TULICHUNGUZE UMBO LA YESU NA MWENENDO WAKE.

by Admin | 13 May 2019 08:46 am05

Kuna maswali mengi tunajiuliza juu ya mwonekano wa nje wa Bwana wetu Yesu Kristo ulikuwaje! Je alikuwa ni mweupe au mweusi, je alikuwa ni mrefu au mfupi, je alikuwa ni mnene au mwembamba?, je! Alikuwa mzuri au wa kawaida?..Biblia inasema nini juu ya jambo hilo?.

Sehemu pekee tunayoweza kuisoma kwenye maandiko na kutupa walau picha ndogo ya mwonekano wake ni Isaya 53:2 Inasema: “Maana alikua mbele zake kama mche mwororo, Na kama mzizi katika nchi kavu; YEYE HANA UMBO WALA UZURI; NA TUMWONAPO HANA UZURI HATA TUMTAMANI”.

Mstari huo unaonyesha kuwa Bwana wetu, alikuwa ni mtu mwenye mwonekano wa kawaida sana..mtu kusema hana umbo inamaanisha kuwa ukimweka katikati ya wanaume wanaovutia unaweza ukashangaa sana, kwenye uzuri tukisema tunamweka katikati ya wenye sura nzuri (ma-handsome) yeye anaweza akawa miongoni mwa wale wa mwisho mwisho pengine,..Ni mtu ambaye mtu akipishana naye barabarani hawezi kuyateka macho yako, kama mtu wa ajabu au ageuke nyuma amtazame, alikuwa ni wa kawaida sana kimwonekano, na ndicho kilichowakuta hata watu aliokuwa nao wakati ule, japo alijulikana sana, umaarufu wake ulienea duniani kote, lakini ilikuwa bado tu ni shida watu kumkariri sura yake, kwasababu si sura ambayo huwezi ukaitilia maanani ukimwona, alikuwa ni mtu wa kawaida. Bwana Yesu hakuwa kama hao watu wanaoonekana kwenye sinema, na kwenye picha wazuri, wanavutia. Sio kwamba alikuwa ni mtu mbaya kwa sura, kwasababu hakuna mtu mbaya duniani, watu wote ni wazuri, lakini tunaweza kusema alikuwa ni mtu wa kawaida.

Unajua kama ulishawahi kugundua jambo mfano umeenda mahali tuseme kwenye ofisi Fulani, ukakutana na wanafanyakazi wa pale, ukikaa tu dakika chake kuyasoma yale mazingira utaweza kumgundua boss wao ni nani, hata kabla ya kuambiwa chochote…utamgundua pengine kwa kiti chake anachokalia, utamgundua kwa wafanyakazi jinsi wanavyomnyenyekea, au anavyowaamrisha, utamgundua hata wakati mwingine kwa mavazi yake, na utembeaji wake…Lakini kwa Bwana YESU haikuwa hivyo, alipokaa na mitume wake kwa miaka zaidi ya mitatu na nusu bado makuhani, na watu wengi walishindwa kumtambua alipoketi katikati ya makutano au wanafunzi wake. mpaka walipotaka kumkamata iliwabidi wakaombe msaada kutoka kwa mmoja wa wanafunzi wake awasaidie.

Hilo tunalithibitisha siku ile Bwana aliyokuja kusalitiwa na Yuda..

Yohana 18:3 “Basi Yuda, akiisha kupokea kikosi cha askari na watumishi waliotoka kwa wakuu wa makuhani na Mafarisayo, akaenda huko na taa na mienge na silaha.

4 Basi Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawaambia, NI NANI MNAYEMTAFUTA?

5 Wao wakamjibu, Ni Yesu Mnazareti. Yesu akawaambia, NI MIMI. Yuda naye aliyemsaliti alikuwa amesimama pamoja nao.

6 Basi alipowaambia, Ni mimi, walirudi nyuma, wakaanguka chini.

7 Basi akawauliza tena, Mnamtafuta nani? Wakasema, Yesu Mnazareti.

8 Yesu akajibu, Nimekwisha kuwaambieni ya kwamba ni mimi; basi ikiwa mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao”.

Unaona?, Unaweza kudhani wale watu walikuwa wanajifanya kutokumjua, utauliza walishindwaje wakati kila siku walikuwa wanamwona Hekaluni akifundisha, lakini ni kweli ilikuwa ni ngumu kumtambua Bwana, hata wewe ungekuwepo bado ungehitaji msaada wa kusaidiwa kumtambua. Hiyo yote ni kwasababu ya mwenendo wake wa unyenyekevu, hakuwa na nguo za kipekee sana kumtofautisha na mitume wake, hakuwa mzuri wa uso zaidi ya mitume wake, hakujipiga scrabing kujionyesha kuwa yeye anatunzwa zaidi ya mitume wake, wala hakuwahi kujionyesha kuwa yeye ni mkuu zaidi ya wengine, kama ingekuwa ni hivyo wale watu wasingetumia nguvu kumtambua, lakini hawakuweza mpaka YESU alipowathibitishia mara mbili ya kuwa yeye ndiye.

Unyenyekevu wa Bwana wetu Yesu Kristo ulikuwa ni mkuu sana, na sisi tunapaswa tuuige mfano huo, unakumbuka pale alipokuwa anawatawadha wanafunzi wake miguu aliwaambia maneno haya: “Ninyi mwaniita, Mwalimu, na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo” (Yohana 13:13), lakini mimi mbele yenu ni kama atumikaye..nami nimewapa kielelezo kama mimi nilivyowatendea ninyi nanyi mkatende vivyo hivyo.” Akamalizia na kusema..

“MKIYAJUA HAYO HERI NINYI MKIYATENDA.”

Tusipende kuitwa wakuu, tusipende kujionyesha sisi ni tofauti na watu wengine hata kama Mungu katupa vipawa vikubwa kiasi gani, Heshima ya utumishi wako haipo katika uzuri wa sura yako ndugu mchungaji, ndugu nabii, ndugu mwalimu… heshima ya utumishi wako haipo katika mavazi unayoyabadilisha kila siku na magari na ma bodyguards, unaotembea nao na msafara au nyumba yake kama raisi. na kuwaonyesha ili watu wote wakuone..Usijidanganye ukidhani hapo ndipo umeupa heshima utumishi wako Mbele za Mungu, kama hutataka kujinyenyekeza kuna hatari mbele.

Imefikia hatua mpaka akionekana mtumishi yeyote wa Mungu anatembea kwa miguu au havai nguo zinazovutia kama watu wengine, anaonekana mlokole aliyekosa maarifa, hamjui Mungu, watu hawamsikilizi tena, Nataka nikuambie ungekuwa kipindi cha mwokozi wako wakati upo hapa duniani ungemfanyia hivyo hivyo tu. Sio kwamba na support uvaaji mbaya hapana, lakini vipo vipimo tofauti tofauti kulingana na mtu, huyu hivi Yule vile, usiutafute uzuri wa nje wa Bwana, hautaupata…kwasababu uso wake haukuwa wa umuhimu sana kwetu zaidi ya Maneno yake, ndio maana karuhusu maneno yake yahifadhiwe mpaka leo na hajaruhusu picha ya uso wake ihifadhiwe mpaka leo.

Kwahiyo ni vizuri kubadilika na kuwa kama YESU KRISTO, Tuipende kweli, tuuishi kweli na kuishika. Tukifahamu kuwa Uzima wa mtu haupo katika urembo alionao au wingi wa vitu alivyonavyo.

Na pia kama hujampa Bwana maisha yako, bado hujachelewa ni vyema ukafanya hivyo leo, saa ya wokovu ni sasa, maadamu mlango wa Neema bado haujafungwa, utafika wakati utafungwa na wengi watatamani kuingia wasiweze, hebu wewe usiwe mmoja wao, hivyo unachopaswa kufanya hapo ulipo ni kutubu kwa kudhamiria kuacha maisha yote ya nyuma ya dhambi ya uasherati, ya wizi, utukanaji, uzinzi, ulevi, uvaaji mbaya, nk na baada ya kutubu tafuta haraka sana kushiriki na wengine kanisani, ili upate kubatizwa kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako kama hujafanya hivyo..kumbuka ubatizo ni wa muhimu sana katika kukamilisha wokovu wako na ubatizo sahihi ni wa kuzamishwa mwili wote kwenye maji na kwa jina la Bwana Yesu Kristo (kulingana na Matendo 2:38) na Baada ya hapo Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu atakayekuongoza katika kuielewa biblia na kuijua kweli yote ya maandiko na atakayekusaidia kushinda dhambi, kwasababu kwa nguvu zako mwenyewe hutaweza kushinda dhambi hata kidogo.Kwahiyo Huu ndio wakati wa kukimbilia msalabani kwa Imanueli kusafishwa dhambi zako.

Ikiwa umebarikiwa na ujumbe huu.(naomba u – Share) kwa watumishi wengine na watu wengine nao wapone. Mungu akubariki.

Pia kwa Maombezi, Ushauri au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba 

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/05/13/tulichunguze-umbo-la-yesu-na-mwenendo-wake/