitengenezwa upya Hivyo walipokuwa wakiingia katika nchi ya ahadi walikuwa tayari kwa kumtumikia Mungu na kwa kupitia wao MUNGU KUONYESHA UTUKUFU WAKE KWA MATAIFA YOTE YA DUNIA NZIMA.

Mwangalie Musa, mwanzoni alidhani kuwa anaweza kuwaokoa wana wa Israeli,kwa siasa na elimu yake na cheo chake alichokuwa nacho Misri, lakini haikuwa hivyo badala yake ndio alijitafutia matatizo, mpaka pale alipokimbilia jangwani huko nchi isiyokuwa na raha zile alizokuwa anazipata katika jumba la kifalme Misri, na kukaa huko muda mrefu kumtafakari na kuulizia juu Mungu wa baba yake Ibrahimu. Mungu alimtweza huko kwa muda wa miaka 40, akiiua ile asili ya kidunia iliyokuwa ndani yake, akiishusha milima yote ya majivuno iliyokuwa imejificha ndani yake, akitoa elimu yake ya kipagani iliyokuwa imeujaza moyo wake kwa muda wa miaka 40 alikuwa anamwandalia tu Mungu njia ya kupitia, mpaka pale alipokamilishwa biblia inasema alikuwa ni mjuzi wa usemi na kunena [mwanasiasa mzuri] (Matendo 7:22) lakini alipokutana na Bwana hata ule ujuzi wake wa kuongea hakuwa nao tena ndani yake ulishakufa, Bwana pia anamshuhudia Musa na kusema kuwa yeye ndio alikuwa mtu MPOLE kuliko wote duniani(Hesabu 12:3), jaribu kufikiria jambo hilo, utagundua kuwa kutembea na Mungu au kuwa karibu na Mungu sio kiwango cha upako ulichonacho, hapana bali ni jinsi gani moyo wako umeandaliwa katika kanuni azitakazo yeye. Sasa baada ya Musa kufikia viwango hivyo ndipo UTUKUFU WA MUNGU ULIPOFUNULIWA JUU YAKE. NA WATU WOTE WAKAUONA.

Mambo yanatupa mwongozo gani katika Roho?.

Kumbuka Wana wa Israeli katika mwili ndio sisi(Wakristo) katika roho. Kwasababu hata Bwana wetu aliandikiwa hivyo..katika Mathayo 2:15 ikisema…Kutoka Misri nalimwita mwanangu..Unaona maneno hayo yalikuwa ni ya wana wa Israeli, baadaye yakaja kuwa ya Bwana wetu Yesu Kristo kadhalika pia ni ya kwetu sisi leo hii kama tukitii KUTOKA MISRI MUNGU ALITUITA..Na kama tuliitwa kweli kutoka Misri hatuna budi kupitia njia ya nyikani na jangwani ili kuifikia nchi ambayo Mungu ataachilia UTUKUFU WAKE kuwaokoa wengine.

SASA NYIKANI NA JANGWANI NI WAPI KWA SASA?.

Unapopompa Bwana maisha yako kwa mara ya kwanza, hauna budi kuwa radhi kusalimisha kila kitu chako kwake ili aweze kukufanya kuwa mwanafunzi wake, ili Mungu baadaye aweze kukutumia wewe kuachilia utukufu wake uwaangazie wengine ni sharti ukubali kutii kupitia madarasa ya Mungu na ndio maana Bwana Yesu aliwaambia maneno haya wale wote ambao walitaka kuwa wanafunzi wake.

Luka 14.25 “Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia,

26 Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

27 MTU YE YOTE ASIYEUCHUKUA MSALABA WAKE NA KUJA NYUMA YANGU, HAWEZI KUWA MWANAFUNZI WANGU.

28 Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia?

29 Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki,

30 wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza.

31 Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini?

32 Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali.

33 BASI, KADHALIKA KILA MMOJA WENU ASIYEACHA VYOTE ALIVYO NAVYO, HAWEZI KUWA MWANAFUNZI WANGU.”

Unaona hapo?. Zipo gharama za kuwa mwanafunzi, kumbuka sio watu wote wanaweza wakawa wanafunzi wa Kristo,. Kama Usipokuwa tayari kupoteza kila kitu ulichonacho kwa ajili ya Kristo, kama vile mwanafunzi shuleni, anasahau kabisa dunia ikoje anakaa bweni miaka kadhaa akisoma tu,asijishughulishe na kitu kingine na kusahau tamaa za nje alizokuwa anaziona, na ndivyo ilivyo kwa wale wanaopenda kuwa wanafunzi wa Kristo, usipokubali kupita katika njia ya jangwa na kuishi maisha ya kumwangalia yeye tu, hutaweza kuwa mwanafunzi wake, usipokuwa tayari kuichukia hata nafsi yako kwa ajili ya Kristo, usipokuwa tayari kuacha anasa zako, usipokuwa tayari kuacha hizo biashara haramu kwa ajili ya Kristo, na usipokuwa tayari kuchukiwa na ndugu, hata wakati mwingine wazazi kwa ajili ya Kristo, huwezi kuwa mwanafunzi wake, usipokuwa tayari kuishi kwa kumtegemea Mungu tu, akufundishe, kama wana wa Israeli jangwani, kama Yohana jangwani, kama Musa jangwani, kama Eliya jangwani, kama Elisha nyikani, huwataweza kumwandalia Mungu njia ya kushukia. Usipokuwa tayari kupoteza vitu uvipendavyo kwa ajili ya madarasa ya Kristo hutaweza kumtengenezea njia ya yeye kushukia.

Isaya 40:3 “Sikiliza, ni sauti ya mtu aliaye, ITENGENEZENI NYIKANI njia ya Bwana; NYOSHENI JANGWANI njia kuu kwa Mungu wetu.

Hivyo yeye atakayeshinda kulivuka hilo jangwa na hiyo nyika ambayo Mungu atampeleka huko makusudi kwa ajili ya kumfundisha hapo ndipo atatiwa mafuta na Mungu mwenyewe ili kuwahudumia watoto wake.

Bwana Yesu anasema mtu wa namna hiyo ni mkuu zaidi ya nabii yoyote yule. Mtu yoyote Yule ambaye atamtengenezea Bwana njia iliyonyooka, huyo ni mkuu kushinda nabii yoyote Yule alishawahi kutokea duniani Bwana YESU anasema hivyo.

Mathayo 11:9…..Naam, nawaambia, na aliye mkuu zaidi ya nabii.

10 Huyo [mtu huyo] ndiye aliyeandikiwa haya, Tazama, mimi namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako mbele yako.

Hivyo kama na sisi tunataka tuwe wajumbe watakaomtangulia mbele yake, inatupasa tumwandalie njia kwanza kabla ya kufika, na njia haiandaliwi mahali popote tu isipokuwa NYIKANI NA JANGWANI.

Tusijidanganye tunasema sisi ni watumishi wa Mungu, sisi tuna nena kwa lugha, sisi tuna upako, sisi tunatoa pepo, sisi tunaponya magonjwa, na huku madarasa ya Mungu tumeyakwepa, na huku ndani ya mioyo yetu tuna viburi, ndani ya mioyo yetu tuna sanamu, ndani ya mioyo yetu hatujaumbiwa saburi na unyenyekevu, ndani ya mioyo yetu ni wanung’unikaji, tusijidanganye ikiwa tumelikwepa hilo jangwa ambalo kwa hilo tungefundishwa sheria na kanuni za Mungu,

Na maombi yangu, tusikwepe madarasa ya Mungu yanapoletwa mbele yetu, pale tunapoteremshwa jangwani tusipindishe njia na kutaka kurukia moja kwa moja Kaanani siku hiyo hiyo, Mungu huwa anatembea katika kanuni zake, ikiwa wewe ni mtoto kweli wa Mungu siku inakuja Mungu atakapeleka nyikani tu, hilo ni darasa lisilokwepeka. vinginevyo mbele za Mungu tutaonekana watoto wachanga tusiomjua yeye. Hawakuwa na bahati mbaya mitume wa Kristo kupoteza vyote walivyonavyo kwa ajili ya Kristo, kadhalika haitakuwa bahati mbaya kwetu nasi tukipoteza vyote tulivyonavyo kwa ajili ya Kristo, kwasababu hiyo ndiyo njia pekee ya kuwa WAKUU MBELE ZA MUNGU na kuwa wanafunzi wake.

Ubarikiwe sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

MBINGUNI YUPO NANI SASA?

MELKIZEDEKI NI NANI?.

MWEZI NI ISHARA GANI KWETU?.

SEHEMU YA MAANDIKO ILIYOFICHWA.

MAVAZI YAPASAYO


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/01/01/njia-ya-bwana-inatengenezwa-wapi/