Kwanini mke wa Ayubu hakupitia matatizo?

by Admin | 24 December 2024 08:46 am12

SWALI: Kwanini mke wa Ayubu hakupitia matatizo?


JIBU: Ni vema kufahamu kibiblia si kila tendo au jambo lililoandikwa lina umuhimu kulijengea hoja, kana kwamba usipolijua litakupunguzia sehemu  katika roho yako. Hapana, Kwamfano maswali kama Yohana alibatizwa na nani, Au mke wa Petro aliitwa nani au kaburi la Yesu lipo wapi kwasasa,  haya hayatusaidii sana kwasababu sio fundisho au agizo tuliloamuriwa tulishike.

Lakini ikiwa ni kutanua upana wa fikra zetu, basi tunaweza jifunza mambo kadhaa kuhusu matukio kama haya mfano wa hili la  mke wa Ayubu, kutohusishwa katika majaribu.

Ni swali ambalo watu huuliza, mbona watoto wote wa Ayubu, walikufa mifugo na mali pia viliondoka, lakini hatuoni mke wa Ayubu kuguswa.

Tukumbuke kuwa hakukuwa na agizo kwamba vyote alivyonavyo Ayubu ni LAZIMA viathiriwe…Hapana. Kwani tunaona hata miongoni mwa watumwa wake wapo walionusurika kifo. Na hao waliachwa wawe kama mashahidi wa yaliyotokea.

Ayubu 1:16

[16]Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Moto wa Mungu umeanguka kutoka mbinguni na kuwateketeza kondoo, na wale watumishi, na kuwaangamiza; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. 

Vivyo hivyo hata katika eneo la familia ya Ayubu hwenda ilipasa  abakie shahidi wa kueleza hali ya moyoni iliyokuwa inaendelea katika nyumba hiyo.

Mke wa Ayubu anatufunulia machungu yaliyowapata kiasi cha mwanadamu wa kawaida kushindwa kuvumilia, isipokuwa tu kumkufuru Mungu. Kikawaida mpaka mtu kufikia hatua ya kutoa maneno ya matusi, na kufuru kwa muumba wake, ujue kabisa jambo lililomkuta limeijeruhi sana nafsi yake mpaka kushindwa kuvumilia.

Ni Ayubu tu peke yake ndiye aliyeweza kustahimili hivyo, hata mke wake alipomshauri alikataa. Hii ni kutuonyesha jinsi gani mtu huyu alivyo mwogopa Mungu, zaidi ya matatizo yake. Kama tusingesikia aliyoyafanya mkewe, hakika tusingejua-fika hali waliyokuwa nayo Ayubu, na nguvu aliyojaliwa hata kutoa majibu kinyume na uhalisia wa kibinadamu.

habari ya Ayubu hutupa sisi funzo kubwa la uvumilivu katika Imani. Kwasababu tunapostahimili, sikuzote mwisho wake Mungu huwa anatupa faraja kubwa zaidi ya mwanzo.

Yakobo 5:11

[11]Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma. 

Shalom

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >>

https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

HUJAPEWA MBAWA ZA KUKIMBIA MATATIZO

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 9 (Kitabu cha Ayubu).

Kuguguna maana yake nini? (Ayubu 30:3 )

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/12/24/kwanini-mke-wa-ayubu-hakupitia-matatizo/