by Admin | 17 August 2022 08:46 am08
Ipo hekima ambayo Mungu anaitumia, pindi anapotaka kututoa katika hatua moja ya kimaisha kwenda nyingine.
Kiasili, nafsi zetu sisi wanadamu zinapenda kupokea majibu ya maombi pale tu tunapoomba… Lakini hekima ya Mungu wakati mwingine si kutupa kile tunachokiomba wakati ule ule tunapoomba… Wakati mwingine inaweza kuchukua muda mrefu kupokea majibu, na bado ikawa ni mapenzi ya Mungu.
Yapo mambo ambayo tukimwomba Mungu, ni rahisi kupokea majibu papo kwa hapo, lakini yapo ambayo yatachukua muda kujibiwa!..Sasa si kwasababu Mungu hawezi kujibu papo hapo! La!, anaweza kwasababu hakuna kinachomshinda yeye, lakini anapoyachelewesha wakati mwingine kwa faida yetu.
Hebu tengeneza picha, mtoto wa miaka 6 ambaye hajui hata kusoma, anamwomba Baba yake ambaye ni tajiri sana, ampe gari!.. Ni kweli Baba yake anao uwezo wa kumpa gari pale pale alipoomba, lakini hawezi kumpa kwasababu bado hajajua hata kusoma, atawezaje kuendesha hilo gari?..kwasababu aendapo akipewa gari katika akili hiyo aliyonayo, kitakachofuata ni Ajali!.. na mzazi atakuwa amemwua mtoto wake, badala ya kumpa uzima!..
Kwahivyo Ni sharti kwanza aende darasani akafundishwe kusoma na kuandika, na hesabu.. halafu akishajua hayo yote, ndipo aende kwenye shule ya udereva, akajifunze kanuni za uendeshaji magari, na baada ya kuhitimu na kupata leseni, ndipo baba yake ampe gari!..
Hivyo zoezi zima hilo la kusoma mpaka kupata leseni mpaka siku ya kukabidhiwa gari, linaweza kuchukua miaka hata 10. Kwahiyo ni sawa na kusema kwamba, mtoto kajibiwa ombi lake la kupewa gari baada ya miaka 10.
Lakini endapo mtoto Yule angeomba “peremende” kwa Baba yake, ni dhahiri kuwa “angepatiwa muda ule ule alioomba”.
Na kwa Mungu wetu ni hivyo hivyo, yapo mambo ambayo tukiomba tutajibiwa wakati huo huo, lakini yapo mambo mengine yatachukua muda mrefu sana, hata miaka kadhaa kujibiwa!!…
Hivyo kama umezoea kumwomba Mungu jambo na kupokea majibu yake saa hiyo hiyo, na ukamwomba jambo lingine ukaona hujajibiwa muda huo huo kama unavyotaka wewe!!.. Fahamu kuwa sio kwamba Mungu kakunyima hilo jambo, au kwamba hajasikia maombi yako!.. Amesikia maombi yako, na tayari majibu kashayaachia, lakini yatakuja kudhihirika siku nyingi za mbeleni endapo ukidumu katika kuishikilia ahadi hiyo.
Hebu tujifunze mfano mmoja juu ya wana wa Israeli, kipindi wanatoka Misri..
Tunasoma katika maandiko kuwa, kipindi wanaingia Kaanani, Mungu hakuwatoa wakaanani katika ile nchi ndani ya siku moja, au ndani ya mwaka mmoja, biblia inasema ilichukua miaka kadhaa, Mungu kuwaondoa Wakaanani na wengineo waliokuwa wanaikalia ile nchi ya Ahadi.
Sasa ni kwasababu gani Mungu hakuwaondoa Wakaanani wote na wahivi wote ndani ya siku moja??..Jibu: Si kwasababu hakuwa na uwezo huo, alikuwa nao tele, lakini kwafaida ya watoto wake Israeli, ilikuwa hana budi kuwapa urithi huo kidogo kidogo!…kwasababu angewapa siku ile ile, basi yangezuka matatizo mengine, ambayo tunayasoma katika mistari ifuatayo…
Tusome,
Kutoka 23: 27 “Nitatuma utisho wangu utangulie mbele yako, nami nitawafadhaisha watu wote utakaowafikilia, nami nitawafanya hao adui zako wote wakuonyeshe maungo yao.
28 Nami nitapeleka mavu mbele yako, watakaomfukuza Mhivi, na Mkanaani, na Mhiti, watoke mbele yako.
29 SITAWAFUKUZA MBELE YAKO KATIKA MWAKA MMOJA; NCHI ISIWE UKIWA, NA WANYAMA WA BARA WAKAONGEZEKA KUKUSUMBUA.
30 NITAWAFUKUZA KIDOGO KIDOGO MBELE YAKO, HATA UTAKAPOONGEZEKA WEWE, NA KUIRITHI HIYO NCHI”
Umeona hapo?..Sababu ya wao kutopewa Nchi yote ndani ya siku moja, ni lli wanyama wasiongezeke juu ya nchi, na kuwaletea madhara.. Kwasababu kipindi wanatoka Misri, walikuwa wachache.. halafu wanakwenda kupewa nchi kubwa!.. ni lazima sehemu kubwa ya nchi hiyo itakuwa MAPORI!.. Kwasababu hakuna watu wa kuijenga wala kukaa juu yake..na hivyo Nyoka wataongezeka, chatu na fisi wataongezeka, watakaokula mifugo yao..hali kadhalika samba na mbu!, watakuwa wengi kwasababu ya wingi wa mapori, na hivyo itanyanyuka shida nyingine..
Kwahiyo hekima ya Mungu, ikaamua maadui wa Israeli wasifukuzwe wote, bali waachwe kwanza kwa kitambo kifupi, waendelee kufyeka mapori, mpaka idadi ya Israeli itakapoongezeka, kufikia kiwango cha kuweza kuitawala nchi nzima, ndipo maadui wote waondolewe!.
Na sisi ni nini tunajifunza hapo?…tunajifunza kuwa wavumilivu, na kuwa na Subira katika ahadi za Mungu na kwamba si kila ombi litajibiwa siku tunayoitaka sisi.
Ikiwa wewe ni binti au kijana, na umemwomba Mungu akupe mwenza wa maisha, na unaona hujibiwi kwa wakati unaotaka wewe, huenda ni kwasababu wakati wake haujafika! Aidha Umri wako ni mdogo, au pengine akili yako bado haijakuwa vya kutosha, bado haijafundishwa vya kutosha maisha ya ndoa,.. Na ili Mungu asikupoteze ndio maana hakupi unachotaka kwa wakati huo huo.
Vile vile Ukimwomba Mungu mali na huku akili yako inawaza kwenda kujionyesha mbele za watu, fahamu kuwa Mungu ameshasikia maombi yako, lakini hutapokea saa hiyo hiyo, ulipopmba…badala yake utakwenda kwanza kwenye madarasa yake ambayo atakufundisha maisha ukiwa na mali, (huenda yakachukua hata miaka 20), inategemea na akili yako, na ukifaulu madarasa yake! basi atakupatia!..kwasababu utakuwa umeshajengeka vya kutosha, kiasi kwamba mali haziwezi kukuangusha wala kukurudisha nyuma kiroho, wala kuwaharibu wengine.
Na maombi mengine yote ni hivyo hivyo..yanayo hatua mpaka tuone matokeo, hivyo tuwe wavumilivu na watu wa subira..
Bwana Yesu atubariki.
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
HEKIMA NI NINI? NA UFAHAMU UNAPATIKANA WAPI?
Tofauti kati ya lijamu na hatamu ni ipi kibiblia?
Kigao ni nini? Na Je kinafunua nini kwa agano jipya?
Tofauti kati ya Hekima, ufahamu na maarifa, ni ipi?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/08/17/ijue-hekima-ya-mungu-katika-kukuinua-kimaisha/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.