MAFUMBO YA MUNGU.

by Admin | 16 September 2019 08:46 pm09

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo, karibu tuyatakari maandiko pamoja, lakini kabla hatujaendelea mbele zaidi naomba ulitafakari fumbo hili fupi kwa muda kidogo, ukipata au ukikosa jibu endelea kusoma habari hii, nitakupa majibu mbeleni… Fumbo lenyewe ni hili “Daudi ananyoa hata mara mia kwa wiki lakini kidevu chake bado kina ndevu nyingi, Je! Unaweza kunielezea ni kwanini? ”….Tafakari kisha utanipa jibu baadaye.

Lengo la kusema hivi ni kuwa kitabu kinachoitwa biblia ni kitabu kilichobeba mafumbo mengi sana, ambayo wakati mwingine majibu yake yanaweza yakawa ni marahisi kama tu tukimruhusu yeye aliyeyatunga kutufunulia, lakini pale tunapokosa kupata majibu sahihi, hatutaki kukiri kuwa hatufahamu, matokeo yake tunaishia kuona labda biblia ilikosewa au pengine tunaishia kutoa tafsiri zisizo sahihi ili tu tuonekane tunafahamu kile kilichoandikwa, hakuna asiyejua biblia imejaa mafumbo mengi sana, lakini miongoni mwa hayo ni suala la uungu wa kiMungu, kama vile biblia inavyosema Mungu ni MMOJA tu, lakini inakuwaje Yesu naye anaonekana kuwa ni Mungu, Roho Mtakatifu naye ni Mungu kama Mungu ni mmoja…

Sasa tunapokosa majibu ya maswali kama haya huwa tunaishi kusema Mungu ni mmoja ila kagawanyika katika nafsi tatu zinazojitegemea..Majibu tunayoyatoa ni marahisi sana, lakini hatujui kuwa tunazua maswali mengi, hata kwa wale ambao hawamjui Mungu wa wakristo, ndio linawafanya waende mbali zaidi ya ukristo wanapopata majibu kama hayo ambayo hayaoenekani kwenye biblia..Lakini hiyo yote ni kwasababu tumeukwepa uongozo wa Roho Mtakatifu kutufundisha ni jinsi gani Kristo ni Mungu na Roho Mtakatifu ni Mungu Yule Yule asiyekuwa na mshirika mwingine pembeni.

Kipengele kingine ambacho nacho kimezua utata mwingi, tunakipata katika mstari huu:

Mathayo 16:13 “Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?

14 Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.

15 Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?

16 Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.

17 Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.

18 Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.

19 Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni”.

Mstari huu, unatafsiriwa na wengi hususani kanisa Katoliki kuwa mwamba huo unaozungumziwa kuwa Bwana Yesu atalijengea kanisa lake ni Petro, hivyo inaamika tangu zamani kuwa sisi sote tumejengwa juu ya Petro, na yeye ndiye PAPA wa kwanza, na kanisa la Kwanza ndio kanisa Katoliki.. Lakini kiuhalisia hapo Kristo hamzungumzii Petro bali anazungumzia juu ya UFUNUO ambao Petro alifunuliwa na Baba yake wa mbinguni wa kumjua YESU KRISTO ni nani, ambao wengi sana walishindwa kuuju, huo ndio mwamba ambao kanisa linajengwa juu yake?….Kwamba kwa ufunuo huo ndio atakalolijengea kanisa lake na malango ya kuzimu hayatalishinda…

Hivyo pale alikuwa hazungumziwi Petro na Petro hakuwa Papa, yeye alioa ma-papa huwa hawaowi, Yeye hakusujudia sanamu mahali popote wala kumwomba Mariamu dua mahali popote, lakini Mapapa wanafanya hivyo….vile vile Petro alimkana Bwana, lakini kanisa haliwezi kumkana Bwana, vilevile injili kwetu kwa mataifa ililetwa na mtume Paulo kuliko hata Mtume Petro , hivyo ambaye angestahili zaidi kuwa mjenzi wa kanisa basi angekuwa ni Paulo na sio Petro…Hivyo tunapaswa tumwombe Roho Mtakatifu atusaidie sana katika kuyachambua maandiko..

1Wakorintho 2:10 “Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata MAFUMBO YA MUNGU.

11 Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu.”

Kadhalika leo hii tukikosa shabaha ya ufunuo wa Roho kumhusu Yesu Kristo katika katika maisha yetu, hatutaweza kusimama wala kumshinda shetani, Tunapomwona Yesu Kristo kwa kiganja chake, mtoa rizki tu, wa kubariki tu, wa kutusaidia kutatua matatizo yetu ya kimwili tu!…Na hatumfahamu kama mwana wa Mungu aliyetumwa kutuokoa, na kututakasa na dhambi zetu, kisha atupe uzima wa milele.. hatutakaa kamwe tumshinde shetani. Tutakuwa matajiri wa mali, lakini maskini wa roho.

Sasa tukirudi kwenye fumbo letu juu, linalouliza “Daudi ananyoa hata mara mia kwa wiki lakini kidevu chake bado kina ndevu nyingi, Je! Unaweza kuelezea ni kwanini”?..Jibu ni kuwa Daudi ni KINYOZI, huwa ananyoa vichwa vya watu wengi kila siku, hivyo basi hilo halihusiani na kidevu chake…je! ulifikiri hivyo? Au ulifikiri kwamba Kidevu cha Daudi ndicho kinachonyolewa mara mia kwa wiki?..Kama ulifikiri kuwa ni kidevu cha Daudi ndicho kinachonyolewa mara mia kwa wiki, na ukatafuta na ukajitafutia sababu za nywele hizo kuota kwa kasi kiasi hicho basi fahamu kuwa ulikosea… Na biblia sehemu nyingi ndio ipo kwa mafumbo kama hayo hayo…Unasoma hivi, na kufikiri hicho unachokisoma ndio tafsiri yenyewe kumbe, umekosea pakubwa, tafsiri yake ni nyingine tofauti na hiyo uliyokuwa unaifikiria wewe, na Yesu Kristo kumwelewa haihitaji kumhakiki kwa andiko peke yake bali kwa Roho Mtakatifu, kwasababu maandiko pasipo Roho yanapotosha.

2 Wakorintho 3: 6 “Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, BALI WA ROHO; KWA MAANA ANDIKO HUUA, BALI ROHO HUHUISHA”.

Bwana atusaidie sote tuweze kumwelewa yeye kwa utimilifu wote, kama anavyotaka yeye sisi tumwelewe.

Ubarikiwe na Bwana.

Kama hujampa Kristo Maisha yako, mlango upo wazi sasa, lakini hautakuwa wazi hivyo si siku zote, parapanda ya mwisho inakaribia kulia, na Kristo kuchukua watu wake waliokombolewa kwa damu yake, je! Una uhakika umo miongoni mwao?..una uhakika wa kwenda na Bwana atakapokuja?..Uamuzi ni wako.

Maran atha! Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

ANGALIA JINSI USIKIAVYO:

FIMBO YA HARUNI!

JE! MBINGUNI KUNA MALAIKA WA KIKE?. NA JE! TUKIFIKA MBINGUNI TUTAFANANA WOTE?


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/09/16/mafumbo-ya-mungu/