by Admin | 31 January 2019 08:46 pm01
Kila mmoja wetu anapiga hatua, na hizi hatua tunapiga kuelekea mahali Fulani, ilikuwa juzi ikawa jana, na sasa imekuwa leo, na hiyo ipo bayana kabisa kuwa yapo mambo mazito mbele yetu yanayotusubiri , upo unyakuo mbele yetu, na kama unyakuo hatutaukuta basi kifo hatutakikwepa..Leo unaweza ukasema kesho kutwa nitafanya hivi au nitafanya vile, au mwakani nitakuwa nimeshafika mahali Fulani, lakini kumbuka hata aliyekufa jana naye sio kwamba alijua safari yake imefika, hapana na yeye pia aliiona mbele yake kuwa itakuwa hivi au vile n.k…
Mtume Paulo aliwaambia watakatifu waliokuwa Rumi maneno haya “wokovu wetu sasa upo karibu nasi kuliko tulipoanza kuamini”..Unaona? Hii ikiwa na maana kuwa leo hii tupo karibu na unyakuo zaidi kuliko ilivyokuwa jana na juzi, kuliko ilivyokuwa enzi za mtume Paulo..Na kama ni hivyo basi inatupaswa sisi watu wa kizazi hiki tuwe makini kiasi gani?..Ni wazi kuwa inatupaswa tumtafute Mungu zaidi, tujishughulishe na mambo ya mbinguni kuliko wao, tuishi maisha ya kujichunga mara nyingi zaidi ya wao.
Je! Unafahamu kuwa kanisa tunaloishi ndilo kanisa la mwisho lijulikanalo kama Laodikia, na kuwa baada ya hili kuisha hakutakuwa na kanisa lingine lolote? kulingana kitabu cha Ufunuo 2&3. Kanisa hili litamalizikia na unyakuo, na ndilo kanisa la 7, Tofauti lile la mitume walilokuwa wanaishi ambao lilikuwa ni kanisa la Kwanza lijulikanalo kama Efeso,
Unafahamu kuwa unyakuo utakuwa ni kwa siri sana, na si kila mtu atafahamu habari hiyo kama wengi wanavyodhani? Kwamba Kutakuwa na makelele barabarani, na maajali.? Ni kundi dogo sana litakaloondoka, kiasi kwamba ulimwengu hautajua lolote, isipokuwa kikundi kidogo sana.
Unafahamu kuwa Ile Roho ya Mpinga-Kristo tayari imeshaanza kufanya kazi, na hiyo haitendi kazi pengine popote nje ya Kiongozi mkuu wa kidini mwenye wafuasi wengi kuliko wote duniani huko Vatican Roma?
Unafahamu kuwa Injili hii unayohubiriwa moja ya hizi siku itasikika Israeli kwa nguvu na wayahudi wote wataamini, na tukio hilo ukilishuhudia basi ujue kuwa unyakuo ulishakuacha siku nyingi. Kwasababu Mungu alishaahidi kuwa atawarudia watu wake, wayahudi, na siku atakayowarudia unyakuo utakuwa umeshapita.
Kwani ule unabii waliotabiriwa juu yao kwamba watarudi katika nchi yao umeshatimia, jopo kubwa la wayahudi wamesharudi kwao, na wachache waliosalia wanarudi kwa kasi sana, wanachongojea ni kumwagiwa roho ya Neema tu.Wamwamini masihi wao waliomsulibisha. Na kisha wawe tayari kumpokea.
Takwimu zinaonyesha kuwa hakuna taifa ambalo injili ya Kristo Yesu haijahubiriwa mpaka sasa, kila mji na kila kijiji, Yesu Kristo kashatajwa,na kumbuka biblia inasema pindi tu habari njema za ufalme zitakapohubiriwa katika ulimwengu wote hapo ndipo ule mwisho utakapokuja..Unadhani ni kitu gani Mungu anasubiria sasa..
Biblia imesema mambo mengi sana juu ya yatakayotekea siku za mwisho hatuwezi kuyazungumza yote hapa, lakini moja ya dalili ya wazi kabisa ambayo hata wewe unaiona ni juu ya kutokea kwa manabii wengi wa uongo. Wimbi hili lilianza kulipuka mwanzoni mwa miaka ya 2000, lakini limekuja kukolea zaidi kuanzia kipindi cha miaka ya 2010, Hii inayoonyesha wazi ni jinsi ule mwisho unavyokuja kwa haraka sana kushinda sisi tunavyofikiri.
Ishara nyingine ni kuwa Maasi yataongeza..Leo hii tunashuhudia vitendo viovu, na vya kikatili kila mahali, mambo machafu kwenye mitandao, kila aina ya uozo upo wazi siku hizi hadharani, wala sio siri tena hata watoto wadogo hakuna kitu chochote wasichokijua kinachoendelea cha ulimwengu huu.
Biblia inasema wakati huu wa mwisho ukikaribia kufika ndipo wale watu wa kukufuru na kudhihaki watakapoongoza, wakisema iko wapi ile ahadi ya kuja kwake,.. mbona YESU harudi tumwone, miaka 2,000 imepita amekufa nini?, pamoja na hayo mithali kadha wa kadha za kejeli zimetungwa kwa watu wote wote wanaomtazamia Kristo kuja. Hata injili zenyewe zimegeuzwa sasa, hakuhubiriwi tena kuja kwa Kristo kama zamani, bali mafanikio ya kidunia. Injili shetani alizomhubiria Bwana za kumpa Milki zote za dunia endapo akimsujudia.
Na kwa bahati mbaya watu wanaangalia wakidhani kuwa siku hiyo ikikaribia kufika pengine duniani kutakuwa na vita na machafuko ya kila namna.Lakini biblia inatuambia kuwa wakati wasemapo AMANI! AMANI!, ndipo uharibifu unapokuja kwa ghafla..
1Wathesalonike 5:2 “Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.3 Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.”
Na ndio maana mtume Paulo anasema:
Warumi 13:11 “Naam, tukiujua wakati, kwamba saa ya kuamka katika usingizi imekwisha kuwadia; kwa MAANA SASA WOKOVU WETU U KARIBU NASI KULIKO TULIPOANZA KUAMINI
12 Usiku umeendelea sana, mchana umekaribia, basi na tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru.
13 Kama ilivyohusika na mchana na tuenende kwa adabu; si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu.
14 Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake”.
Ndugu kwanini ujiweke katika hali ya hatari kama hii, leo ni siku nyingine, tumeukaribia mwisho kuliko jana, usiseme bado nipo, bado sijawa tayari, utajikuta unaangukia kifo au dhiki kuu gafla. Saa ya wokovu ni sasa,hiyo kesho hata Bwana kasema tusiisumbuke kwasababu hatujui yatakayozaliwa ndani ya siku moja. umekufikia ujumbe huu mahali ulipo, unadhani ni kwa bahati bahati tu. Jua kuwa Mungu anataka kusema na wewe ili ayabadilishe maisha yako.
Bwana anasema, laiti mwenye nyumba angelijua saa ambayo mwizi atakuja usiku basi angelikesha. Hata ingekuwa ni wewe ungefanya hivyo.Lakini kwasababu hutaki kuibiwa usiku na ndio maana kubla hujalala unahakikisha umeufunga vizuri mlango wako kwa makomeo, Sio kwasababu unapenda kujifungia hapana. Ni kwasababu unachukua tahadhari kwasababu hujui ni lini mwizi atakuja.
Halikadhalika mimi na wewe hatujui siku ya kuja kwa BWANA, kwahiyo ni wajibu wetu kukesha, kuamka usingizini, kuvua mambo yetu ya kale, kuanza maisha mapya na Mungu wetu katika kizazi hichi cha hatari tunachoishi. Lakini tunajua tu muda umekwenda sana.
Ikiwa utataka kutubu kwa kumaanisha kabisa kuacha dhambi zako, basi Kristo atakupokea na kukuosha dhambi zako.Na ukishabatizwa katika ubatizo sahihi wa kimaandiko (yaani ubatizo wa kuzamishwa na kwa jina la YESU KRISTO), kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako(Matendo 2:38). Basi yeye mwenyewe atakutia muhuri kwa Roho wake Mtakatifu kuwa ni wake,(Waefeso 4:30) na kisha baada ya hapo utaishi katika tumaini ukijua kabisa hata leo hii mambo yakibadilika utakuwa katika upande salama Ikiwa utaendelea kudumu katika njia zake..
Pia na wewe ambaye tayari ni Mkristo kumbuka kuwa “WOKOVU WETU U KARIBU NASI KULIKO TULIPOANZA KUAMINI”. Hivyo huu si wakati wa kulegea au kupoa,au kutazama mambo ya ulimwengu huu, bali huu ni wakati wa kuzidi kujitakasa kila iitwapo leo, maadamu tunaona siku inakaribia na kwamba muda wowote tunaweza kuitwa juu nyumbani kwa Baba. Biblia inasema “tuutimize wokovu wetu kwa kuogopa na kutetemeka Wafilipi 2:12”
Ubarikiwe sana.Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
AGENDA KUBWA YA SHETANI KWA KANISA HILI LA LAODIKIA.
VIUNO VYENU VIWE VIMEFUNGWA NA TAA ZENU ZIWE ZINAWAKA
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/01/31/wokovu-wetu-u-karibu-nasi-kuliko-tulipoanza-kuamini/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.