IJUE FAIDA YA KUFUNGA PAMOJA NA WANYAMA WAKO.

by Admin | 24 September 2023 08:46 pm09

(Masomo maalumu yahusuyo mifungo na maombi).

Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze Biblia Neno la Mungu wetu lililo taa ya miguu yetu na Mwanga wa njia yetu (Zab 119:105).

Biblia inatufundisha sehemu kadhaa FAIDA za kufunga (yaani kujizuia kula na kunywa kwa kitambo) kwamba kwa kufanya hivyo tunafungua milango mingi, ambayo isingeweza kufunguka kwa maombi ya kawaida tu.

Mathayo 17:20  “Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu.

21  [LAKINI NAMNA HII HAITOKI ILA KWA KUSALI NA KUFUNGA”.

Lakini JE UNAJUA FAIDA ZA KUIFUNGISHA NA MIFUGO YAKO PIA? AU KAZI YAKO, AU BIASHARA YAKO?. Si watu tu wanaopaswa kufunga hata wanyama pia.. Utauliza hilo limekaaje?, hebu turejee biblia kidogo nyakati zile za Nabii Yona alipokwenda kuhubiri katika mji wa Ninawi.

Biblia inaonyesha kuwa Mfalme wa Ninawi alipiga mbiu kuwa wanadamu na wanyama wote walioko Ninawi wafunge wasile wala wasinywe (Zingatia hilo: si wanadamu tu bali hata wanyama wa kufungwa).

Yona 3:6 “Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu. 

7 Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu ASIONJE KITU, WALA MNYAMA WALA MAKUNDI YA NG’OMBE, WALA MAKUNDI YA KONDOO; WASILE, WALA WASINYWE MAJI;

 8 bali na wafunikwe nguo za magunia, MWANADAMU NA MNYAMA PIA, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake. 

9 Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe?  10 Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende”.

Unaona alichofanya Mfalme wa Ninawi??…Na matokeo yake tunaona baadaye Mungu anawataja wanyama kuwa wamestahili rehema kwa mfungo huo..Maana yake wanyama nao pia wasingefungishwa huenda wangepona watu tu  lakini wanyama wangepigwa (wangekufa!!)..Maana yake uchumi wao watu wa Ninawi ungeharibika, hata baada ya wao kupokea msamaha!!.

Yona 4:10 “Bwana akamwambia, Wewe umeuhurumia mtango, ambao hukuufanyia kazi, wala kuuotesha; uliomea katika usiku mmoja, na kuangamia katika usiku mmoja;

 11 na mimi, je! Haikunipasa kuuhurumia Ninawi, mji ule mkubwa; ambao ndani yake wamo watu zaidi YA MIA NA ISHIRINI ELFU, wasioweza kupambanua katika mkono wao wa kulia na mkono wao wa kushoto; TENA WAMO WANYAMA WA KUFUGWA WENGI SANA?

Nataka uangalie hayo maneno ya mwisho ya Bwana… “TENA WAMO WANYAMA WA KUFUGWA WENGI SANA?”

Kumbe hata wanyama pia wanaweza kuingizwa kwenye mkondo wetu wa BARAKA AU LAANA!.. Mfalme wa Ninawi aliliona hili, alijua siku ile ya gharika ya Nuhu hata wanyama waliangamizwa na dunia, na yeye akajua dhambi zimewachafua si tu watu, bali hata na wanyama wao wa kufugwa, hivyo nao pia ni lazima watakaswe kwa toba na  kwa kufunga, na utaona aliwavisha mpaka hao wanyama mavazi ya magunia!.

Ni vizuri kulijua hili ndugu, kuwa unapofunga fanya hivyo pia kwa wanyama wako (inaweza isiwe mara kwa mara lakini weka desturi hiyo)!!!

Unapofunga hebu pia funga pia na shamba lako, usinyeshee chochote siku hiyo, usiweke mboleo siku hiyo, wala usilipalilie, kama unafuga kuku, usiwalishe siku hiyo, usilishe ng’ombe wako siku hiyo, usilishe mbuzi wako siku hiyo, vile vile usifungue biashara yako siku hiyo, fanya hivyo kwa Imani  na utaona matokeo makubwa sana baada ya hapo!.

Wengi hawaoni matokeo katika kazi zao kwasababu wanasahau kufunga biashara zao, badala yake wanafunga tu wao, pasipo kujua kuwa vifungo pia havipo tu katika mwili, bali pia katika biashara na mifugo, hivyo nayo pia inapaswa ifungishwe.

Bwana akubariki.

Maran atha

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

NJIA SAHIHI YA KUFUNGA.

HIZI NI NYAKATI ZA KUFUNGA NA KUOMBA.

NINI MAANA YA KUTUBU

Je tunaruhusiwa kutumia vidonge wakati wa kufunga?

Ninawi ni nchi gani kwasasa?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/09/24/ijue-faida-ya-kufunga-pamoja-na-wanyama-wako-na-kazi-zako/