by Admin | 30 December 2024 08:46 pm12
Mwandishi na Uchambuzi wa kitabu cha wafilipi
Kama pale mwanzo kinavyojitambulisha “Waraka wa Paulo mtume kwa wafilipi”.
Paulo ndiye mwandishi wa kitabu hiki. Ni moja ya nyaraka ambazo Paulo aliziandika akiwa kama mfungwa, aidha kule Rumi.
Maudhui makuu ya waraka huu mfupi wenye sura nne(4) yalikuwa ni kuwatia moyo watakatifu na kuwahimiza waiendeleze furaha ya Mungu ndani yao,bila kukwamishwa na dhiki za aina yoyote, lakini pia sehemu ya pili ni kuwataka wapige hatua katika mwenendo wao ndani ya injili waliyoipokea.
Tukianza na hiyo sehemu ya kwanza:
Paulo anahimiza watakatifu kufurahi katika dhiki zote, ikizingatiwa kuwa Kanisa hili lilishuhudia vifungo na mapigo mengi ya Paulo. Kama tunavyosoma kwenye Matendo 16:16-40, Kule ambapo Paulo na Sila walipigwa sana na kutupwa gerezani, biblia inatuambia kulikuwa ni huku Filipi. Lakini hata katika waraka huu bado anashuhudia kuwa dhiki zake, zimekuwa wazi kwa maaskari, na watu wote wa huko (1:12-13).
Hivyo Paulo alijua watu wa Filipi huwenda wakawa na huzuni nyingi juu yake, au juu ya injili, kutokana na dhiki nyingi walizoziona kupitia yeye.
Lakini hapa anawaeleza kuwa yeye anafuraha sikuzote katika Kristo.
> Anaendelea kueleza furaha yake haiathiriwi na watu wanaomzushia fitna ili apitie mateso, maadamu anayeathirika ni yeye si Kristo. Basi bado anafurahi..(1:17-18)
> Anasema hata akihukumiwa kifo kwa ajili ya watakatifu, bado furaha yake itazidi zaidi wala haiwezi kuathiriwa..
Wafilipi 2:17-18
[17]Naam, hata nikimiminwa juu ya dhabihu na ibada ya imani yenu, nafurahi; tena nafurahi pamoja nanyi nyote.
[18]Nanyi vivyo hivyo furahini, tena furahini pamoja nami.
Hivyo anawahimiza pia na wafilipi wafurahi kama yeye, wala wasione huzuni kwasababu ya dhiki hizi, kwasababu tumewekewa kuwa sehemu yetu katika ushuhuda wa injili.
Wafilipi 1:29
[29]Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake;
Hizi ni sehemu nyingine kadha wa kadha Paulo akihimiza jambo hilo hilo,
Wafilipi 3:1
[1]Hatimaye, ndugu zangu, furahini katika Bwana.
Wafilipi 4:4
[4]Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, Furahini.
Sehemu ya Pili:
Katika sehemu ya pili Paulo anahimiza watakatifu kuwa na mwenendo unaipasa injili waliyopokea. Na hiyo ni ili wasiwe na ila na lawama,na udanganyifu. Kuonyesha kuwa injili, inayo na taratibu zake..Sio kuamini tu na kusema nimeokoka…bali pia kutii agizo lake.
Wafilipi 1:27
[27]Lakini mwenendo wenu na uwe kama inavyoipasa Injili ya Kristo, ili, nikija na kuwaona ninyi, au nisipokuwapo, niyasikie mambo yenu, kama mnasimama imara katika roho moja, kwa moyo mmoja mkiishindania imani ya Injili;
Anaendelea kusema watakatifu wana wajibu wa kunia mamoja, kutenda mambo yote bila majivuno,wala manung’uniko, wala mashindano, wanapaswa kutenda yote bila ubinafsi bali na ya wengine..
Anasisitiza watakatifu wanapaswa wawe wanyenyekevu, wenye nia ya Kristo..ambaye yeye hapo mwanzo alikuwa kama Mungu lakini alijishusha kwa kukubali kuachia nafasi yake, akawa kama mtumwa, akajinyenyekeza mpaka mauti ya msalaba,lakini Mungu akamkweza zaidi ya vitu vyote..Na sisi tulioipokea injili tunapaswa tuwe na nia hiyo hiyo ya unyenyekevu.(2:1-16)
Anasisitiza zaidi Wakristo wanapaswa wawe wapole, pia wawe waombaji na wenye shukrani.(4:5)
Halikadhalika ni wajibu wetu sote kuutumiza wokovu tulioupokea kwa kuogopa na kutetemeka, kwasababu ndiye Mungu atendaye kazi ndani yetu.(2:12-13)
Pamoja na hayo Watakatifu wana wajibu pia wa kuyahakiki mambo yote yaliyo mazuri na kuyaiga, (2:1-2)
Wafilipi 4:8
[8]Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.
Lakini pia anawatahadharisha kujiepusha na wahubiri wa uongo akianzana na wayahudi (watu wa tohara), ambao wanahubiri wokovu kwa njia ya torati zaidi ya ile tuipatayo ndani ya Kristo Yesu kwa njia ya imani. (3:1–16,)
Pamoja watumishi ambao fundisho lao ni la mambo ya duniani tu, na sio yale ya kumwelekeza mtu mbinguni (3:17-21).
Mwisho, Paulo anatoa salamu zake, na shukrani kwa huduma ya utoaji kanisa hilo lililomfanyia, na linaloendelea kumfanyia.
Hivyo kwa hitimisho, waraka huu maudhui kuu ni kuwafariji watakatifu wafurahi katika mambo yote, tukizingatia tunda la Roho ni furaha. Yesu alisema tufurahi na kushangalia pale tunapoudhiwa, kwa ajili ya jina lake. Hivyo, hakuna eneo lolote furaha ya Mungu ndani yetu ,inastahili kukatishwa. Tupitiapo magonjwa kama Epafrodito(2:25-30), shida, njaa, tumefundishwa kuyaweza yote ndani ya Kristo(4:12-3). Hivyo furaha yetu haiwezi kuathiriwa..Ilinde furaha yako.
Lakini anahimiza mwenendo upasao injili. Kwamba huo utaweza kufanikiwa pale tunapokubali kuwa na nia kama ile ya Kristo, ya unyenyekevu.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >>
https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Rudi Nyumbani
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/12/30/uchambuzi-wa-kitabu-cha-wafilipi/
Copyright ©2025 unless otherwise noted.