Ni kwa namna gani haki huinua taifa? (Mithali 14:34)

by Admin | 22 July 2023 08:46 am07

Swali: Maandiko yanasema “Haki huinua Taifa”.. Je hii imekaaje kiundani zaidi?

Jibu: Tusome,

Mithali 14:34 “HAKI HUINUA TAIFA; Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote”.

Kwa tafsiri ya kawaida mtu mwenye haki ni yoyote yule anayefanya matendo ya haki bila kujali kile anachokiamini, lakini kibiblia ni tofauti kidogo…Kibiblia  mtu “mwenye haki” ni yule anayemcha Mungu na “asiye haki” ni yule asiyemcha Mungu.

Kwahiyo hata kama mtu atajitahidi kufanya matendo mazuri na yenye kukubalika katika jamii yake yote, lakini kama moyoni mwake hamwamini Mungu, huyo kibiblia ni mtu asiye haki hata kama ana sifa njema.

Kwahiyo wanapoongezeka watu wanaomcha Mungu wengi katika Taifa maana yake “Haki na yenyewe inazidi kuongezeka”. Na matokeo ya kuwepo Wenye haki wengi juu ya nchi kuliko wasio haki ni kunyanyuka kwa Taifa, na kinyume chake wanapokuwepo wasio haki wengi katika nchi kuliko wenye haki basi Taifa linakuwa hatiani kuanguka. Sasa utauliza ni kwa namna gani?.. Hebu tujikumbushe kidogo ile habari ya Ibrahimu na Elohimu wakati ule wa Maangamizi ya Sodoma na Gomora

Mwanzo 18:22 “Basi wale watu wakatoka huko wakaelekea Sodoma; lakini Ibrahimu alikuwa akali akisimama mbele za Bwana.

23 Ibrahimu akakaribia, akasema, JE! UTAHARIBU MWENYE HAKI PAMOJA NA MWOVU? 

24 Huenda wakawapo wenye haki hamsini katika mji, utaharibu, WALA HUTAUACHA MJI KWA AJILI YA HAO HAMSINI WENYE HAKI WALIOMO? 

25 Hasha usifanye hivyo, ukamwue mwenye haki pamoja na mwovu, mwenye haki awe kama mwovu. Hasha; Mhukumu ulimwengu wote asitende haki? 

26 BWANA AKASEMA, NIKIONA KATIKA SODOMA WENYE HAKI HAMSINI MJINI, NITAPAACHA MAHALI POTE KWA AJILI YAO. 

27 Ibrahimu akajibu, akasema, Basi, nimeshika kusema na Bwana, nami ni mavumbi na majivu tu.

28 Huenda wakapunguka watano katika wale hamsini wenye haki, je! Utaharibu mji wote kwa kupungua watano? Akasema, Sitauharibu, nikiona humo arobaini na watano. 

29 Akazidi tena kusema naye, akinena, Huenda wakaonekana humo arobaini? Akasema, Sitafanya kwa ajili ya hao arobaini. 

30 Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema, Huenda wakaonekana huko thelathini? Akasema, Sitafanya, nikiona humo thelathini. 

31 Akasema, Tazama, nimeshika kusema na Bwana, huenda wakaonekana huko ishirini? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao ishirini. 

32 Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema mara hii tu, Huenda wakaonekana huko kumi? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi.

 33 Basi Bwana alipokwisha kuzungumza na Ibrahimu, akaenda zake; Ibrahimu naye akarudi mahali pake”.

Umeona? Kumbe Miji ya Sodoma na Gomora iliteketea kwasababu ya kukosekana wenye haki ndani yake, kumbe wangeonekana tu wenye haki 10, basi miji ile yote ingepona!…lakini walipokosekana ndipo miji ile ikaanguka na kuangamia.

Ikiwa na maana kuwa Amani ya Miji na Mataifa ni kwasababu ya wenye haki ndani yake, ni kwasababu ya watu wa Mungu kuwepo ndani yake, hao wakiondolewa Taifa au mji unaanguka na kuangamia.

Ndio maana maandiko yanazidi kutufundisha kuwa dhiki kuu haitaanza mpaka Kanisa (wenye haki) watakapoondolewa, ikimaanisha kuwa uwepo wa watu wa Mungu katika dunia ndio unaozuia mambo kuharibika.. lakini hao watakapoondolewa ndipo Mataifa yataanguka, na ulimwengu mzima kwa ujumla.

2Wathesalonike 2:6  “Na sasa lizuialo mwalijua, yule apate kufunuliwa wakati wake.

7  Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi; LAKINI YUKO AZUIAYE SASA, HATA ATAKAPOONDOLEWA.

8  Hapo ndipo atakapofunuliwa yule asi, ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa ufunuo wa kuwapo kwake”

Je na wewe ni miongoni mwa wenye haki?

Kumbuka katika zama hizi tunahesabiwa haki mbele za Mungu kwa njia ya kumwamini Yesu Kristo… Na si kwa matendo yetu yasiyo na Imani yoyote…

Wagalatia 2:16 “hali tukijua ya kuwa mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria, bali kwa imani ya Kristo Yesu; sisi tulimwamini Kristo Yesu ili tuhesabiwe haki kwa imani ya Kristo, wala si kwa matendo ya sheria; maana kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki”.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/07/22/ni-kwa-namna-gani-haki-huinua-taifa-mithali-1434/