by Admin | 8 September 2019 08:46 pm09
Inadhaniwa na wengi ili kwamba mtu asemehewe dhambi zake na Mungu ni lazima aongozwe sala Fulani ijulikanayo kama sala ya Toba, na kwamba mtu asipoongozwa sala hiyo basi huwezi kusamehewa dhambi zake, Na hiyo imewafanya watu wengi hata wale wasio wakristo kusema wameokoka, kisa tu huko nyuma walishawahi kuongozwa Sala ya Toba. Lakini biblia inatufundisha nini juu ya toba halisi inayopelekea kusamehewa dhambi?. Embu tufuatilie kwa pamoja tukio hili alilokutana nalo Bwana wetu Yesu na mwitikio wake jinsi ulivyokuwa, kuna jambo la Fulani nataka ulione pengine hata na wewe hujawahi kulijua japo ni habari tunayoisoma kila siku, Tusome:
Luka 7:37 “Na tazama, mwanamke mmoja wa mji ule, aliyekuwa mwenye dhambi, alipopata habari ya kuwa ameketi chakulani katika nyumba ya yule Farisayo, alileta chupa ya marimari yenye marhamu.
38 Akasimama nyuma karibu na miguu yake, akilia, akaanza kumdondoshea miguu machozi yake, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake, akiibusu-busu miguu yake na kuipaka yale marhamu.
39 Basi, yule Farisayo aliyemwalika alipoona vile, alisema moyoni mwake, Mtu huyu kama angekuwa nabii, angemtambua mwanamke huyu amgusaye, ni nani, naye ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi.
40 Yesu akajibu akamwambia, Simoni, nina neno nitakalo kukuambia. Akasema, Mwalimu, nena.
41 Akasema, Mtu mmoja mkopeshaji alikuwa na wadeni wawili; mmoja amwia dinari mia tano, na wa pili hamsini.
42 Nao walipokuwa hawana cha kumlipa, aliwasamehe wote wawili. Katika hao wawili ni yupi atakayempenda zaidi?
43 Simoni akajibu akasema, Nadhani ni yule ambaye alimsamehe nyingi. Akamwambia, Umeamua haki.
44 Akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni, Wamwona mwanamke huyu? Niliingia nyumbani kwako, hukunipa maji kwa miguu yangu; bali huyu amenidondoshea machozi miguu yangu, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake.
45 Wewe hukunibusu; lakini huyu tangu nilipoingia hakuacha kunibusu sana miguu yangu.
46 Hukunipaka kichwa changu mafuta; bali huyu amenipaka miguu yangu marhamu.
47 Kwa ajili ya hayo nakuambia, Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana; lakini asamehewaye kidogo, huyo hupenda kidogo.
48 Kisha alimwambia mwanamke, UMESAMEHEWA DHAMBI ZAKO.
49 Ndipo wale walioketi chakulani pamoja naye walianza kusema mioyoni mwao, Ni nani huyu hata asamehe dhambi?”.
Utaona pia sehemu nyingi ambazo Bwana Yesu anatamka hili Neno “UMESAMEHEWA DHAMBI ZAKO.” Watu wanachukizwa na kumwona kama ni mkufuruji, kujiamulia kumtolea mtu tu hukumu kana kwamba yeye ni Mungu, utasoma hilo pia katika (Marko 2:112) pale alipomwona Yule mtu aliyepooza na kumwambia umesamehewa dhambi zako, watu walikasirika sana na kusema huyu anakufuru..Lakini hawakuona kitu ambacho Kristo alikuwa anakiona, wao walidhani anajiamulia tu kutamka maneno yale kwa kila mtu, hata kwa Yule ambaye hana mpango na Mungu kumwambia “Umesamehewa dhambi” hapana Bali Kristo alikuwa anaona ndani kabisa kwenye vyumba vya ndani vya mioyo ya watu wale
Alikuwa anaona mioyo ya Toba, mioyo inayojutia dhambi zao, mioyo inayosema laiti Mungu angenisikia akanisamehe wingi wa dhambi zangu hizi, nitamtumikia milele, mioyo inayosema sitakaa nirudie tena dhambi hizi natuja ni kwanini nilijihusisha katika dhambi hizi,..Ndicho Bwana Yesu alichokiona ndani ya yule mwanamke na Yule mtu aliyepooza..Sasa japo kwa nje! Hawakuzungumza na Bwana lolote, lakini ndani walikuwa wanamlilia Bwana.. Na pale pale utaona Yesu anawatamkia hadharani “UMESAMEHEWA DHAMBI ZAKO”, Sasa wale watu ambao hawajui chochote na huku wakimwona yule kahaba asemi chochote, na kumsikia Bwana Yesu anazungumza maneno kama yale wanasema anakufuru. Na kumbuka Bwana hakusema “nimekusamehe dhambi” hapana! Bali alisema “umesamehewa” ikiwa na maana kuwa alikuwa ni kama anatoa taarifa ya kitu ambacho kimefanyika tayari huko mbinguni…ni sawa na wewe umwambie mtu Fulani “umesamehewa riba” hiyo haimaanishi ni wewe ndio umemsamehe, bali wewe unasimama kama mwakilishi wa kitu ambacho kimefanyika sehemu nyingine. Na ndio Mamlaka Kristo aliyokuwa nayo ya kusamehe dhambi duniani. Alikuwa hafanyi chochote isipokuwa ameona kwanza kwa Baba yake.
Yohana 5: 19 “Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile vile”.
Lakini endapo Bwana angemwona yule mwanamke amekuja na marhamu na kulia chini ya miguu yake, na kuanza kumpangusa miguu yake kwa machozi yake, na ndani ya moyo wake hana moyo wa Toba, ni Dhahiri kuwa asingemwambia yale maneno, labda angemwambia maneno mengine ya kumjenga lakini sio kumwambia amesamehewa dhambi zake.
Ndugu Mungu hategemei Sala 100 za toba unazoongozwa kila siku, hategemei unafungua kinywa chako kumkiri yeye mbele zake mara ngapi na kulia kwa kupaza sauti ya kuomba msamaha mara ngapi..Ikiwa ndani yako hakuna moyo wa kudhamiria kabisa kugeuka moja wa moja kuacha dhambi na kumfuata Kristo,..Toba yako ni batili.
Mtu mmoja anaweza akawa ni muuaji, jambazi na gaidi lakini siku moja akajutia makosa yake na kusema kuanzia leo Mungu wangu ninakugeukia na haya mambo siyataki tena, na akayaacha kweli akaanza kumtafuta Mungu, lakini wewe unayekwenda kila siku madhahabuni pa Mungu na kulia daima na kumwambia Mungu nisamehe, unaongozwa kila siku sala ya Toba lakini bado huku nyuma unazini kisiri siri, unatazama picha chafu za ngono kisirisiri, unakunywa pombe kisirisiri unajiita ni mshirika wa siku nyingi kanisani nataka nikuambie ukweli ni kwamba Mungu “HAKUWAHI KUKUSAMEHE DHAMBI ZAKO”.
Bwana anaisamehe mioyo ya Toba, sio midomo ya toba.
Hivyo hatupaswi kujidanganya kwa namna yoyote ile. Toba ya kweli haipo midomoni bali moyoni, Iwe ni kwa sala au sio kwa sala kinachojalisha ni kugeuka kwa dhati ndani ya moyo, na kujutia kile kitu na kusema sifanyi tena kwa vitendo..Je! wewe umegeuka? kama bado basi wakati ndio huu, fanya uamuzi wa busara usio na majuto, mguekie yeye ili upokee msamaha halisi na wa kweli kutoka Mbinguni kwa Mungu Baba..
Ubarikiwe sana.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada zinazoendana:
SAMEHE KUTOKA NDANI YA MOYO WAKO.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/09/08/toba-igusayo-moyo-wa-bwana-2/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.