Kusujudu ni nini, na je tuna sharti la kusujudu kwa Mungu?

by Admin | 1 October 2024 08:46 am10

Swali: Je kusujudu ni nini, na sisi wakristo tunayo amri ya kusujudu mbele za Mungu?


Kusujudu ni kitendo cha kuinama kwa kuelekeza kichwa chini kama ishara ya kuabudu au kutoa heshima kwa Mungu, mtu au shetani.. Zaidi ya kuinama tu, kusujudu pia kunaweza kuhusisha kupiga magoti na kuinamisha kichwa chini mpaka kufikia kugusa ardhi (soma 2Nyakati 7:3).

Maandiko yanatuonyesha mara kadha wa kadhaa watu wakimsujudia Mungu, na watu wakiwasujudia wanadamu na vile vile wakimsujudia shetani.

     1.Watu kumsujudia Mungu

Mfano wa watu waliosujudu mbele za Mungu ni yule Mtumwa, Ibrahimu aliyemtuma kwenda kumtafutia mwanae Isaka, mke.. Maandiko yanasema alipokutana tu na Rebeka na kupata uhakika kuwa ndiye binti aliyechaguliwa na Bwana, basi yule mtumwa alisujudu mbele za Bwana mpaka chini..

Mwanzo 4:24 “Akasema, Mimi ni binti wa Bethueli mwana wa Milka, aliyemzalia Nahori.

25 Tena akamwambia, Kwetu kuna majani na malisho ya kutosha, na mahali pa kukaa wageni.

26 YULE MTU AKAINAMA AKAMSUJUDU BWANA. 

27 Akasema, Na atukuzwe Bwana, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, ambaye hakuacha rehema zake na kweli yake kwa bwana wangu. Bwana akaniongoza mimi nami njiani hata nyumba ya nduguze bwana wangu”.

Wengine waliosujudu mbele za Bwana katika biblia ni Musa (soma Kutoka 34:8-9) na Wana wa Israeli kipindi utukufu umeshuka juu ya Nyumba ya Mungu (2Nyakati 7:3)…pamoja na mwandishi Ezra na wenzake katika Nehemia 8:6.

    2. Watu kusujudia Malaika.

Mfano wa watu waliowasujudia Malaika ni Yohana, Mtume wa Bwana YESU.

Ufunuo 22:8  “Nami Yohana ndimi niliyeyasikia na kuyaona mambo hayo. Na hapo nilipoyasikia na kuyaona nalianguka, ili NISUJUDU mbele ya miguu ya malaika yule mwenye kunionyesha hayo.

9  Naye akaniambia, Angalia, usifanye hivi; mimi ni mjoli wako, na wa ndugu zako manabii, na wa wale wayashikao maneno ya kitabu hiki. MSUJUDIE MUNGU”.

Mwingine aliyejaribu kumsujudia Malaika ni Yoshua (soma Yoshua 5:14)

    3. Watu kuwasujudia wanadamu.

Mfano wa watu waliomsujudia mwanadamu katika biblia ni wale wana 11 wa Yakobo, ambao walisujudu mbele ya ndugu ya Yusufu, walipofika nchi ya Misri.

Mwanzo 43:27 “Akawaulizia hali yao, akasema, Je! Baba yenu, yule mzee mliyemnena, hajambo? Angali hai?

28 Wakasema, Mtumwa wako baba yetu hajambo, angali hai; WAKAINAMA, WAKASUJUDU”.

Mwingine aliyemsujudia mwanadamu ni Jemedari Yoabu (2Samweli 14:22), mwengine tena ni Arauna (2Samweli 24:20) na yule mwanamke wa Tekoa (2Samweli 14:4).., Hamani aliyesujudiwa na watu (Esta 3:2)

     4. Watu kumsujudia shetani na jeshi lake.

Mfano wa watu waliomsujudia shetani na majeshi yake ni Wana wa Israeli, kipindi wanakatiza Moabu, ambapo waliisujudia miungu ya Moabu, na kufanya dhambi kubwa mbele za Mungu..

Hesabu 25: 1 “Basi Israeli akakaa Shitimu, kisha watu wakaanza kuzini pamoja na wanawake wa Moabu;

2 kwa kuwa waliwaalika hao watu waende sadakani, sadaka walizowachinjia miungu yao; watu wakala chakula, WAKAISUJUDU HIYO MIUNGU YAO. 

3 Ikawa Israeli kujiungamanisha na Baal-peori; hasira za Bwana zikawaka juu ya Israeli”.

Mwingine aliyesujudia mashetani ni Mfalme Yeroboamu (1Wafalme 16:31)

Swali ni je! Watu waliozaliwa mara ya pili (wa agano jipya) ni sahihi KUSUJUDU??

Jibu ni NDIO!.. Lakini anayepaswa na kustahili kusujudiwa ni MUNGU PEKE YAKE!… Wengine waliosalia ambao ni wanadamu au malaika hatupaswi kuwasujudia hata kidogo.. Maandiko kwa kupitia kinywa cha Bwana wetu YESU KRISTO yanatufundisha hilo moja kwa moja..

Mathayo 4:8 “Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake,

9  akamwambia, Haya yote nitakupa, UKIANGUKA KUNISUJUDIA.

10  Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, MSUJUDIE BWANA MUNGU WAKO, UMWABUDU YEYE PEKE YAKE.

11  Kisha Ibilisi akamwacha; na tazama, wakaja malaika wakamtumikia”

Hivyo anayestahili KUSUJUDIWA ni Mungu peke yake sawasawa na maandiko hayo..

Lakini pia kusujudu na kuabudu ni lazima kufanyike katika roho na kweli ndivyo biblia inavyotufundisha, Kusujudu (kwa kuanguka chini) kunafaa sana kwa maombi ya Rehema na Toba, vile vile kwafaa sana kwa maombi ya maombi ya kupeleka mahitaji, kwani ni ishara ya unyenyekevu na kujishusha mbele za Mungu.

Na kusujudu si kanuni ya maombi, kwamba kila maombi ni lazima yaambatane na kusujudu, na kwamba usiposujudu basi maombi yako hayatasikiwa wala kukubalika,… bali ni tendo linaloambatana na msukumo wa kiungu na mzigo wa Roho Mtakatifu ndani.

Bwana atusaidie.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

FAIDA ZA MAOMBI.

UNAMFAHAMU MUNGU WA KWELI?

KWANINI MUNGU HAJIBU MAOMBI?

HUDUMA YA MALAIKA WATAKATIFU.

KUNA AINA NGAPI  ZA MAOMBI?

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/10/01/kusujudu-ni-nini-na-je-tuna-sharti-la-kusujudu-kwa-mungu/