by Admin | 28 September 2019 08:46 pm09
Kuna nguvu ya kipekee sana, inayoendelea duniani kote leo, hiyo inawavuta watu kwa Kristo, Nguvu hiyo ni nguvu ya Roho Mtakatifu, inazungumza mioyoni mwa watu, ikiwashawishi kuwavuta kwa Mungu. Nguvu hiyo ndio ile ile nguvu iliyokuwa inawavuta wale Wanyama kipindi cha Nuhu, waielekee Safina.
Kipindi kifupi kabla ya gharika kushuka juu ya nchi, ghafla tu Nuhu alianza kuona Wanyama wanasogea karibu na mahali Safina ilipokuwa inatenengenezwa, pengine kaamka asubuhi ghafla anaona simba wawili wakike na kiume wamelala pembezoni mwa kichaka Fulani kilichopo karibu na Safina ilipokuwepo, na wamekaa kama wanasubiri kuingia mahali Fulani hivi, halafu wamekuwa wapole jambo ambalo si la kawaida.
Mita kadhaa mbele pengine anaona tembo wamesimama kama vile wanahaja na kitu Fulani, nao hawana madhara…baada ya siku moja nyingine au mbili anaona chui, swala…na wote wakiwa na shauku ya kuingia ndani ya Hiyo nyumba yao mpya (safina). Kama vile kuku, au ng’ombe au mbuzi wanavyokuwaga na shauku ya kuingia mabandani mwao kila inapofika jioni..Giza linapoingia utaona kuku wamekusanyika mlangoni mwa banda lao wakingoja mlango ufunguliwe waingie…
Ndivyo ilivyokuwa kipindi kile cha gharika, shauku ya wale Wanyama kuingia ndani ya Safina, ilikuwa ni kubwa mpaka ikazima ukali wao, wote wakawa wapole wakitii na kusubiri amri ya kuingia ndani ya Safina.
Sasa ni nani aliowaongoza hao Wanyama mpaka wafike mlangoni mwa Safina?..je! walihubiriwa na watu kwamba kuna gharika inakuja hivyo wajiepushe?..Jibu ni hapana!…Kuna nguvu Fulani ndani yao iliyokuwa inawasukuma waende mahali ambapo ni salama Zaidi…Kuna mazingira Fulani yaliwafanya wahisi kuwa mwisho umefika na kuna mauti kubwa inakuja mbeleni(hukumu), na Zaidi ya hayo kuna kitu kiliwafanya pia wahisi kuwa kuna Maisha yataendelea baada ya hukumu hiyo, ili kuendelea kuishi hayo Maisha yanayokuja, daraja lake ni kutafuta hifadhi sasa.
Unajua hata watabiri wa vimbunga na matetemeko, wanatumia ishara ya Wanyama kutabiri maafa?..Endapo wakiona kuna tabia ya kipekee ya Wanyama imezuka mahali Fulani, labda ndege wote wameondoka mijini na kukimbilia milimani au mahali pa mbali, na wakati si jambo la kawaida, wanatangaza kuwa kuna janga litatokea siku si nyingi, hivyo watu wachukue tahadhari, na kweli baada ya kipindi Fulani kifupi labda wiki, mwezi au mwaka janga linatokea mahali hapo.
Kama Mungu, aliiachia hii nguvu ya wokovu hata kwa Wanyama (Warumi 8:19-22), si Zaidi wanadamu?…Hata sasa hii nguvu ipo, Wewe mwenyewe unajua ndani yako kuna nguvu Fulani inakushuhudia kwamba tunaishi siku za mwisho! Na kwamba siku moja mwisho wa mambo yote utafika, na ulimwengu utahukumiwa….Na hiyo nguvu haiishii hapo, inazidi kukushuhudia kwamba kutakuwa na maisha baada ya hukumu…Na pia haiishii hapo, inakusukuma kuifuata Safina mahali popote ilipo…Usiipuuzie hiyo sauti!!.
Nuhu wetu wa Sasa ni Yesu Kristo, Safina ni Neno lake, Wote aliopewa Nuhu walikwenda kwake kadhalika wote aliopewa Bwana Yesu na Baba walikwenda kwake na wanakwenda kwake sasa hivi..
Yohana 6:37 “Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe.
38 Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka”.
Yohana 6: 43 “Basi Yesu akajibu, akawaambia, Msinung’unike ninyi kwa ninyi. Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho”.
Muda unakwenda kwa kasi sana! Je! Hii nguvu bado ipo ndani yako? Au umeizimisha? Je! Kama ipo Umeikaribia Safina kiasi gani?..Umemkaribia Nuhu kiasi gani?, Jibu unalo..Fanya maamuzi thabiti kabla hazijafika siku za hatari, ambazo wengi watatamani waingie safinani na watashindwa…
Luka 13:23 “Mtu mmoja akamwuliza, Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache? Akawaambia,
24 Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze.
25 Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana, tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako;
26 ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu.
27 Naye atasema, Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu.
28 Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje”.
Biblia inaposema kama zilivyouwa siku za Nuhu ndivyo itakavyokuwa siku za kuja kwake mwana wa Adamu, tunapaswa tujifunze pia tabia kama hizi, za kuvutwa safinani, vile vile tunapaswa tujue kuwa sio wanyama wote waliingia bali ni wachache..Vivyo hivyo leo hii wanaoitii hiyo sauti ni wachache,..Tujitahidi na sisi tuwe miongoni mwao, kwa kuitikia wito huo wa Mungu uitao mioyoni mwetu kila siku.
Tafadhali share na wengine
Bwana akubariki.
Mada Nyinginezo:
FAHAMU KINACHOMGHARIMU MUNGU, KUTOA URITHI WAKE.
JE! MUNGU ATAIANGAMIZA DUNIA TENA BAADA YA GHARIKA YA NUHU?
MANENO HAYA YANA MAANA GANI? “..KWA SABABU HAMTOI ROHO KWA KIPIMO. (YOHANA3:34)
JE! MUNGU ANAUPENDELEO KWA WANAUME ZAIDI YA WANAWAKE?
JE! KUFANYA MASTURBATION (PUNYETO) NI DHAMBI?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/09/28/ipo-nguvu-ituvutayo-kwa-kristo-ithamini/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.