YEYE ATAWABATIZA KWA ROHO MTAKATIFU NA KWA MOTO.

by Admin | 13 January 2023 08:46 am01

Maandiko yanasema kuwa Bwana Yesu hakuwahi kumbatiza mtu yeyote kwa maji katika huduma yake yote…

Yohana 4:1 “Kwa hiyo Bwana, alipofahamu ya kuwa Mafarisayo wamesikia ya kwamba, Yesu anafanya wanafunzi wengi kuliko Yohana, na kuwabatiza,

(lakini Yesu mwenyewe hakubatiza, bali wanafunzi wake)

Umeona?.. kila mahali Bwana Yesu alipofika aliwaachia wanafunzi wake wabatize!.. lakini yeye mwenyewe hakubatiza mtu yeyote kwa maji. Sasa hiyo haimaanishi kuwa ubatizo wa maji hauna maana!. (mbele kidogo tutaelewa zaidi umuhimu wake).

Sasa kufuatia mwenendo huo wa Bwana Yesu kutombatiza mtu yeyote, ni kuonyesha kuwa anao ubatizo mwingine ambao atawabatiza nao watu, ambao hakuna mwanadamu yeyote anayeweza kuufanya!… Ubatizo wa maji mwanadamu anaweza kuufanya kwa mwanadamu mwenzake, Lakini ubatizo huo ambao Bwana Yesu atakwenda kuwabatiza nao watu hakuna anayeweza kuufanya zaidi yake yeye mwenyewe.. Na ubatizo huo si mwingine zaidi ya ule wa Roho Mtakatifu.

Tunapobatizwa kwa Maji, miili yetu inazama kwenye maji mengi na kuibuka juu, kama ishara ya kufa na kufufuka na Kristo.. Lakini tunapobatizwa kwa Roho Mtakatifu ni kitendo cha Bwana Yesu kuzichukua roho zetu na kuzizamisha katika Roho Mtakatifu, Ni tendo kuu sana ambalo hakuna mwanadamu yeyote wala malaika yeyote anayeweza kulifanya.. kama maandiko yanavyosema katika Yohana 3:16.

Luka 3:16 “Yohana alijibu akawaambia wote, Kweli mimi nawabatiza kwa maji; lakini yuaja mtu mwenye nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya viatu vyake; YEYE ATAWABATIZA KWA ROHO MTAKATIFU NA KWA MOTO”

Hiyo ikimaanisha kuwa kama vile ubatizo wa maji ulivyo wa muhimu vile vile na ubatizo wa Roho Mtakatifu ni wa muhimu sana..Ni lazima tubatizwe na watu katika Maji na vile vile tubatizwe na Bwana Yesu katika Roho Mtakatifu.

Wapo watu wanaosema kuwa ubatizo wa Roho Mtakatifu sio wa muhimu, bali ule wa maji tu unatosha, na wapo wanaosema ubatizo wa Roho Mtakatifu ndio wa muhimu, hivyo mtu akishaupata ubatizo wa Roho Mtakatifu hakuna haja tena ya ubatizo wa maji. Nataka nikuambie kuwa hiyo imani ni imani potofu ambayo imetengenezwa na ufalme wa giza kuwaua watu kiroho, maandiko yanasema “…Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu (Yohana 3:5) ”

Kuzaliwa kwa maji ni ubatizo wa Maji, na kuzaliwa kwa Roho ni ubatizo wa Roho Mtakatifu (Haihitaji elimu kubwa kuelewa hili, ni tafakari nyepesi kabisa).

Na zaidi ya yote tunazidi kuthibitisha kuwa ubatizo wa maji ni wa muhimu hata baada ya kuupokea ule wa Roho Mtakatifu, wakati ule Petro alipofika nyumbani kwa Kornelio, maandiko yanasema baada ya wale watu wa nyumbani kwa Kornelio kushukiwa na Roho Mtakatifu, bado Mtume Petro aliwaagiza wakabatizwe katika maji na kwa jina la Yesu Kristo.

Matendo 10:44  “Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno.

45  Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu.

46  Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu,

47  Ni nani awezaye kuzuia maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vile vile kama sisi?

48  Akaamuru wabatizwe kwa Jina lake Yesu Kristo. Ndipo wakamsihi azidi kukaa siku kadha wa kadha”

Umeona?, hao watu walitangulia kubatizwa na Bwana Yesu mwenyewe kwa  ubatizo wa Roho mtakatifu, lakini bado walikwenda kubatizwa tena na akina Petro kwa ubatizo wa Maji. Kwasababu Petro alijua kuwa hawa wasipozaliwa kwa Maji na kuwaacha tu wawe wamepokea ubatizo wa Roho hawataweza kuuona ufalme wa Mungu, sawasawa na maneno ya Bwana.

Je! na wewe umebatizwa kwa Maji?.. Kama bado na umeshasikia ukweli namna hii, upo hatarini sana…Na kumbuka kama ulibatizwa uchangani, basi huna budi kubatizwa upya kwa sababu hukuwa umejitambua wakati huo, zaidi sana kama pia ulibatizwa kwa maji machache, ni lazima ubatizwe upya kwa maji mengi (Yohana 3:23)

Na je! umeshabatizwa pia kwa Roho Mtakatifu?.. kama Bado msihi Bwana naye ni mwaminifu atakupa Roho wake mtakatifu, kwasababu yeye anatamani uwe naye kuliko wewe unavyotamani.. lakini ni sharti kwanza utubu kwa kumaanisha kuacha dhambi zako zote na kubatizwa kwa maji kama tayari umeshausikia ukweli, kwa kukamilisha mambo hayo, maandiko yanasema Yule Roho ni kwaajili yetu, na kwa vizazi vyetu, Bwana Yesu anatubaziwa kwa huyo bureeeeeeeeee..

Matendo 2:37  “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?

38  Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

39  Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

TOFAUTI YA UBATIZO WA YOHANA NA UBATIZO WA BWANA YESU

JE! UMEBATIZWA UBATIZO SAHIHI?

NUNUA MAJI YA UZIMA.

MFANO WA MAMBO HAYO NI UBATIZO.

UBATIZO NI NINI NA ULIO SAHIHI NI UPI?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/01/13/yeye-atawabatiza-kwa-roho-mtakatifu-na-kwa-moto/