MADHIHIRISHO MATATU YA MUNGU.

by Admin | 13 February 2024 08:46 am02

Mungu amejifunua katika Ofisi kuu 3, (Baba, Mwana na Roho Mtakatifu).

Lakini katika dhihirisho zote hizi tatu (3) Mungu anabaki kuwa mmoja na si watatu.

Sasa swali ni je kama ni mmoja kwanini ajifunua hivyo katika utatu?

Jibu rahisi ni kwamba, Mungu kajidhihirisha hivyo kwa lengo la kumkamilisha Mwanadamu na si kujitambulisha yeye. Na kwanini mwanadamu akamilishwe kupitia dhihirisho hizo tatu?..Ni kwasababu alikuwa amepotea na kujitenga mbali naye kwasababu ya dhambi.

(Dhambi zinatutenganisha sisi na Mungu) Kama maandiko yanavyosema…katika Isaya 59:2.

Mwanzo katika Edeni Mungu alikuwa karibu sana na MTU, aliweza kumwona, kumsikia, na hata kuzungumza naye (Mwanzo 3:8). Lakini baada ya dhambi kuingia ule ukaribu na Mungu ukapotea, Adamua akawa hawezi kumwona tena Mungu wala kumsikia kama alivyokuwa anamsikia mwanzo…Ile dhambi ikamtenga mbali na Mungu. (Isaya 59:2).

Na Mungu kwa upendo wake kwetu, akaanza mpango wa kuturejesha karibu naye tena. Tumwone tena, tuseme naye, tutembee naye na tumhisi ndani yetu kama mwanzo. Lakini matengenezo hayo si ya mara moja kama maharibifu. (kuharibu mahusiano ni mara moja, lakini kujenga inagharimu muda mrefu).

Na neno la ahadi ni kwamba siku moja MASKANI ya MUNGU itakuwa pamoja na wanadamu kuliko hata ilivyokuwa EDENI.

Ufunuo 21:3 “Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, NAYE ATAFANYA MASKANI YAKE PAMOJA NAO, NAO WATAKUWA WATU WAKE. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao”.

Sasa mahusiano hayo yaliyoharibika Mungu alianza kuyatengeneza hatua kwa hatua..na sasa tupo katika hatua ya mwisho wa matengenezo hayo.. Hebu tuzitazame hizo hatua moja baada ya nyingine.

     1.MUNGU JUU YETU. (Kama Baba)

Hii ni hatua ambayo Mungu alianza kuongea na watu kwa njia ya Maono na Ndoto, lakini akawa haonekani. Na alisema na watu wachache tu walioitwa manabii. Huu ni wakati ambao MUNGU alijidhihirisha kama NENO tu!.. (Maana yake MANENO YAKE ndiyo yaliyokuwa yanafahamika tu lakini yeye mwenyewe haonekani kwa macho).

Yohana 1:1 “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu”.

     2. MUNGU PAMOJA NASI (Kama Mwana).

Huu ni wakati ambao Mungu aliuvaa mwili, ili yale MANENO aliyokuwa anasema na watu kwa njia ya maono na ndoto basi ayaseme kwa mdomo wa damu na Nyama na kuyafafanua na kuyafundisha ili watu wamwone na kumwelewa.. Na mwili ambao aliuvaa ndio ukaitwa YESU.

Yohana 1:14  “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli”.

Umeona?..Mungu anaanza kumsogelea tena mwanadamu kwa karibu.. Kwahiyo YESU ni Mungu aliyeuvaa mwili kwa lengo hilo la kuyasema yale maneno ya Mungu yaliyokuwa yanayosikika kwa ndoto na maono kupitia manabii..

Kuzidi kuuthibitisha uungu wa YESU basi soma mistari ifuatayo (Yohana 20:28, 1Yohana 1:1-2, Tito 2:13, Isaya 9:6 na 1Timotheo 3:16).

Lakini isingetosha tu Mungu aonekane katika mwili na kuyahubiri maneno yake kwa mdomo kama alivyokuwa anaongea na Adamu pale Edeni na huku bado mwanadamu hajui kanuni ya kuishi katika mapenzi ya Mungu…Hivyo akaongeza mpango wa pili juu yake wa kumfundisha mwanadamu njia na kanuni za kuishi kimatendo, kwahiyo ikambidi aishi kama mwanadamu ambaye anamcha Mungu.

Lengo si kutafuta ukamilifu yeye, bali ni kutufundisha sisi ukamilifu, ndio maana akaishi chini ya wazazi ili awafundishe watoto namna ya kuishi maisha ya kumcha Mungu, na tena akawa mtu mzima ili awafundishe watu wazima kanuni za kumcha Mungu, ndio maana akawa anaomba, akawa anafunga, akawa anamwambudu Mungu kana kwamba kuna Mungu juu n.k.

Hivyo maisha yake yakawa njia ili sisi tufahamu njia (soma Yohana 14:6). Lakini yeye hakuwa mtu, bali ni Mungu ndani ya mwili wa Mtu kwa lengo la kutufundisha njia..

Wafilipi 2:5 “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu;

6 ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho;

7  bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu”

Lakini pia isingetosha yeye ahubiri maneno yale kwa kinywa chake, na awe mwalimu wa kutufundisha sisi na ili hali bado tuna laana ya dhambi tuliyoirithi toka kwa wazazi wetu wa kwanza Adamu na Hawa

Hivyo akaongeza mpango mwingine wa tatu (2) juu ya hiyo miwili, kwamba autoe mwili wake huo kuwa sadaka ya dhambi baada ya kumaliza huduma kazi hizo mbili.. Hiyo ndio sababu kwanini Kristo afe msalabani..Ni ili sisi tupate ondoleo la dhambi.

   3. MUNGU NDANI YETU (Kama Roho Mtakatifu).

Baada ya kurejesha uhusiano namna hiyo, kwamba sasa tunamwona MUNGU na tumeondolewa dhambi na kile kizuizi kulichokuwa kinatutenga sisi na Mungu, na ile laana ya Adamu tuliyokuwa tunaibeba. Mungu aliongeza mpango mwingine wa Mwisho ambao kupitia huo tutakuwa karibu na Mungu moja kwa moja, kwamba tutamsikia na kumwona na kumwelewa sana.

Na mpango huo si mwingine Zaidi ya yeye kuingia ndani yetu, kama ROHO, ili atusaidie madhaifu yetu..Ni sawa na mchezaji aliye katika michezo anayepewa kinywaji cha kuongeza nguvu na kusisimua misuli ili ashinde katika mchezo ule.

Na Roho Mtakatifu ni MUNGU katika ROHO, ambaye anaingia ndani yetu na KUSISIMUA uwezo wetu wa kumwelewa MUNGU, UWEZO wetu wa KUSHINDA DHAMBI, uwezo wetu wa KUMCHA MUNGU, Uwezo wetu wa kukumbuka n.k (Yohana 14:26 na Yohana 16:12-13).

Sasa kuthibitisha kuwa Roho Matakatifu ndiye yule yule Mungu soma 2Wakorintho 3:17.

Hii ni zawadi kubwa na kipekee sana, na ya mwisho inayomsogeza Mtu karibu na Mungu kuliko zote.

Sasa swali la ziada ni hili; Kwanini KRISTO aondoke!

Sababu ya KRISTO kuondoka na kwenda juu mbinguni ni kwenda kutuandalia sisi makao (Yaani ile YERUSALEMU MPYA), Makao ya watakatifu. (soma Yohana 14:2, Ufunuo 3:12 na Ufunuo 21:2).

Na makao hayo anayokwenda kutuandalia ni ili wakati utakapofika tukae naye milele, katika mbingu mpya na nchi mpya. (Maskani yake iwe pamoja nasi)…Hapo yale yaliyoharibika Edeni yatakuwa yametengenezwa upya tena katika utukufu Mkuu kuliko ule wa kwanza.

Ufunuo 21:3  “Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.

4  Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.

5  Na yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi akasema, Tazama, nayafanya yote kuwa mapya. Akaniambia, Andika ya kwamba maneno hayo ni amini na kweli”.

Je umeuona mpango wa Mungu??…na je umeyaona pia madhara ya dhambi??… Dhambi ilitutenga mbali na Mungu na mpaka sasa inatutenga mbali na Mungu..

Na kanuni pekee ya kumkaribia MUNGU ni kwa kutubu dhambi kwa kumaanisha kuziacha (Mithali 28:13). Unapotubu kwa kumaanisha kuziacha unamkaribisha YESU maishani mwako ambaye humwoni kwa macho sasa, lakini siku moja utamwona… Lakini zawadi kubwa atakayokupa ambayo itakufanya ujihisi upo naye hata kama humwoni ni ROHO MTAKATIFU (ambaye kiuhalisia ni yeye mwenyewe katika mfumo wa Roho).

Na huyo Roho Mtakatifu atakulinda na ulimwengu, mpaka siku ya mwisho, ambayo BWANA YESU ATAKUJA na kutupa TAJI ZA UZIMA, na kukaa naye milele katika maisha ya furaha, yasiyo na mwisho, wala dhiki wala mateso, wala uchungu, wala vilio..kwasababu mambo ya kwanza yatakuwa yameshapita.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

KWANINI YESU KRISTO NI MWANA WA DAUDI?

KWANINI KUWE NA UTAWALA WA MIAKA 1000

Kwa namna gani tumefanyika Makuhani na Ufalme?.(Ufunuo 1:6)

REKEBISHA YAFUATAYO ILI UCHUMI WAKO UKAE SAWA.

KAMA SI YESU, HABARI YETU INGEKUWA IMEISHA ZAMANI SANA.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/02/13/madhihirisho-matatu-ya-mungu/