Mwandishi na uchambuzi wa kitabu cha Wathesalonike wa kwanza.

by Admin | 1 January 2025 08:46 pm01

Kitabu hichi kama kinavyojitambulisha katika mwanzo wake  ‘Waraka wa kwanza wa Paulo mtume kwa Wathesalonike’.

Paulo ndiye mwandishi wa waraka huu. Aliuandika akiwa Korintho. Tumelijua hilo  kufuatana na ujio wa Timotheo kutoka Makedonia na kumpa ripoti nzuri ya maendeleo yao ya kiroho,  kuanzia eneo la imani, upendo na tumaini, ambazo tunazisoma katika kitabu cha Matendo ya mitume sura ya 18.

Kwasababu ya ugumu wa kuwafikia uliochangiwa na shetani,  Akasukumwa kuandika nyaraka hizi mbili kwa watakatifu hawa, kuwajenga katika maeneo kadha wa kadha,  ambazo zilipishana kwa miezi kadhaa tu.

Kitabu hichi kina sura tano (5)

Maudhui kuu ya waraka huu ni matatu(3)

  1. kwanza ni kuwahimiza watakatifu kudumu katika imani  husasani katika nyakati za dhiki.
  2. Pili kuwapa mwongozo wa mwenendo sahihi upasao ndani ya imani.
  3. Tatu, kuwapa majibu ya maswali yahusuyo ujio wa pili wa Yesu Kristo na kiyama ya wafu ambayo walikuwa nayo.

Tuyaangalie hayo maeneo matatu kwa ufupisho;

1) Kuhusu kudumu katika Imani.

Paulo anaanza kwa kuwashuhudia kwa maneno mengi dhiki alizozipata katika kuieneza injili kwao, na jinsi alivyoweza kustahimili, Na kwamba wao pia wanapopitia dhiki za namna mbalimbali kutoka kwa watu wa taifa lao, wasivunjike moyo na kuiacha imani. Wajue kuwa dhiki pia wamewekewa watakatifu.

1 Wathesalonike 2:14

[14]Maana ninyi, ndugu, mlikuwa wafuasi wa makanisa ya Mungu yaliyo katika Uyahudi, katika Kristo Yesu; kwa kuwa mlipata mateso yale yale kwa watu wa taifa lenu wenyewe, waliyoyapata na hao kwa Wayahudi;

[15]ambao walimwua Bwana Yesu, na hao manabii, na kutuudhi sisi; wala hawampendezi Mungu, wala hawapatani na watu wo wote;

1 Wathesalonike 3:3

[3]mtu asifadhaishwe na dhiki hizi; maana ninyi wenyewe mnajua ya kuwa twawekewa hizo.

2) Sehemu ya pili ambayo inahusu mwenendo upasayo wa imani.

Paulo anagusia maeneo mengi kuanzia upendo hadi utakatifu kwamba wana wajibu wa kuongezeka katika hivyo ili wasionekane katika lawama katika siku ile ya kuja Bwana wetu Yesu Kristo kutoka mbinguni.

1 Wathesalonike 3:12-13

[12]Bwana na awaongeze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi, na kwa watu wote, kama vile sisi nasi tulivyo kwenu;

[13]apate kuifanya imara mioyo yenu iwe bila lawama katika utakatifu mbele za Mungu, Baba yetu, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu pamoja na watakatifu wake wote.

> Anagusia pia katika eneo la kudhibiti miili yetu katika utakatifu na heshima na sio katika tamaa mbaya(4:1-5),

> Halikadhalika wakristo kuonyesha mwenendo wa adabu kwa walio nje, kwa kutenda shughuli zetu wenyewe ili tusiwe na uhitaji wa vitu vyao (4:11-12)

> Pia kama watakatifu ni mwiko kulipana baya kwa baya (5:15),

> Tunapaswa sikuzote tudumu katika kuomba, kufurahi, kushukuru kwa kila jambo, tusimzimishe Roho, tusipuuzie unabii, tujitenge na ubaya wa kila namna.(5:16-23)

> Lakini Paulo anahimiza mwenendo wetu unapaswa uende mpaka kwa wale wanaotusimamia na kutuchunga kwamba tuwastahi.

1 Wathesalonike 5:12-13

[12]Lakini, ndugu, tunataka mwatambue wale wanaojitaabisha kwa ajili yenu, na kuwasimamia ninyi katika Bwana, na kuwaonyeni;

[13]mkawastahi sana katika upendo, kwa ajili ya kazi zao. Iweni na amani ninyi kwa ninyi.

> Na katika yote ni wajibu wetu sote kufarijiana na kuonyana na kuvumiliana na kutiana nguvu(5:14-15)

3) Sehemu ya tatu ambayo anatoa majibu ya maswali yahusuyo ujio wa pili wa Kristo, na kiyama ya wafu

Paulo anawafiriji kwa kuwaambia wafu waliolala katika Kristo, siku ya mwisho wataamshwa wote..wasidhani kuwa hawatawaona wapendwa wao waliotangulia.

1 Wathesalonike 4:13-16

[13]Lakini, ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini.

[14]Maana, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye.

[15]Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti.

[16]Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza.

Sambamba na hilo, anawafumbua macho juu ya nyakati na majira ya kurudi kwa Yesu kwamba hakutakuwa na taarifa zozote au viashiria vyovyote kwa watu wa dunia. Bali itawajilia kwa ghafla tena katika nyakati ambazo wanasema kuna amani na shwari.

Hivyo anawatahadharisha watakatifu nao kuwa macho wakati wote.

1 Wathesalonike 5:1-11

[1]Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie.

[2]Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.

[3]Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.

[4]Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi.

[5]Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza.

[6]Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi.

[7]Maana walalao usingizi hulala usiku, pia na walewao hulewa usiku.

[8]Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu.

[9]Kwa kuwa Mungu hakutuweka kwa hasira yake, bali tupate wokovu, kwa Bwana wetu Yesu Kristo;

[10]ambaye alikufa kwa ajili yetu, ili tuishi pamoja naye, kwamba twakesha au kwamba twalala.

[11]Basi, farijianeni na kujengana kila mtu na mwenzake, vile vile kama mnavyofanya.

Hivyo kwa ufupi ni kuwa waraka huu. Unawataka wakristo kuthibitika katika imani, haijalishi ni changamoto gani za kimaisha au ugumu gani watakutana nao kwa wapinga-kristo, Wanapaswa waendelee kusimama hivyo hivyo  mpaka mwisho katika Kristo Yesu.

Lakini pia wajue  Bwana anarudi, na atakuja ghafla, Hivyo yawapasa  wawe watu wa mchana sikuzote wasilale usingizi kwa kuhakikisha wanaishi maisha ya utakatifu, na adabu, ili atakaporudi Bwana wasiwe na lawama yoyote.

Bwana akubariki.

Je! Umeokoka? Kama ni la, fungua hapa kwa mwongozo wa sala ya wokovu. >>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Mwandishi na Uchambuzi wa kitabu cha Wafilipi.

VITA VYA KIFIKRA BAADA YA KUZALIWA MARA YA PILI

Mwandishi na uchambuzi wa kitabu cha Yakobo.

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/01/01/uchambuzi-wa-kitabu-cha-wathesalonike-wa-kwanza/