ADHABU KALI KUTOKA KWA MUNGU, ITAMPATA MTU WA NAMNA GANI?

by Admin | 6 January 2022 08:46 am01

Mithali 15:10a “Adhabu kali ina yeye aiachaye njia;..”.

Mapigo ya Mungu yanatofautiana na mtu na mtu.. Tofauti na tunavyodhani kuwa muuaji ndiye atakayeadhibiwa sana siku ile kuliko mtu aliyeuacha wokovu.

Jibu la la! Maandiko yanatuambia, “Adhabu kali ina yeye aiachaye njia”, hasemi tu ‘adhabu’ ina yeye aichaye njia, hapana, bali adhabu KALI..

Bwana Yesu alirudia , maneno hayo hayo tena katika

Luka 12:47 “Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana.

48 Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na Zaidi”.

Leo hii inasikitisha kuona kuwa watu wengi wanakiri kwa vinywa vyao kuwa wameokoka, lakini kimatendo wapo mbali na Kristo, hawa wote ni kundi la wakristo walioicha njia, au waliojua mapenzi ya Bwana wao lakini wasiyafanye, wanaojua kuwa kutazama pornography hakumpendezi Mungu, lakini wanatazama, kuishi na mume/mke ambaye si wako ni dhambi mbele za Mungu lakini wao bado wanaendelea kuishi nao, tena wanazaa nao,

Wanaojua, kabisa kuvaa nguo za nusu uchi, na kujichubua ni dhambi, lakini bado wanaendelea kufanya mambo kama hayo,. Wachungaji na watumishi wanaojua kabisa, uasherati ni kosa kubwa sana kwa watu kama hao, lakini sasa imeshakuwa desturi yao. Hao ndio Kristo anaowazungumzia kuwa watakuwa na adhabu kali sana kule kuzimu.

Ndugu yangu, mateso yaliyopo kule, usidiriki kuyapima kwa akili zako, ni mahali ambapo hata hao wanaoteswa huko hawatamani, kukuona mtu kama wewe umefika huko, ni mateso makali sana, yasiyoelezeka, soma (Luka 16:27-29).

Na ndio maana Bwana Yesu alisema maneno haya;

Marko 9:45 “Na mguu wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima, u kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili, na kutupwa katika jehanum; [

46 ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.]

47 Na jicho lako likikukosesha, ling’oe, ulitupe; ni afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu, una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum;

48 ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki”.

Ndugu,unaposikia injili halafu huitendei kazi, ujue kuwa inageuka na kuwa adhabu kwako, na kwa jinsi unavyoendelea kuisikia ndivyo unavyojiongezea mapigo. Yathamini Maisha yako ya rohoni, siku hizi ni za mwisho, Unyakuo ni wakati wowote, Bado hujui siku zako za kuishi hapa duniani zimebakia ngapi, sikuzote kifo huwa kinakuja ghafla tu, hakina hodi je! Mimi na wewe tumejiandaaje? Kwa injili zote hizi tulizozisikia?

Ni heri tuyasalimishe Maisha yetu kwa Bwana leo, atuokoe, na kutufungua, tumaanishe kabisa kumfuata yeye bila lawama yoyote, tuweke kando mambo ya ulimwengu yanayopita, tuutafute utakatifu kwa bidii, kwasababu pasipo huo kamwe mbingu hatutaiona (Waebrania 12:14),

Lakini Ikiwa utatamani kutubu leo, na kuanza Maisha yako upya na Bwana, katika kipindi hichi kifupi tulichobakiwa nacho, basi yeye yupo tayari kukusamehe.. Ukiiomba sala hii fupi ya TOBA, ukiisema kwa Imani, basi utapokea msamaha hapo hapo ulipo.. Hivyo kama upo tayari kuyasalimisha leo Maisha yako kwa Bwana.

Hapo ulipo unaweza kutafuta mahali pa utulivu peke yako, kisha piga magoti, nyosha mkono wako mmoja juu, kama ishara ya kuyasalimisha Maisha yako kwa Bwana. Kisha, ukishakuwa katika utulivu, sema maneno haya, kwa sauti:

BABA YANGU, NAJA MBELE ZAKO, NINAKIRI KUWA NIMEKUWA MWANA MWASI MBELE ZAKO KWA MUDA MREFU, KWA WINGI WA DHAMBI ZANGU, NIMESTAHILI ADHABU NA MAPIGO MAKALI KUTOKA KWAKO, NI KWELI BWANA NILIYAJUA MAPENZI YAKO LAKINI SIKUYATENDA. LAKINI LEO MIMI MWANAO (TAJA JINA LAKO) NIMEDHAMIRIA KUYAANZA MAISHA YANGU UPYA NA WEWE.  NAOMBA UNISAMEHE BABA YANGU.

KUANZIA LEO NINAACHA NJIA ZANGU MBAYA ZOTE, NINAMKATAA SHETANI NA KAZI ZAKE ZOTE, NINAUKATAA ULIMWENGU. NAOMBA DAMU YA MWANAO YESU KRISTO, UNISAFISHE NA KUNITAKASA KABISA.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNISAMEHE. KAMA ULIVYOSEMA KATIKA NENO LAKO, YEYOTE AJAYE KWANGU SITAMTUPA NJE KWAKE. NAMI NAAMINI UMENIPOKEA, NA KUNIFANYA KIUMBE KIPYA LEO. NAOMBA UNIPE UWEZO WA KUUSHINDA ULIMWENGU NA KUUISHIA WOKOVU SIKU ZOTE ZA MAISHA YANGU.

ASANTE BWANA YESU KWA NEEMA YAKO, NA MSAMAHA WAKO.

AMEN.

Basi ikiwa umeisema sala hiyo ya Imani, fahamu kuwa Mungu anatazama moyo wako, na sio sala tu.  Yupo mwanamke ambaye alikuwa na dhambi nyingi, lakini kwa jinsi alivyomaanisha tu mbele za Yesu, kabla hata hajaomba msamaha au kujieleza chochote, muda huo huo Bwana alimwambia “umesamehewa dhambi zako”. Hiyo ni kuonyesha kuwa Toba hasaa haipo katika maneno matupu tu, bali katika moyo.(Luka 7:36-50)

Na wewe pia ikiwa toba yako, imeambatana na kuachana na huyo mume/mke wa mtu, imeambatana na kuacha kutazama picha za ngono mitandaoni milele, imeambatana na kuacha kuishi na huyo girlfriend/boyfriend ambaye hamjaona naye.. Ujue kuwa msamaha kutoka kwa Bwana umeshaupokea.

Hivyo, kuanzia leo, anza kuishi Maisha ya kuukulia wokovu, na kama hukubatizwa unapaswa ubatizwe, Ikiwa utahitaji msaada huo, basi wasiliana nasi kwa namba zetu hizi 0693036618/0789001312 tutakusaidia kwa neema za Bwana.

Pia tunayo mafundisho mengi Zaidi ya 1000, na majibu ya maswali mengi ya biblia yaliyoulizwa. yatakayokusaidia kupokea maarifa mengi juu ya Neno la Mungu, na kukusaidia kusimama imara, unaweza kuyapata katika tovuti yetu hii www.wingulamashahidi.org.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

TOBA IGUSAYO MOYO WA BWANA.

Je! Kuna dhambi kubwa na ndogo, na kama hakuna je! Mtu aliyeua na aliyetukana je watapata adhabu sawa?

Kwanini Mungu awachome watu kwenye ziwa la moto na hali yeye ndiye aliyewaumba?

TABIA YA WAZI INAYOWATOFAUTISHA MANABII WA UONGO NA WALE WA UKWELI.

Mungu anaposema “nitaliweka jina langu” ana maana gani?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/01/06/adhabu-kali-ina-yeye-aiachaye-njia/