Mbinguni ni sehemu gani?

by Admin | 2 October 2019 08:46 pm10

JIBU: Ili tusichanganyikiwe jambo la muhimu  tulinalopaswa kujua ni kuwa Katika biblia Neno “mbinguni” limetumika kuwakilisha sehemu tofauti tofauti tatu.

Sehemu ya kwanza ni anga hili ambalo lipo juu yetu: Ambalo ndilo hili tunaloliona lenye nyota, mawingu, mwezi jua na sayari, ambalo ndege wote wa angani wanaruka na kufurahia, biblia imelitaja kama mbingu..Tunasoma..

Isaya 55:10 “Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula;

11 ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.”

Luka 17:24 “kwa kuwa, kama vile umeme umulikavyo toka upande huu chini ya mbingu hata upande huu chini ya mbingu, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu katika siku yake”.

Sehemu ya Pili ya mbingu ni makao ya Mungu yalipo: Na hii ipo katika Roho, sehemu ambayo Mungu na malaika zake wanaishi, hatuwezi kuiona kwa jicho la kibinadamu wala hatuwezi kufika huko kwa kifaa chochote cha kibinadamu, lakini ni mahali halisi kabisa. Tiketi ya pekee ya kufika huko biblia inatuambia ni Yesu Kristo tu, Na hii mbingu ni pana sana ndio imejumuisha ile mbingu mpya na nchi mpya ambayo itakuja kuwa ni makao ya watakatifu baadaye, pamoja na ile paradiso (peponi) kule ambapo wale wote waliokufa zamani na wanaokufa sasa hivi katika Kristo wanahifadhiwa kwa muda wakisubiria ufufuo siku ile ya Unyakuo ili kwa pamoja waingie katika makao ya Mungu mwenyewe yaliyo juu sana na ndio maana utaona mtume Paulo alinyakuliwa mpaka mbingu ya Tatu, mbingu hii ya tatu ni hiyo ya makao ya Mungu mwenyewe,  akaonyeshwa sehemu ya maono ya huko, na kusema mambo yaliyo huko hayajuzu hata mwanadamu kuyatamka,(2Wakorintho 12:2-4). na ndiko watakatifu waliokombolewa watakapokwenda siku ile ya Unyakuo itakapofika, ni mahali patakatifu na pasafi ambapo mtu yeyote mchafu hataingia..

1Wafalme 8:27 “Lakini Mungu je? Atakaa kweli kweli juu ya nchi? Tazama, mbingu hazikutoshi, wala mbingu za mbingu; sembuse nyumba hii niliyoijenga!”

1Timotheo 6:16 “ambaye yeye peke yake hapatikani na mauti, amekaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa; wala hakuna mwanadamu aliyemwona, wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye hata milele. Amina.”

Na sehemu ya tatu biblia inapataja kama mbinguni ni mahali pa juu sana, makao ya juu sana: Mahali ambapo Mungu pekee ndiye anayestahili kuwepo, jambo ambalo hata hapa duniani linaweza kufikiwa,

Watu walio ndani ya Yesu, ambao wameokoka kikamilifu kwa kumwamini Yesu na kubatizwa, katika ulimwengu wa roho, ni sawa na wameketi pamoja na Kristo mbinguni..

Waefeso 2:5 “hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, tumeokolewa kwa neema.

6  Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu;”

Kadhalika pia, Ufalme wowote au mtu yeyote anayetafuta kuinuliwa ziadi ya vitu vingine vyote huyo katika roho anaonekana anakipandia cheo cha Mungu kilipo, na Mungu yupo mbinguni, hivyo anaonekana kama amefika mbinguni.

Danieli 4:19 “Ndipo Danieli, aliyeitwa jina lake Belteshaza, akashangaa kwa muda, na fikira zake zikamfadhaisha. Mfalme akajibu akasema, Ee Belteshaza, ndoto ile isikufadhaishe wala tafsiri yake. Belteshaza akajibu, akasema, Bwana wangu, ndoto hii iwapate wao wakuchukiao, na tafsiri yake iwapate adui zako.

20 Ule mti uliouona, uliokua, ukawa na nguvu, urefu wake ukafika mpaka mbinguni, na kuonekana kwake mpaka dunia yote;

21 ambao majani yake yalikuwa mazuri, na matunda yake mengi, na ndani yake chakula cha kuwatosha wote; ambao chini yake wanyama wa kondeni walikaa, na ndege wa angani walikuwa na makao yao katika matawi yake;

22 ni wewe, Ee mfalme, uliyekua, na kupata nguvu; maana ukuu wako umekua na kufika mpaka mbinguni, na mamlaka yako yamefika mpaka mwisho wa dunia.

Mathayo 11:23 “Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa mpaka mbinguni? Utashushwa mpaka kuzimu; kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika katika Sodoma, ungalikuwapo mji huo hata leo.”

Isaya 14:12 “Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa!

13 Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini.

14 Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye Aliye juu.

15 Lakini utashushwa mpaka kuzimu; Mpaka pande za mwisho za shimo”.

Hivyo kwa vyovyote vile, tunapaswa tujitahidi ili tufike huko, si kwa kujiinua tukiyatumainia haya Maisha, bali kwa kupitia Yesu Kristo, kwasababu biblia inasema mambo tuliyoandaliwa huko, jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia.

Ubarikiwe.


Mada Nyinginezo:

JE! NI KWELI DUNIA ILIUMBWA TAKRIBANI MIAKA 6000 ILIYOPITA? NA JE! SHETANI ALIKUWEPO DUNIANI WAKATI DUNIA INAUMBWA?

TUMEAMBIWA TUNAPOSALI TUSIPAYUKE-PAYUKE, JE! HUKO KUPAYUKA PAYAUKA NDIO KUPI?

JE! KUNA DHAMBI KUBWA NA NDOGO?

NI NANI ANAYETAWALA DUNIA KATI YA MUNGU NA SHETANI?.


Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/10/02/mbinguni-ni-sehemu-gani/