MAMBO AMBAYO MALAIKA WANATAMANI KUYACHUNGULIA.

by Admin | 31 January 2019 08:46 pm01

Siku hiyo itakuwa ni siku ya namna gani?, Siku hiyo ya watakatifu wote kunyakuliwa, siku hiyo ambayo itakuwa ni mwisho wa taabu zote kwa wana wa Mungu..Siku ambayo tutakutana na YESU uso kwa uso, siku ambayo Bwana atakapokwenda kuweka wazi mambo yake yote aliyokuwa ametuandalia tangu zamani , makao yetu ya milele, Biblia inasema ni mambo ambayo hata malaika watakatifu wanatamani kuyachulingulia wayaone yakoje..

Ni kama tu vile na sisi tulivyo na shauku ya kuona walau kwa uchache jinsi mbingu ilivyo, kwani tumekuwa tukiisikia uzuri wake usio wa kawaida tangu zamani jinsi ulivyo lakini tusiuone, Na kwa namna hiyo hiyo malaika nao sasa huko juu mbinguni, wanatamani kwa shauku kubwa walau waonjeshwe mambo walioandaliwa wateule wa Mungu na YESU KRISTO mwenyewe siku ile itakavyokuwa. Huko walipo Malaika watakatifu wanasikia tu! kuwa kuna utukufu mkubwa Bwana amewaandalia watakatifu wake, wanafahamu kuwa ni utukufu ulio mkuu sana usioneneka. lakini bado hawajauona ni wa namna gani, wanajua kuwa siku ya ukombozi wa watoto wa Mungu ni siku KUU sana, mambo yasiyoneneka wala kutamkika yatafunuliwa katika siku hizo, hivyo hiyo inawafanya wao nao waitamani siku hiyo ije kwa haraka wao nao wayashuhudie mambo hayo ya ajabu.

1Wakorintho 2:9 “Lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao”.

Na Sio malaika tu peke yao, hata viumbe vingine vyote vinaitamani hiyo siku ifike, Mtume Paulo anasema ..

Warumi 8:18 “Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama UTUKUFU ULE UTAKAOFUNULIWA KWETU.

19 Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia KWA SHAUKU NYINGI kufunuliwa kwa wana wa Mungu.

20 Kwa maana viumbe vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake yeye atiyevitiisha katika tumaini;

21 kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu”.

Kwasasa hatuwezi kusema mengi kwasababu bado hatujafunuliwa mambo yenyewe lakini tunafahamu sifa moja ya Mungu KUWA YEYE HUWA HASEMI UONGO, na kama alivyosema “ kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu”..Alimaanisha kuwa tunaweza kuchukulia hivyo vitu kwa upeo wetu wa kibinadamu kiwepesi wepesi lakini siku tutakapokuja kuyaona hayo mambo ndipo tutakapojua kweli mawazo yake yalikuwa mbali sana na sisi tulivyokuwa kufikiri.

Siku hiyo sisi tutakapoondoka hapa duniani, haitakuwa heri kwetu tu sisi na viumbe vyote, bali itakuwa heri pia kwa Malaika wote walioko mbinguni. Kutakuwa na shangwe na furaha isiyoneneka.

Hivyo ndugu tukikaa na kuyatafakari hayo kwa utulivu, basi hatutajali ni mambo mangapi yatapita mbele yetu mabaya, sisi siku zote tutaelekeza macho yetu mbinguni, hatutajali ulimwengu unasemaje, sisi tutamtazama mwokozi wetu YESU KRISTO daima, huku tukingojea kwa saburi yale Mungu aliyoutandalia, tutaishi kama wapitaji na wasafiri tu hapa duniani.

1Petro 1:9-16

“9 KATIKA KUUPOKEA MWISHO WA IMANI YENU, YAANI, WOKOVU WA ROHO ZENU.

10 Katika habari ya wokovu huo manabii walitafuta-tafuta na kuchunguza-chunguza, ambao walitabiri habari za neema itakayowafikia ninyi.

11 Wakatafuta ni wakati upi, na wakati wa namna gani ulioonywa na Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, ambaye alitangulia kuyashuhudia mateso yatakayompata Kristo, NA UTUKUFU UTAKAOKUWAKO BAADA YA HAYO.

12 Wakafunuliwa ya kuwa si kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yenu walihudumu katika mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiri ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. MAMBO HAYO MALAIKA WANATAMANI KUYACHUNGULIA.

13 Kwa hiyo vifungeni viuno vya nia zenu, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo.

14 Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu;

15 bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;

16 kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”

Tukaze mwendo, ikiwa maisha yako sasa yapo mbali na Kristo, huu ni wakati wa kumrudia yeye maadamu mlango wa neema bado upo wazi, kumbuka siku ile ukijikuta umeachwa majuto hayatakuwa kwasababu unakwenda Jehanum, hapana majuto makubwa yatakujia kwasababu umekosa mambo mazuri ya umilele Mungu aliokuwa amewaandalia watoto wake tangu zamani.

Hivyo tubu kabisa kwa kudhamiria kuanza maisha mapya katika Bwana, na haraka bila kukawia nenda ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa kwenye maji tele, na kwa Jina la YESU KRISTO..Ili upate ondoleo la dhambi zao kulingana na Matendo 2:38., kisha Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu kama alivyoahidi, na kuanzia hapo nawe utakuwa umeingizwa na kuwa mmojawapo wa waliostahili kuuona huo utukufu ambao utakuja kufunuliwa siku za hivi karibuni. Tunaishi katika siku za mwisho Zidi kudumu katika utakatifu, na ushirika na kusali daima.

Bwana akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/01/31/mambo-ambayo-malaika-wanatamani-kuyachungulia/