WANA-NDOA: Baba Mkwe, Na mama Mkwe.

by Admin | 14 February 2022 08:46 pm02

Nakusalimu katika jina la Bwana Yesu, utukufu na ukuu vina yeye milele na milele amina.

Huu ni mwendelezo wa mafundisho ya wana-ndoa.

Ustawi  bora wa ndoa, hautegemei tu, mume au mke kutimiza wajibu wao wa mwilini,. Hiyo ni sehemu moja wapo, lakini pia ipo nyingine ambayo ni ya muhimu sana, na shetani pia anaifahamu, na kuipiga vita sana, na wewe kama mwanandoa, ukikosa jicho hilo la rohoni kulitambua, yapo mambo mengi sana mazuri utayakosa katika maisha yako ya ndoa.

Kama vile mafanikio ya mtoto  yanavyochangiwa na kuwaheshimu na kuwasikiliza wazazi wake. Vivyo hivyo mafanikio bora ya ndoa yanategemea sana, utii na heshima, na kuwasikiliza wakwe zako. Leo tutaona kibiblia ni kwa namna gani hili jambo lilivyo na nguvu nyingi sana katika ustawi mzuri wa ndoa.

MAMA-MKWE.

Ikiwa wewe ni binti uliyeolewa, fahamu kuwa baraka zako za kimaisha, hazipo tena kwa mama yako mzazi, bali zipo kwa mama-mkwe wako.

Vilevile ikiwa wewe ni kijana uliyeoa, fahamu pia, ubora na ustawi mzuri wa boma lako, hautegemei tena, wazazi wako, bali Baba-mkwe wako.

Ni ngumu kupokea, na ndio hapa, vita vinapokuwepo, lakini ndivyo Mungu alivyopenda iwe.

Ukisoma kitabu cha Ruthu kinaeleza kwa marefu, jinsi mama-mkwe alivyokuwa msingi wa Ruthu kufanikiwa na kupendwa na Mungu, kiasi kwamba hadi leo hii, tunakisoma kitabu hiki, ni kwasababu ya siri aliyoitambua kwa mkwe wake Naomi, utasoma, wakati Ruthu amefiwa na mume wake, hakutaka kuachana na mkwe wake, na kwenda kuolewa tena kwao, lakini alienda naye mpaka nchi ya ugenini, akakubali kuwa kama kijakazi wake, akakubali kuwa kama bibi mjane, japokuwa alikuwa kijana, lakini hakuachana naye hata kwa nukta moja, wakati mke-mwenza Orpa karudi kwao kuolewa, tena yeye hakumwacha mkwe wake Naomi kama tunavyosoma Habari, Lakini mwisho wa siku tunajua ni nini alikutana nacho Ruthu..Badala ya unyonge, ikiwa furaha. Hadi kupewa neema ya uzao wa Bwana Yesu kupitia kwake, angali hakuwa hata mwanamke wa kiyahudi bali wa kimataifa.

Kwa maelezo  marefu juu ya Habari hiyo  fungua link hii, >> https://wingulamashahidi.org/2020/02/19/ewe-mke-heshima-yako-ipo-kwa-wakwe-zako/

Au nitumie msg inbox nikutumie somo lake kwa urefu..

Hiyo ni kuonyesha kuwa mwanamke yeyote uliyeolewa, hatua kubwa za mafanikio yako, ipo kwa mkwe-wako. Shusha kiburi chako, jinyenyekeze, utamwona Bwana, hata kama ni mbaya bado, lipo zuri utalipata tu kwake ambalo ndio litakuwa chanzo cha kupanda juu kwako.

BABA-MKWE

Lakini leo nataka tuone pia baraka zilizo kwa Baba-Mkwe. Na hii hasaa inamuhusu mwanamume. Kamwe usimdharau baba wa mke wako, hata kama atakuwa ni mnyomge kiasi gani, lipo zuri moja tu atakuwa nalo, ambalo huwezi kulipata mahali pengine popote isipokuwa kwake, ambalo litakufaa sana.

Embu mtafakari Musa, alikuwa ni mtu aliyezungumza na Mungu uso kwa uso, akitaka jambo lolote kutoka kwa Mungu alikwenda moja kwa moja kuzungumza naye, Mungu alimpa Musa idadi kubwa ya watu, ili awachunge, lakini katika kuwachunga kule, kulikuwa hakuna utaratibu maalumu, watu walikuwa wanaenda tu, hivyo hivyo,kwa foleni kama vile hospitalini, na wakati wote huo, Mungu hakuwahi kuzungumza na Musa juu ya jambo hilo.

Sio kwamba alikuwa halioni, alikuwa analiona, lakini ni utaratibu wa Mungu, si kila jambo atakuagiza ufanye au atazungumza na wewe moja kwa moja, haijalishi wewe ni nani.. Hata wakati wote Mungu alipokuwa anazungumza na wana wa Israeli, hata siku moja hakuwahi kuwaambia mbona mnaniweka katika mahema yenye giza aliwaacha tu hivyo hivyo,.Lakini utaona miaka mingi sana baadaye Daudi aliligundua hilo, akasema nitamjengea Mungu nyumba. Na Mungu alipoona Daudi kawaza vile akapendezwa naye sana akambariki.(2Samweli 7)

Ndivyo ilivyokuwa kwa Musa, Kusanyiko lote, hakuweza kulimudu, hakuweza kulichunga ipasavyo, lakini Mungu alikuwa anazungumza naye kila siku, lakini  sio kwa Habari hizo. Ndipo siku moja Baba-mkwe wake (yaani baba wa mke wake), alipomtembelea kule jangwani, akaona jambo ambalo, Musa wala Israeli hawakuliona. Tusome;

Kutoka 18:14 “Mkwewe Musa alipoyaona yote aliyowafanyia watu, akasema, Ni jambo gani hili uwatendealo hao watu? Kwani wewe kuketi hapo peke yako, na watu wote kusimama kwako tangu asubuhi hata jioni?

15 Musa akamwambia mkwewe, Ni kwa sababu watu hunijilia mimi wapate kumwuliza Mungu;

16 wakiwa na neno, hunijilia; nami naamua kati ya mtu na mwenziwe, nami nawajuvisha amri za Mungu, na sheria zake.

17 Mkwewe Musa akamwambia, Jambo hili ufanyalo si jema.

18 Huna budi utadhoofika wewe, na hawa watu walio pamoja nawe pia; maana jambo hili ni zito mno kwako; huwezi wewe kulitenda peke yako.

19 Sikiza sasa neno langu, nitakupa shauri, na Mungu na awe pamoja nawe; uwe wewe kwa ajili ya watu mbele ya Mungu, nawe umletee Mungu maneno yao;

20 nawe utawafundisha zile amri na sheria, nawe utawaonyesha njia ambayo inawapasa kuiendea, na kazi ambayo inawapasa kuifanya.

21 Zaidi ya hayo utajipatia katika watu hawa watu walio na uwezo, wenye kumcha Mungu, watu wa kweli, wenye kuchukia mapato ya udhalimu; ukawaweka juu yao, wawe wakuu wa maelfu, na wakuu wa mia, na wakuu wa hamsini, na wakuu wa kumi;

22 nao wawaamue watu hawa sikuzote; kisha, kila neno lililo kubwa watakuletea wewe, lakini kila neno dogo wataliamua wenyewe; basi kwako wewe mwenyewe utapata nafasi zaidi, nao watauchukua huo mzigo pamoja nawe.

23 Kwamba utafanya jambo hili, na Mungu akikuagiza hivyo, basi utaweza kusimama wewe, na watu hawa wote nao watakwenda mahali pao kwa amani.

24 Basi Musa akasikiza neno la mkwewe, akayafanya yote aliyokuwa amemwambia.

25 Musa akawachagua watu wenye uwezo katika Israeli yote, akawaweka wawe vichwa juu ya watu, wakuu wa maelfu, na wakuu wa mia, na wakuu wa hamsini, na wakuu wa kumi.

26 Nao wakawaamua watu sikuzote; mashauri magumu wakamletea Musa, lakini kila neno dogo wakaliamua wenyewe.

27 Kisha Musa akaagana na mkwewe; naye akaenda zake, mpaka nchi yake mwenyewe”.

Umeona? Alichokifanya Musa, kilileta matokeo makubwa sana kwake na kwa wale aliowachunga. Hata sasa, wewe ni Baba, una familia ndogo au kubwa, usimdharau mkwe wako, kama yupo hai, kaa naye, msikilize kwa makini, hata kama atakuwa mjinga, usione shida kumwomba ushari wa kindoa, lipo moja litakusaidia kwa ustawi bora wa familia yako. Halikadhalika na mwanamke pia, shikamana na mama-mkwe wako.

Hizo ni kanuni za kiroho, zizingatie kwa afya ya maisha yako ya kindoa.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

KWANINI NDOA NYINGI ZINAVUNJIKA? (Sehemu ya 1: Upande wa wanaume)

MAFUNDISHO YA NDOA.

NDOA NI NINI?

NDOA NA HARUSI TAKATIFU.

MISTARI YA BIBLIA KUHUSU NDOA.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/02/14/wana-ndoa-baba-mkwe-na-mama-mkwe/