by Admin | 2 January 2019 08:46 am01
Biblia inatuambia kuwa malaika ni roho watumikao, kuwahudumia wale watakaourithi wokovu. (Waebrania 1:14). Biblia inatuambia pia shetani naye ni mshitaki wetu, yeye na jeshi lake la mapepo wakitushita sisi mbele za Mungu wetu mchana na usiku tunaona kama walivyofanya kwa Ayubu (Ufunuo 12:7), vivyo hivyo malaika watakatifu wa Mungu ambao hao Mungu aliwaweka kwa lengo la kutuhudumia sisi (yaani wakristo), wanasimama mbele za Mungu wetu usiku na mchana wakipeleka habari zetu njema mbele zake.
Na ndio maana Bwana Yesu alisema “Angalieni msidharau mmojawapo wadogo hawa; kwa maana nawaambia ya kwamba MALAIKA WAO MBINGUNI SIKU ZOTE HUUTAZAMA USO WA BABA YANGU ALIYE MBINGUNI.” (Mathayo 18.10).
Hii ni huduma kuu ya malaika walio nayo sasa.
Lakini japo malaika hawa wamepewa uwezo mkubwa zaidi yetu sisi, japo ni watakatifu sana kuliko sisi, japo ni wakamilifu kuliko sisi lakini tunasoma wanaposimama mbele za Mungu ili kupeleka habari zetu mbaya wanatetemeka na kuogopa, Embu fikiria leo hii unajiita mkisto, na siku ile ulipofanyika kuwa mwana Mungu, ulifahamu kuwa Kristo alilituma jeshi lake la malaika kukulinda pamoja na kuhusukia kuchukua dua zako na matendo yako mema mbele za MUNGU. Lakini jaribu kifikira wewe unayejiita mkristo halafu leo hii unakwenda kuzini, na huku unajua kabisa wapo malaika watakatifu walitumwa kutembea na wewe, halafu wanakuona unafanya kitendo hicho cha aibu na cha kichafu ambacho mtu anayejiita Mkristo hastahili kukifanya. Wewe unadhani malaika watakatifu watapeleka repoti gani nzuri ya kwako mbele za Mungu.?
Kwasababu kumbuka unapoomba maombi yako yanachukuliwa na malaika na kufikishwa mbele ya kiti cha enzi, unapofanya wema, wema wako unachukuliwa na malaika moja kwa moja na kuwasilishwa mbele ya kiti cha enzi, anapofanya tendo lolote jema linachukuliwa na kupelekwa katika kumbukumbu za kimbinguni zikingojea kusomwa mbele ya kiti cha enzi mbinguni, kadhalika yule malaika husika naye huwa anajisikia fahari kupeleka habari njema kama hizo mbele za Mungu. Hata akifika pale atakusifia kwa maneno mazuri na kumkumbusha Mungu na mambo mengine ya kwako mazuri unayoyafanya hata kama hujawahi kumwomba Mungu. Malaika wanakuwaanapanda j na kushuka juu yako kupeleka mema yako na kukuhudumia sawasawa na maono aliyoyaona Yakobo (aliona malaika wakipanda juu na kushuka) Mwanzo 28:12 “Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake”.
Lakini unapokuwa ni mwovu halafu unasema umeokoka, umebatizwa, umepokea Roho Mtakatifu, hataweza kupeleka habari yoyote njema mbele za Mungu kwa ajili yako?. Kumbuka yeye ni mtakatifu lakini matendo yako yanamfanya ajione mchafu na asiyestahili kupeleka habari zako mbaya mbele zake. Na hii ni mbaya sana kwasababu wakati Mungu atakapopokea ripoti za wana wake wengine duniani, za kwako zitakuwa hazifiki, na hapo atakapomuuliza malaika husika aliyepewa jukumu la kutembea na wewe, vipi habari za huyu mtu kwanini hazinifikii, lakini kwa kuwa malaika wa Bwana ni wenye hekima nyingi, watajaribu kuzungumza tu yale mema ya nyuma uliyokuwa anayafanya na kusitiri ubaya wako. Lakini jicho la Mungu linaloona mbali, litatazama lenyewe. Na yeye na kuuangalia mwenendo wako yeye mwenyewe. Hapo ndugu usitamani ufikie hatua hiyo kwasababu hakuna msamaha tena ghadhabu ya Mungu ni kali, hatua hiyo ukishafikia ni nani atakayekutetea?.
2Petro 2:10 “Na hasa wale waufuatao mwili katika tamaa ya mambo machafu. na kudharau mamlaka.
11 Wenye ushupavu, wenye kujikinai, hawatetemeki wakiyatukana matukufu; IJAPOKUWA MALAIKA AMBAO NI WAKUU ZAIDI KWA UWEZO NA NGUVU, HAWALETI MASHITAKA MABAYA JUU YAO MBELE ZA BWANA.
12 Lakini hao kama wanyama wasio na akili, ambao walizaliwa kama wanyama tu wa kukamatwa na kupotezwa, wakikufuru katika mambo wasiyoyajua, wataangamizwa katika maangamizo yao;
13 Wakipatikana na madhara, ambayo ni ujira wa udhalimu wao, wakidhania kuwa ulevi wakati wa mchana ni anasa; wamekuwa ni mawaa na aibu wakifuata anasa zisizo kiasi katika karamu zao za upendo, wafanyapo karamu pamoja nanyi;
14 wenye macho yajaayo uzinzi, watu wasiokoma kutenda dhambi, wenye kuhadaa roho zisizo imara, wenye mioyo iliyozoezwa kutamani, wana wa laana;
15 wakiiacha njia iliyonyoka, wakapotea, wakiifuata njia ya Balaamu, mwana wa Beori, aliyependa ujira wa udhalimu;”.
Unaona hapo biblia inasema “; IJAPOKUWA MALAIKA AMBAO NI WAKUU ZAIDI KWA UWEZO NA NGUVU, HAWALETI MASHITAKA MABAYA JUU YAO MBELE ZA BWANA”.
.. Unasema wewe ni mkristo lakini unapojisikia tu kutenda dhambi unakwenda kufanya bila kuogopa kuwa Mungu juu anakutazama. Unakuwa mlevi wa chini chini, hutaki ujulikane kwa wakristo wenzako, hujui kuwa malaika wa Bwana wanaona mambo unayoyafanya, wanakosa jambo jema la kwenda kuzungumza juu yake mbele ya kile kiti kitakatifu cha Enzi mbinguni. Unakula rushwa, unakuwa mwizi, unaabudu sanamu, unatazama pornography na unafanya mustarbation kisirisiri ni kweli mwanadamu hakuona lakini wapo wengine wanaokuona, na hao si wengine zaidi ya malaika wa Bwana na mashetani.
Ikiwa sifa zako njema hazipelekwi na malaika basi uwe na uhakika kuwa mambo yako maovu yanachukuliwa na mapepo na kuimbwa mbele ya kiti cha enzi cha Mungu usiku na mchana.
Sasa baada ya Mungu mwenyewe kushuka na kuangalia matendo yako, kwa dua za hayo mashetani ambazo ziliwasilishwa mbele zake, akiona jinsi uliyoonywa mara nyingi ugeuke hutaki ndipo hapo Bwana anatoa tamko. HUYU SI WANGU TENA!. Unakabidhiwa shetani, kuanzia huo wakati unakuwa milki halali ya shetani, hali yako inakuwa mbaya kuliko ulivyokuwa mwanzoni wale malaika waliotumwa kukulinda wanaondoka, habari zako zinasitishwa kutajwa mbinguni wema wako wote unasahauliwa.
Tafsiri ya jina shetani au Ibilisi ni MCHONGEZI au MSHITAKI. Kazi ya shetani kubwa ni kutushitaki mbele za Mungu usiku na mchana…Malaika wao wanapeleka habari zetu njema mbele za Mungu lakini shetani na majeshi yake wao wanapeleka habari mbaya mbele za Mungu. Hiyo ndiyo vita kubwa inayoendelea katika ulimwengu wa Roho, kati ya malaika na mapepo.
Hawapigani kwa kukatana na mapanga, hapana bali wanashindana kwa hoja.
Tuchukue mfano mwepesi..mkristo mmoja anayeitwa Rodgers anayesema ameokoka leo kafunga na kusali lisaa limoja, katoa zaka kanisani, na kamsaidia ndugu mmoja aliyekuwa na uhitaji mtaani kwake, sasa kinachotokea katika ulimwengu wa Roho yule malaika wake anayetembea naye anapeleka habari za wema wake huo mbele za Mungu, na kumwambia Mungu kuwa Mtumishi wako Rodgers kafanya hichi na kile leo, hivyo anastahili thawabu Fulani kulingana na Neno lako hili na lile, Lakini bahati mbaya wakati malaika hao wanamsifia Rodgers mbele za Baba, Rodgers pasipo kulijua hilo kesho yake anakwenda kuzini..kinachotokea sasa ni shetani na malaika zake wanakwenda kumchongea Rodgers mbele za Mungu, kwamba yule mtu mnayesema ameokoka na anastahili kupata hichi na kile leo hii tumemwona anazini hivyo kulingana na Neno hastahili kuitwa mtoto wa Mungu kwasababu maandiko yanasema aziniye na mwanamke hana akili kabisa(Mithali 6:32) na zaidi ya yote maandiko “Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu 1Yohana 3:9 ” …na kumbuka haya mapepo yanatoa kabisa mistari mbele za Mungu kumshtaki Rodgers na kwasababu yametoa hoja za nguvu mbele za Mungu, wanakuwa wamewashinda wale malaika wanaomsifia Rodgers na hivyo Rodgers anakabidhiwa shetani. Hivyo ndivyo shetani anavyowashitaki watu.
Unakumbuka maandiko yanasema wana wa Mungu (Malaika) siku moja walipokwenda kujihudhurisha mbele za Mungu shetani naye alikwenda katikati yao kumshitaki Ayubu? (Hiyo inapatikana katika kitabu cha Ayubu 1:6-12).
Kwahiyo Mtu anayeishi maisha ya uvuguvugu na bado anasema ni Mkristo, anafanyika kuwa chombo cha shetani kikamilifu, kama ulikuwa mzinzi kidogo hapo ndipo unajikuta nguvu mbaya ya uasherati unakuvaa unakuwa unakuwa zaidi ya hapo, pombe ulikuwa unakunywa kidogo, unafikia hatua ya kumaliza hata kreti, tabia yako inabadilika ghafla na kibaya zaidi hata kumrudia Mungu hutaweza tena kwasababu Bwana Yesu alishasema hakuna mtu anayeweza kuja kwangu, isipokuwa kwanza kavutwa na Baba yangu aliye mbinguni. Sasa kama ni Mungu mwenyewe kakukataa unadhani ile nguvu ya kutubu wakati huo utaitolea wapi?. Haiwezekani.Na mwisho wake ni Mauti, kwasababu biblia inasema mshahara wa dhambi ni MAUTI, Na ndio maana malaika watakatifu wanaogopa kupeleka mashitaka yako mabaya juu mbele za Mungu, kwasababu wanafahamu madhara yatakayomkuta mtu huyo mara baada ya kukataliwa.
Ni jambo la kuogopesha sana. Leo hii Bwana anapotuambia tuwe moto, anaamisha kweli kweli, maana tukiwa vuguvugu ndio huko kutapikwa kunafuata. Inasikitisha kuona kwamba mtu anasema ameokolewa na Bwana lakini mambo ya kidunia hajayaacha,.bado anavaa kidunia, anavaa vimini, anavaa suruali, anakwenda Disko, anasikiliza nyimbo za kidunia, anaipenda dunia kuliko kumpenda Mungu, anatazama pornography, anakwenda kwa waganga,ni mtukanaji. Biblia inasema ni heri mtu huyo asingookoka kabisa, kwasababu hata wale malaika watakatifu wasingeletwa kumtazama, Lakini kuwa vile halafu unaishia kuwatia visirani, na kuwafedhehesha unadhani mwisho wake utakuwa ni nini?.
Wana wa Israeli walipokuwa wanatoka Misri Bwana aliwaagizia malaika wake aende mbele yao, na akawaonya wasimtie kisirani kwa mienendo yao mibovu kwa kuwa hatawasamehe,(kutoka 23:20) Unaona tunasema tumekuwa wakristo tujue kuwa hatupo wenyewe. Bali Roho wa Kristo yupo pamoja nasi kadhalika na jeshi la kifalme la malaika wa mbinguni lipo pembeni yetu kutuhudumia. Hivyo tunapaswa tuwe makini sana na mienendo yetu.
Ni maombi yangu, leo hii utaulinda wokovu wako, kila wakati. Ikiwa malaika tu wenyewe wanaogopa kupeleka habari zetu mbaya, japo wao ni watakatifu, unadhani sisi tunapaswa tuishije. Malaika japo wokovu hauwahusu wao lakini wanasita kuizungumza mienendo yetu mibaya mbele za Mungu, si zaidi sisi ambao tupo duniani ambao wokovu unatuhusu? Tunapaswa tujilinde sana mienendo yetu ya kikisto.
Ikiwa bado hujampokea Kristo katika maisha yako huu ndio muda, unachopaswa kufanya ni kutubu mwenyewe kwa kumaanisha kuacha dhambi zako na maisha yako ya kale, kisha ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo upate ondoleo la dhambi zako, (Matendo 2:37-38)na baada ya hapo utafanyika mwana wa Mungu kwa Roho wa Kristo atakayekuja ndani yako.. Nawe pia jeshi hili la kimbinguni la malaika watakatifu litatumwa kwako kukulinda, kukutetea na kupelekea habari zako njema mbele za kiti cha Enzi usiku na mchana.
Bwana akubariki sana.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
JIFANYIE RAFIKI KWA MALI YA UDHALIMU.
HISIA YA MUNGU ILIYO MBAYA KULIKO ZOTE.
HERI, WALE MUNGU ASIOWAHESABIA MAKOSA YAO.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/01/02/hudumu-ya-malaika-watakatifu/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.