KWANINI MUNGU HAJIBU MAOMBI?

KWANINI MUNGU HAJIBU MAOMBI?

Kawaida MUNGU huwa anajibu maombi, isipokuwa Majira yake mara nyingi ni tofauti na Majira yetu.. Sisi uwa tunapenda tujibiwe maombi muda ule ule tunapoomba!.. Hiyo inaweza kutokea ikiwa ombi uliloomba linastahili kujibiwa wakati huohuo..

Lakini ikiwa si mapenzi ya Mungu upate hiko ulichokiomba kwa wakati huo, basi itakupasa usubiri mpaka wakati wa Bwana, na hiyo haimaanishi kuwa Mungu hajakujibu!.. Ameshakujibu isipokuwa jibu lako hajaliweka leo, bali kaliweka kesho, au mwezi ujao au mwaka ujao, au miaka kadhaa ijayo..Kwasababu majibu mengine yanahitaji kwanza mtu aandaliwe ndipo apokee alichokiomba.

Haiwezekanani mtoto ambaye hajaanza hata shule amwombe baba yake amnunulie gari ili aendeshe kwasababu tu baba yake ana uwezo, halafu yule mzazi amjibu kwa kumnunulia hilo gari na kumpa aendeshe siku ile ile alipoomba..Ni kitu ambacho hakiwezekani! Kwa mzazi mwenye akili timamu.

Badala yake mzazi atalichukua lile ombi la mwanae na kuliweka akiba, mpaka atakapokuwa mtu mzima, amekomaa kiakili na kielimu ndipo ampe zawadi ile ya gari, ambayo aliomba miaka kadhaa nyuma…kwasababu wakati huo atakuwa anajua jinsi ya kuliendesha na amekomaa kiakili. Lakini mtoto huyo huyo akiomba peremende kutoka kwa baba yake ni rahisi kupewa wakati ule ule alioomba, kwasababu ombi lake ni dogo, na halihitaji maandalizi yoyote.

Vile vile na kwa upande wa Mungu wetu (ambaye tunamwita BABA)..yapo maombi ambayo anayajibu papo kwa hapo na mengine yatachukua muda, mpaka mtu ajibiwe…

Ndio maana baada ya kuomba ni vizuri kuruhusu mapenzi ya MUNGU yatimie kama Daudi alivyosema katika..

Zaburi 69:13 “Nami maombi yangu nakuomba Wewe, Bwana, Wakati ukupendezao; Ee Mungu, Kwa wingi wa fadhili zako unijibu, Katika kweli ya wokovu wako.

14 Uniponye kwa kunitoa matopeni, Wala usiniache nikazama. Na niponywe nao wanaonichukia, Na katika vilindi vya maji”.

LAKINI PAMOJA NA HAYO YAPO MAOMBI AMBAYO MUNGU HAJIBU KABISA!!. NA MAOMBI HAYO NI KAMA YAFUATAYO.

   1. MAOMBI YA TAMAA.

Mfano wa maombi ya tamaa ni yale mtu anaomba kitu si kwasababu ana haja na hiko kitu, bali kwasababu anataka kukitumia kwa anasa, au kwa mashindano, au kwa maonesho.

Mfano mtu ataomba Mungu ampe pesa, si kwasababu anataka atokane na changamoto Fulani za msingi, bali lengo lake ni ili awe nazo ili awaoneshe watu, au ajivune mbele za watu, au azitumie kwa anasa.. Mtu huyu anaweza asiseme kwa kinywa lakini moyo wake ndivyo vitu unavyovitamani.. Sasa maombi ya mtu wa namna hiyo biblia imesema huwa hayajibiwi.

Yakobo 4:3 “Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu”.

Kwahiyo ni muhimu sana, kuzichunguza NIA zetu, (kwamba kwanini tunaomba)..tuhakikishe nia zetu ni safi, na kweli tuna haja na hiko kitu tukiombacho kwa NIA njema.

    2. MAOMBI YA MTU MWOVU.

Mtu ambaye hamtaki Mungu moyoni mwake, lakini anataka vya Mungu (anataka kupokea kutoka kwa Mungu), maombi yake mtu huyo hayajibiwi!.

Ni muuaji na hataki wala hana mpango wa kuacha uuaji wake, ni mwizi wala hana mpango wa kuacha wizi wake, ni mzinzi na mwasherati wala hana mpango wa kuacha uasherati wake ijapokuwa anasikia mahubiri yahusuyo hayo kila siku, maombi yake mtu huyu hayajibiwi kulingana na biblia.

Isaya 1:15 “Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu nisiwaone; naam, mwombapo maombi mengi, sitasikia; mikono yenu imejaa damu.

16 Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya;

17 jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane”.

    3. MAOMBI YA MANUNG’UNIKO NA MALALAMIKO.

Maombi ya Manung’uniko na malalamiko ni yale mtu anaomba kwa kulaumu, na kunung’unika kana kwamba kaonewa au kadhulumiwa, maombi kama haya majibu yake mara nyingi ni kinyume.. badala ya mtu kupokea anachokinung’unikia kinyume chake anaweza kupoteza hata kile kidogo alicho nacho.

1Wakorintho 10:10 “Wala msinung’unike, kama wengine wao walivyonung’unika, wakaharibiwa na mharabu.

11  Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani”.

Epuka manung’uniko wakati wa maombi.. badala yake kuwa mtu wa shukrani, na mtu wa kumsihi Mungu kwa unyenyekevu na heshima.

    4. MAOMBI YA KUMJARIBU MUNGU.

Mfano wa maombi haya ni yale, shetani aliyompelekea Bwana YESU kule jangwani.

Luka 4:9  “Akamwongoza mpaka Yerusalemu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini;

10  kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake wakulinde;

11  na ya kwamba,mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.

12  Yesu akajibu akamwambia, Imenenwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako”.

Usiombe maombi ya kumwangalia BWANA atafanya nini… maombi ya nama hiyo hayana majibu, na zaidi wakati mwingine yanaishi kupokea adhabu badala ya Baraka.

1Wakorintho 10:9 “Wala tusimjaribu Bwana, kama wengine wao walivyomjaribu, wakaharibiwa na nyoka”

Jihadhari na aina hizo nne (4) za Maombi ili upokee majibu ya Maombi yako.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

FAIDA ZA MAOMBI.

JINSI YA KUPIGANA MAOMBI YA VITA.

Kuomba katika roho ni kupi? na je nifanye nini ili niweze kuomba hivyo?

NDUGU,TUOMBEENI.

KUNA AINA NGAPI  ZA MAOMBI?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments