AGANO LAKO LINABEBWA NA NANI?.

by Admin | 10 July 2019 08:46 pm07

Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe daima. Ni siku nyingine tena Mungu wetu katuangazia jua lake, Hivyo ni vizuri pia tukichukua muda mchache kuyatafakari maneno yake ya uzima. Somo la leo linauliza je! agano lako linabebwa na Nani.?

Wana wa Israeli walipokuwa Jangwani, Mungu alifanya nao agano, Na agano lenyewe ndio ile torati ambayo Mungu alimpa Musa, baadaye Mungu akawachongea zile amri 10 alizoziandika kwa kidole chake mwenyewe kuwa kama ishara ya agano alilioingia nao, ndipo Musa akaagizwa achonge sanduku maalumu ili aziweke ndani yake. Na sanduku hilo ndilo linaloitwa sanduku la Agano.

Na agano hilo lilikuwa ni la daima, ikiwa na maana kuwa mahali popote wana wa Israeli watakapokwenda ni lazima liwatangulie. Sio jangwani tu peke yake, bali mpaka huko watakapokwenda Kaanani liambatane nao..Sasa basi Kwakuwa sanduku hilo litakuwa ni la kuhama nalo, hivyo basi Mungu aliweka utaratibu wa watu maalumu watakaolibeba, ilikuwa sio kujiamulia tu labda mtu yoyote alibebe leo kesho mwingine, hapana Mungu aliliteua kabila moja, kabila la Lawi, tena katikati ya hao walawi ni makuhani tu ndio waliokuwa wanalibeba kwa zamu, mtu mwingine yoyote hakuruhusiwa kulisogelea wala kuligusa, kwani kwa kufanya hivyo atakuwa anajitafutia mwenyewe mauti. (Yoshua 3:3). Na Mungu alifanya hivyo kwa kwasababu maalumu kabisa ambazo sisi tuliozaliwa katika agano jipya ndio tunazielewa vizuri.

Na ndio maana ukiangalia karibu kila mahali, wana wa Israeli walipokuwa wanahama kutoka sehemu moja hadi nyingine makuhani ndio waliolichukua sanduku lile na kutangulia mbele yao. Lakini sasa ilifika wakati Mfalme Daudi, alipokuwa amestarehe katika ufalme wake, akakusudia kulitoa sanduku la Agano kutoka kule Shilo mpaka Yerusalemu mji wake, Yeye bila kukaa chini na kusoma kitabu cha maagano kinaeleza nini (Torati ya Musa) inafundisha nini kuhusu kulibeba sanduku la agano, yeye akabuni wazo aliloliona kuwa bora zaidi, akakusanya umati mkubwa wa watu, na wakuu wake wote, akaandaa gari zuri imara, na ng’ombe wenye nguvu watakao lisukuma lile gari litakalobeba lile sanduku la agano.

Pengine aliona walawi kwa umbali wote ule hawataweza kulibeba, inahitajika wanyama wenye nguvu ili sanduku liwe katika hali ya usalama zaidi.. Ni kweli Daudi alikuwa na Nia nzuri kwa Mungu wake, na ndio maana wakati lipo safarini linakuja alikuwa anamchezea na kumwimbia Mungu kwa nguvu zake zote pamoja na wale watu waliokuwa pamoja naye….

Hakuzingatia usemi wa Samweli “kutii ni bora kuliko dhabihu”. Hakujua kuwa Mungu anatembea katika kanuni zake tu, haijalishi mtu atajitoa kwake kiasi gani, haijalishi unamwimbia kiasi gani, haijalishi ataonyesha bidii kiasi gani kama amehalifu kanuni zake mabaya lazima yamkute…

Muda mfupi baadaye tunaona wale ng’ombe waliowatazamia watalifikisha sanduku, walikunguwaa katikati ya safari, na sanduku likawa katika hati hati ya kudondoka ndipo Yule Uza, mmoja wa wale waliokuwa wanaliendesha lile gari akaruka haraka ili kwenda kulizuia sanduku lisidondoke, Lakini Mungu akampiga pale pale akafa…

2 Samweli 6:6 “Hata walipofika kwa uga ya Nakoni, Uza akalinyoshea mkono sanduku la Mungu, akalikamata kwa maana wale ng’ombe walikunguwaa.

7 Ndipo hasira ya Bwana ikawaka juu ya Uza; naye Mungu akampiga huko kwa kosa lake; hata akafa pale pale penye sanduku la Mungu.

8 Daudi akaona uchungu kwa kuwa Bwana amemfurikia Uza; akapaita mahali pale Peres-uza hata leo.

9 Naye Daudi akamwogopa Bwana siku ile; akasema, Litanijiaje sanduku la Bwana?

10 Basi Daudi hakutaka kulileta sanduku la Bwana kwake mjini mwa Daudi; ila Daudi.”

Shangwe zote ziliisha pale pale, mpaka Daudi akaogopa kulifikisha sanduku la Agano Yerusalemu tena, akaliacha nyumbani kwa mtu mmoja aliyeitwa Obed-edomu, kwa muda wa miezi mitatu. Ndipo alipoona Mungu anambariki Obedi-edomu akagundua kuwa tatizo halikuwa kwenye sanduku isipokuwa kwake yeye.

Akasoma torati akafahamu kuwa ni makuhani wa kilawi tu ndio wanapaswa kulibebe sanduku la agano na si mwanadamu mwingine yoyote, wala mnyama, wala gari. Hivyo Daudi akawaandaa Walawi kwenda kulichukua kutoka kwa Obedi-edomu mpaka Yerusalemu.

1Nyakati 15:12 “akawaambia, Ninyi ni vichwa vya mbari za baba za Walawi; jitakaseni, ninyi na ndugu zenu, ili mlipandishe sanduku la Bwana, Mungu wa Israeli, mpaka mahali pale nilipoliwekea tayari.

13 Kwani kwa sababu ninyi hamkulichukua safari ya kwanza, Bwana, Mungu wetu, alitufurikia, kwa maana hatukumtafuta sawasawa na sheria”.

Ndipo Tunasoma Daudi akamwimbia tena,Mungu kwa mara nyingine, kwa nguvu zake zote, na kwa furaha, mpaka walipotimiza lengo lao.

Kiburi cha namna hii tunakiona kwa mfalme mwingine wa Israeli aliyeitwa Uzia, ambaye Mungu alimpenda sana, kwa bidii yake ya kumtafuta, hivyo alimfanya awe mkuu sana duniani jina lake likavuma, akawa na jeshi kubwa na silaha nyingi za vita, na utajiri usio kuwa wa kawaida, lakini ilifika wakati akataka kumfukizia Mungu uvumba hekaluni kwake, mambo ambayo yanafanywa na makuhani tu peke yao, lakini baada ya kuonywa na kutakaa kuonyesha kuwa anampenda Mungu zaidi ya maagizo yake, akaenda kuvukiza uvumba hekaluni pa Bwana, ndipo Mungu akampiga na ukoma mbaya ambao ulimfanya akae tu nyumbani kwake mpaka siku ya kufa kweke. soma (2Nyakati 26)

Na sisi pia wa agano jipya, pale tunapookolewa kwa damu ya YESU KRISTO, tunakuwa tunaingia Agano na Mungu..Na agano hili Mungu haweki mtu yoyote tu ili alibebe mbele yetu, hapana, alishamchagua mtu wake, ambaye ni KUHANI, Na huyu si mwingine zaidi ya BWANA YESU KRISTO…Mungu sikuzote huwa anamtazama huyu ili kuturehemu sisi, anamtazama huyu ili kutubariki sisi, anamtazama huyu ili kutupa neema, katika kila hatua ya safari yetu ya wokovu tunayopitia hapa duniani, kila mahali tutakapokuwepo huyu Kuhani Mkuu anatakiwa atembee mbele yetu kulibeba Agano letu.

Lakini pale inapotokea hatutaki kumweka Kristo mbele, tunaweka madhehebu yetu mbele, pengine kwasababu tunayaona ni makubwa, yameenea kila mahali duniani kote, yana washirika wazuri na wengi, na utaratibu mzuri, ni sawa na tumechagua Ng’ombe alibebe agano letu..Haijailishi tunamaanisha vipi kumwabudu Mungu kwa unyenyekevu wote, haijalishi tunamtumikia Mungu kwa nguvu zetu zote, hasira ya Mungu ipo juu yetu, kwasababu tumeuacha uongozi wa YESU KRISTO, tunafauata ungozi wa wanadamu, na dini zetu na madhehebu yetu.

Ikiwa leo hii unahubiriwa na unaona kabisa maandiko yapo wazi, kuwa ibada za sanamu ni dhambi, hakuna ubatizo wa kichanga, ulevi ni dhambi, lakini kwasababu dhehebu lako haliamini hivyo basi unaweka kapuni maonyo hayo ya Kristo Yesu Mwenyewe. Nataka nikuambie kuna wakati utafika huyo ng’ombe unayemwamini atakunguwaa na huo ndio utakuwa mwisho wako.. Dini na madhehebu yanapofusha watu macho sana, tunayatanguliza madhehebu yetu mbele na huku nyuma Kristo yupo mbali na maisha yetu. Itatufaidia nini, tupate vipaimara vyote, na komunyo zote, na kushika sakramenti zote, na kuitwa waimbaji maarufu, na maaskofu wakuu wakati msalaba umefarakana na sisi?

Tubu leo hii, mwamini Yesu, acha Neno la Mungu likuongoze (biblia), na si dhehebu wala, dini wala maneno ya mtu yoyote. Fuata Neno, liishi Neno, hapo ndipo sehemu salama, kwasababu Mungu siku zote anatembea katika kanuni zake na si mitazamo ya watu. Tuyafanye maneno yetu kuwa uongo na ya Mungu kuwa kweli.

Ubarikiwe sana.

Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

NINI MAANA YA KUISHI KWA KUUKOMBOA WAKATI?

NINI MAANA YA KUTOKA KATIKA MADHEHEBU?

JE! WEWE NI MWANA WA IBRAHIMU?

ALAMA KATIKA VIPAJI VYA NYUSO.


Rudi Nyumbani

 

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/07/10/agano-lako-linabebwa-na-nani/