by Admin | 30 April 2019 08:46 pm04
Isaya 55:1-2 “ Haya, kila aonaye kiu, njoni majini, Naye asiye na fedha; njoni, nunueni mle; Naam, njoni, nunueni divai na maziwa, Bila fedha na bila thamani.
2 Kwani kutoa fedha kwa ajili ya kitu ambacho si chakula? Na mapato yenu kwa kitu kisichoshibisha? Nisikilizeni kwa bidii, mle kilicho chema, Na kujifurahisha nafsi zenu kwa unono.”
Jina kuu la mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe, Nakukaribisha katika kuyachunguze maandiko nilipokuwa ninautafakari huu mstari, picha iliyojitengeneza moja kwa moja katika kichwani kwangu ni sawa mtu mwenye Hoteli maarufu ya 5 STAR Dubai, ambayo kifungua kinywa chake tu asubuhi gharama zake ni sh laki 3, mbali na gharama za chakula cha mchana na jioni, na zile za kulala..halafu leo hii unamwona anajitokeza hadharani anawakaribisha watu wote waje kula na kunywa katika hoteli ile bure, pasipo gharama yoyote…
Na cha kushangaza zaidi anatoa kauli hii “njoo UNUNUE bure”, hakwambii njoo nikupe bure, hapana bali anasema njoo “UNUNUE” bure, hii ikiwa na maana,utakapofika pale utaandikiwa risiti ya ununuzi kama tu vile mtu aliyelipia gharama zote, na hiyo inakupa uhalali wa kuhudumiwa kwa viwango vile vile bila upendeleo sawa tu na mtu Yule ambaye ametoa pesa yote mfukoni.
Lakini utashangaa sana siku ile usipoona watu wengi katika hoteli hiyo maarufu, maswali mengi yanaweza yakaja kichwani mwako sindio?, pengine utasema hawa wameona kama wamedharauliwa au?, au wameshushwa hadhi?, au wanaogopa kwenda kutokana na hadhi ya hoteli ile au? Au wameona kama wanaingizwa mjini au ni nini?..Ni wazi kabisa utajiuliza kwa offer kubwa kama hiyo ni kwanini pakose watu?.
Ndugu ndivyo Mungu anavyotufanyia sisi wanadamu, anatuita tuje tule, tunywe tujishibishe nafsi zetu kwa vinono kwake, bila gharama yoyote, lakini sisi tunapoona tunapewa vyote hivi kwa bei ya bure, tunaona kama havina thamani kubwa kwetu, na hiyo inatupelekea kuudharau wokovu na kwenda kutafuta vitu ambavyo vitatugharimu maisha yetu na mwisho wa siku visituletee faida yoyote katika roho zetu.
Nataka nikuambie, siku zote kitu kikiwa na thamani kubwa sana isiyoweza kufikiwa na wengi mara nyingi huwa kinageuka na kuwa bure, hiyo ni fact kwasababu kitakosa mnunuzi, hivyo thamani yake inarudi tena katika sifuri, na ndio maana ukitazama hata taifa linalodaiwa matrilioni ya pesa na mataifa tajiri, utaona mfano likishindwa kulipa, wale watu wanaandikiwa msamaha, sio kana kwamba hawaithamini au hawaihitaji ile pesa hapana, bali, wanaona huyu mtu hata atoe vitu vyake vyote hawezi kulipa deni hili hivyo ya nini kumdai!..Ni sawa na kupoteza muda tu! Lakini angalia wale wa madeni ya kati na madogo madogo, hao ndio wanaokuwa wa kwanza kusumbua, na usipowalipa kwa wakati watakupeleka mpaka kwenye mahakama za kimataifa, na utapigwa faini juu.
Na ndivyo ilivyo kwa Mungu wetu, siku zote vitu vyake vyote anavitoa bure kwasababu vina thamani kubwa sana, pumzi unayoivuta ingekuwa tunalipia tu hata kwa senti moja kila dakika ungekuwa unadaiwa sh. Ngapi mpaka sasa?,..babu wa babu yako angekurithisha madeni yake, maji ya mvua yanayolinyesha shamba lako pamoja na kuijaza na mito yote ya maji na chemchemi ungekuwa unalipia leo hii ungeotoa sh. Ngapi?,
Nishati inayotoka kwenye jua, ambayo kwa dakika 1 inayo uwezo wa kulihudumia taifa la Marekani tu kwa miaka milioni moja,uchunguzi unasema hivyo,sasa mfano tungekuwa tunapewa kwa gharama kama vile tunalipia luku tungelipa sh.ngapi?
Lakini hayo yote bado si kitu zaidi ya WOKOVU, ambao huo kama tukisema ni kuulipia basi tujue pesa zake ni sawa na hakuna mwisho…Mungu alimtuma mwanawe wa pekee ili kuuandaa wokovu huu na kuunda kwa muda wa miaka 33 na nusu, kila siku usiku na mchana alikuwa anauunda, katika vipindi vigumu na vya majaribu mazito tangu siku ya kwanza, alikuwa anatutengeneza sisi chakula hichi kizuri cha roho kwa kupitia mwanawe mpendwa YESU KRISTO, mpaka alipofikia karibu na kumaliza shughuli hii, Mungu mwenyewe akaingia gharama ya kumngongelea “hati ya dhambi zetu, pale msalabani”. Ili DENI lile kubwa sana lifutwe..ilichukua maisha ya mtu mtakatifu sana asiyetenda dhambi kulifuta Deni hili. Ili tu sasa kila mmoja awe na uwezo wa kuununua wokovu huo kwa bei ya bure.
Na ndio maana Bwana Yesu pale msalabani alimalizia na kauli hii..
IMEKWISHA!!.
Ile hati ya deni la dhambi imekwisha. Na leo anasema tena Haya,
“kila aonaye kiu, njoni majini, Naye asiye na fedha; njoni, nunueni mle; Naam, njoni, nunueni divai na maziwa, Bila fedha na bila thamani.
2 Kwani kutoa fedha kwa ajili ya kitu ambacho si chakula? Na mapato yenu kwa kitu kisichoshibisha? Nisikilizeni kwa bidii, MLE KILICHO CHEMA, NA KUJIFURAHISHA NAFSI ZENU KWA UNONO.”
Ununue wokovu huu kwa bei ya bure ndugu, wakati ndio huu, sauti inayokulilia kila siku utubu, haitadumu milele hiyo, mzigo wa dhambi ulionao, siku ile hutaweza kuulipia, unajua kabisa ukifa leo ni moja kwa moja jehanum kwa dhambi zako, siku hiyo utaulizwa kule ni nini shida? Hutakuwa na cha kujitetea, wote watakushangaa wokovu ulipatikana kwa bei ya bure, imekuwaje wewe haukuwa nao??. Isitoshe hizi ni siku za mwisho dalili zote zinaonyesha hatujui kama tunaweza kuwa na vizazi vingine mbele yetu,..Huu ni wakati wa kutafuta mambo ya wokovu wa roho yako sana kuliko mambo mengine yasiyotuahidia uzima wa milele.. Weka Msalaba mbele, dunia nyuma. Imani mbele mali nyuma, Itakufaidia nini upate fedha zote na nafsi yako iangamie?.
Ufunuo 22:17 “Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure”.
Tafadhali “Share” Ujumbe huu kwa wengine. Na Bwana atakubariki.
Ikiwa utapenda kumpa Yesu Maisha yako, au kupata ubatizo sahihi, basi tupigie kwa namba zetu hizi +255789001312/ +255693036618. Na pia kama utapenda masomo haya yawe yanakufikia kila siku kwa njia ya Whatsapp. Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Zinazoendana:
NAYE ALIKUWA HANA BUDI KUPITA KATIKATI YA SAMARIA.
LAKINI SISI HATUKUIPOKEA ROHO YA DUNIA.
“WOKOVU WETU U KARIBU NASI KULIKO TULIPOANZA KUAMINI”
TUSIPOUTHAMINI WOKOVU TUTAPATAJE KUPONA?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/04/30/njoni-nunueni-mle-na-mnywe/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.