by Admin | 1 September 2019 08:46 am09
JIBU:
Mathayo 2:10 “Nao walipoiona ile nyota, walifurahi furaha kubwa mno.
11 Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; DHAHABU na UVUMBA, na MANEMANE.
Ukisoma hapo utaona zile zawadi wale mamajusi walizozipeleka ni tatu tu. Ndio tunu zenyewe nazo : (dhahabu, uvumba na manemane)…
Sasa hizi zawadi tatu kila moja ilikuwa na maana yake kubwa, Tukianza na dhahabu, wale mamajusi walifahamu kuwa aliyezaliwa ni mfalme na anastahili heshima ya kifalme na kitu chenye thamani kubwa kuliko vyote ambacho angestahili kupewa mfalme ni dhahabu, kwasababu dhahabu inaweza kubadilishwa na kuwa hata fedha na kutumiwa kwa matumizi mengine yeyote..kwahiyo hii zawadi ya dhahabu ilikuwa ni zawadi yenye manufaa kimaisha, tofauti na hizo zawadi mbili nyingine zilizobakia zenyewe zilikuwa na manufaa ya kiujumbe zaidi kuliko kimatumizi.. Kwa mfano zawadi ya UVUMBA.
Kwa kawaida uvumba sio zawadi tunaweza tukasema uzito wa kumfaa mtu kwa wakati wote, ni zawadi isiyokuwa na thamani kubwa sana,hivyo hatuwezi kivile kuiweka katika makundi ya zawadi kama zawadi , tuchukulie kwamfano Mtu kasafiri kutoka mbali tuseme Marekani halafu anakuletea zawadi ya msalaba au ufunguo..Kwa namna ya kawaida wewe unayoipokea huwezi kwenda kuiuza au kuitumia kwa matumizi yako yoyote, zaidi sana utafahamu moja kwa moja kuwa ni zawadi iliyobeba ujumbe Fulani wa ndani zaidi ya kinachoonekana, Mfano mwingine tunafahamu pale binti anapoagwa baada ya kuposwa na kwenda kuolewa huwa kuna baadhi ya zawadi zinaambatanishwa naye kutoka kwa watu wa nyumbani kwake, licha ya kupewa vitu vya ndani na mali..lakini kuna mambo madogo madogo utakuta anakabidhiwa pia na hayo ndio yana ujumbe mzito kuliko hata vile vitu vya thamani alivyopewa, kwamfano utakuta anapewa ufagio, au ungo,..Ikiwa na maana kuwa mwanamke anapaswa awe Msafi na awe anazingatia Mapishi n.k…
Hivyo hivyo na wale mamajusi walipata ufunuo wa wanayemfauata ni nani, na ndio maana walikwenda na dhahabau lakini wakaongezea kubeba na Uvumba juu yake?..
Sasa Kumbuka katika hekalu la Mungu, uvumba ulikuwa unavukizwa tu na makuhani baada ya sadaka kutolewa sasa ile damu ilichukuliwa na kupelekwa katika madhabahu ya dhahabu iliyokuwa kule patakatifu, na hapo ndipo uvumba ulikochomwa kujaza ile nyumba ya Mungu harufu nzuri ya manukato na utukufu, na kumbuka kazi hiyo aliifanya kuhani mkuu peke yake. Hii ikifunua kuwa Huyu aliyezaliwa Yesu Kristo, licha tu ya kuwa mfalme atakuja kuwa KUHANI pia, kwasababu kila kuhani lazima awe na uvumba mkononi mwake wa kuvukiza mbele za Mungu…Na Yesu Kristo ndiye kuhani mkuu wetu. Haleluya.
Waebrania 4: 14 “Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu.
15 Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi.
16 Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji”.
Kwahiyo wale Mamajusi walipata ufunuo huo kuwa Yule atakuja kuwa kuhani mkuu pia..Jambo ambalo wengi wa waliokuwa pale hawakulifahamu hilo, mpaka alipokuja kupaa mbinguni, mitume ndio wakamwandikia habari zake. Kadhalika MANEMANE, ni zao lililotoka katika miti likiwa na maana ya “Uchungu”, manemane ilitumika kutengenezea dawa, Hivyo zawadi kama ile isingeweza kuonekana inafaa sana kwa mazingira kama yale ya furaha ya kuzaliwa Mfalme duniani, lakini walifanya vile kwasababu ilikuwa inabeba ujumbe mwingine wa ndani zaidi..
Kama tafsiri ya jina lake lilivyo ilifunulia kuwa mtoto aliyezaliwa licha ya kuwa mfalme atapitia mateso na uchungu mwingi, na hilo lilikuja kujidhirisha alipoteswa na kusulibiwa kwa ajili yetu… Wakati akiwa katika safari yake ya kwenda msalabani wale askari walimchanganyia mvinyo na manemane na kumnyeshwa, lakini Bwana aliitema kwa jinsi ilivyokuwa chungu,(Soma Marko 15:23)..Gharama Bwana aliyoilipa kwa ajili ya dhambi zetu ni kubwa sana, mfalme kufa na kuteswa msalabani kwa ajili ya mtu mwenye dhambi asiyestahili kwa chochote, hakika ni jambo la neema sana.
Hivyo wale mamajusi Mungu aliwapa kuona mbali zaidi ya zile hazina walizozipeleka. Kama mamajusi ambao hawakuwa wayahudi walisafiri kutoka nchi za mbali kwa muda wa miaka miwili, ili tu kumwona mfalme YESU akiwa mchanga, tutapataje kupona sisi tulioshuhudia matendo yake makuu ya neema kuu namna hii ambayo kila siku yanatuita tutubu dhambi?. Tutapate kupona tukidharau leo!
Ubarikiwe sana.
Mada zinazoendana:
WACHUNGAJI WA BWANA MAKONDENI.
JE! SISI NI WAFALME NA MAKUHANI KWA NAMNA GANI?
KUFUKIZA UVUMBA NDIO KUFANYAJE?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/09/01/zile-tunu-dhahabu-uvumba-na-manemane-mamajusi-walizozitoa-kwa-bwana-mathayo-2-ziliwakilisha-nini/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.