Mtakatifu ni Nani?

by Admin | 4 October 2019 08:46 am10

 JIBU: Tafsiri ya kibiblia ya MTU MTAKATIFU ni tofauti na tafsiri ya kiulimwengu.
 
Ulimwengu unatafsiri Mtu mtakatifu ni mtu yeyote anayetenda matendo mema! mtu asiyetenda dhambi!..mtu anayekubalika na asiye na mawaa,
 
Lakini Biblia haitafsiri hivyo, kwasababu hakuna mwanadamu yeyote anayeweza kusimama mbele za Mungu kwa Matendo yake, na kujigamba mbele zake, wanadamu wote tunatenda dhambi kwa namna moja au nyingine aidha kwa kujua au kwa kutokujua. Na hivyo wakati unapojiona upo sawa, kumbe haupo sawa..wakati unajiona ni msafi kumbe ni mchafu n.k
 
Sasa Biblia inamtaja mmoja tu ambaye hakuwa na dhambi hata moja na huyo si mwingine zaidi ya YESU KRISTO peke yake! huyo ndiye biblia imemtaja kuwa mtakatifu, kwasababu alizaliwa bila dhambi na aliondoka duniani bila dhambi hata moja. Huyo peke yake ndiye anayeweza kusimama mbele za Mungu kwa matendo yake. Na ndiye pekee Mungu anayemwangalia kuwa ni Mtakatifu. Wengine wote tumetenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu.
 
Warumi 3: 23 “kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;
24 wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu”
 
Sasa Kwa kupitia huyo sisi wengine tutakaomwamini yeye ndio tutahesabiwa kuwa ni watakatifu,. Kama mtu yeyote hatakuwa ndani ya YESU hawezi kuonekana mtakatifu mbele za Mungu, hata kama anajiona ni mkamilifu kiasi gani, hata kama atatenda matendo ya haki kiasi gani…mbele za Mungu ni kama Uchafu tu!
 
Yesu ni kama vazi letu la nje sisi tulio wachafu! Ukimvaa Yesu mbele za Mungu hakuoni wewe, bali anamwona Yesu mwanawe ambaye ni Mtakatifu, hivyo na wewe unaonekana mtakatifu kwa ajili yake. Hiyo ndio maana ya NEEMA, Tunahesabiwa HAKI (yaani tunahesabiwa kuwa watakatifu) bure kwa njia tu ya kumwamini YESU KRISTO. Hapo ndipo mtu unaouna umuhimu wa YESU kuja duniani, Kwahiyo watakatifu ni wale walio ndani ya YESU tu!.
 
Hivyo wale wanaosema duniani hakuna watakatifu, ni kweli kwa mtazamo wa kibinadamu, lakini kwa mtazamo wa Mungu duniani wapo watakatifu maandiko yanatumabia hivyo katika:
 
Zaburi 16:3 “Watakatifu waliopo duniani ndio Walio bora, Hao ndio niliopendezwa nao”.
 
Na hawa ndio wale wale wote walio ndani ya YESU KRISTO.
Sasa utauliza! Ina maana tukiwa ndani ya Yesu hata kama tukitenda dhambi za makusudi, tutazidi kuonekana NI watakatifu mbele za Mungu? jibu ni la! hakuna mtu yeyote aliye ndani ya Kristo, akawaza tena kutenda dhambi za makusudi, hakuna mtu aliye ndani ya Kristo akafanya uasherati, au akalawiti au akaua..ukiona mtu anatenda dhambi za Makusudi huyo bado hajawa ndani ya YESU, bado ni wa Ulimwengu. (Soma 1Yohana 3:9 na Warumi 6:1-2 )..
 
Kwasababu mtu yeyote aliyempokea YESU huwa anapokea hapo hapo kipawa cha Roho Mtakatifu, ambaye huyo kazi yake ni kumwongoza, kumfundisha na kumpasha habari ya mambo yote..kwahiyo mtu wa namna hiyo moja kwa moja atajikuta anatamani kupiga hatua mbele kila siku kuelekea ukamilifu na sio nyuma…Hata ile tamaa ya kufanya dhambi huwa inakufa yenyewe ndani yake, na hivyo hawezi kutenda dhambi mwenyewe za makusudi.
 
Ubarikiwe.

 


Mada Nyinginezo:

JEHANAMU NI NINI?

MANENO YA MUNGU YANAPINDULIWAJE?

ROHO I RADHI, LAKINI MWILI NI DHAIFU.

USITAFUTE FAIDA YAKO MWENYEWE BALI YA WENGINE.

NJAA ILIYOPO SASA.

JIKANE NAFSI MTEULE WA MUNGU.


Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/10/04/mtakatifu-ni-nani/