MBINGU MPYA NA NCHI MPYA. (Sehemu ya 3)

by Admin | 27 August 2021 08:46 am08

Sasa kumbuka kama tulivyoona katika malaka zilizotangulia, huko nyuma kote baada ya Mungu kuiumba dunia, alichokuwa anafanya ni UKARABATI TU, lakini sio uumbaji mwingine. Lakini hatua hii ambayo ndio ya mwisho Mungu atafanya uumbaji mwingine. Na uumbaji huu sio kwamba ataiondoa dunia yote, na kuitupa motoni, kama wengi wanavyodhani hapana, bali atafanya kama vile atakavyofanya kwenye miili yetu mipya ya kimbinguni.

Sasa kama bado hujasoma sehemu ya kwanza na ya pili, basi bofya hapa chini upitie kwanza, ndipo uendelee na sehemu hii ya tatu na ya mwisho>>

MBINGU MPYA NA NCHI MPYA. (Sehemu ya 1)

MBINGU MPYA NA NCHI MPYA. (Sehemu ya 2)

Siku ile tutakapoenda mbinguni, Mungu atatushushia miili mipya isiyokuwa ya udongo, bali imetengenezwa kwa matirio ya kimbinguni. Na itakaposhushwa , hii miili ya sasa tuliyonayo haitauliwa na kutupwa motoni, hapana bali itavaliwa au itamezwa na ile mipya ya kimbinguni, biblia inasema hivyo katika.

1Wakorintho 15.51 “Angalieni, nawaambia ninyi siri; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika,

52 kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika.

53 Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa.

54 Basi huu uharibikao utakapovaa kutokuharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa, hapo ndipo litakapokuwa lile neno lililoandikwa, Mauti imemezwa kwa kushinda.

55 Ku wapi, Ewe mauti, kushinda kwako? U wapi, Ewe mauti, uchungu wako?”.

Umeona hapo, ndivyo itakavyokuwa pia juu ya mbingu mpya na nchi mpya. Sio kwamba dunia yetu, itaangamizwa kabisa iondolewe hapana, bali ITAGEUZWA, na kuwa DUNIA ya ajabu sana, ambayo mfano wake hauwezi kuelezeka, hauwezi kulinganishwa hata kwa chembe na ulimwengu huu wa sasa. Utukufu wake, utakuwa ni wa mbali sana sana sana, tena sana.

Vivyo hivyo na hizi mbingu zilizo juu yetu yaani (sayari, nyota, magimba n.k.) Vitakuwa na mwonekano mwingine tofauti kabisa, vitaanza kuwa na uhai navyo.

Ukisoma Ufunuo 21&22 yote Biblia inatoa tabia za hiyo mbingu mpya na nchi mpya jinsi zitakavyokuwa, nazo ni hizi;

Pia ile Yerusalemu mpya, (mji wa kimbinguni), ndio utashuka juu ya hii nchi mpya na mbingu mpya. Mji ambao utakuwa ni kitovu cha ulimwengu, ambao ni bibi-arusi tu na Kristo ndio watakaouingia.

Zaidi ya yote, ni kuwa Mungu atahamisha maskani yake, na kuileta duniani. Kwa mara ya kwanza mwanadamu ataishi na Mungu, na kuuona uso wake.

Ufunuo 21:3 “Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao”.

Vilevile Muda utaondolewa, hakutakuwa tena na kitu kinachoitwa muda, kwani tutaishi Milele na milele na milele isiyokuwa na mwisho. Katika furaha na amani na vicheko daima.

Hakika ni mambo ambayo hayaelezeki, yaani tutamfurahia Mungu kila inapoitwa leo. Hizi sayari zote zisizohesabika mabilioni kwa mabilioni huko angani zitakuwa na kazi nyingi sana, hazikuumbwa ziwe ukiwa, hatuwezi kufahamu kila kitu lakini tukifika huko ndipo tutajua.

Bwana Yesu alimalizia na kusema maneno haya;

Ufunuo 22:12 “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.

13 Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho.

14 Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake”.

Ndugu yangu, kumbuka ili kufika huko, maandalizi yake yanaanza sasa. Inasikitisha kuona kuwa wapo watu ambao hawatafika huko, Ikiwa leo hii tunaishi maisha ya ukristo vuguvugu, tunasema tumeokoka lakini ulimwengu umejaa ndani yetu. Tunatazamia vipi, tuende mbinguni kwenye unyakuo?. Au tunatazamia vipi tuingie Yerusalemu mpya.

Hizi ni nyakati ambazo, si za kubembelezewa tena wokovu, ni wewe mwenyewe tu kuona, jinsi hali halisi ilivyo. Hakuna dalili ambayo haijatimia. Siku yoyote, unyakuo utapita, na dhiki kuu itaanza.

Ikiwa hujaokoka, embu leo fanya uamuzi sahihi, Tubu dhambi zako kwa kumaanisha kabisa kugeuka, kisha, nenda kabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO, sawasawa na Matendo 2:38, Kisha Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu, 

Ukikamilisha hizo hatua zote, basi ujue tayari wewe ni mwana wa ufalme, jukumu lako litakuwa ni kuutuzwa wokovu wako kwa maisha ya utakatifu na ya kumcha Mungu na ya ibada ya kweli utakayokuwa unayaishi. Ukisubiria unyakuo, na zaidi hiyo mbingu mpya na nchi mpya itakayokuja huko mbeleni.

Lakini ikiwa utahitaji msaada wa kuokoka, au kubatizwa, au swali basi wasiliana nasi kwa namba zetu hizi kwa msaada zaidi. +255693036618/ +255789001312

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

MBINGU MPYA NA NCHI MPYA. (Sehemu ya 1)

MBINGU MPYA NA NCHI MPYA. (Sehemu ya 2)

MKESHA WA KUINGIA MWAKA MPYA KILA MWAKA NI WA KUUTHAMINI SANA.

UNYAKUO.

UFUNUO: Mlango wa 1

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/08/27/mbingu-mpya-na-nchi-mpya-sehemu-ya-3/