Vile vile waraka wa Waefeso uliwahusu waefeso peke yao? Na si makanisa yote ikiwemo sisi, hivyo kuna vitu si sahihi kuvibeba kutoka kwenye waraka huo?.
Jibu: Awali turejee salamu za kwanza za Paulo kwa baadhi ya makanisa…
Wakolosai 1:1 “Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo, ndugu yetu,
2 kwa ndugu watakatifu, waaminifu katika Kristo, WALIOKO KOLOSAI. Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu”.
Ni kweli hapa anaonyesha kuwa waraka huu umekusudiwa kwa wakristo walioko KOLOSAI…
Lakini swali ni je?…ni wakristo walioko Kolosai tu ndio waliokusudiwa wasome huu waraka au hata makanisa mengine ya mahali pengine ikiwemo sisi tuishio wakati huu wa mwisho?.
Jibu la swali hili tutalipata katika waraka huu huu wa Wakolosai…
Wakolosai 4:16 “Waraka huu ukiisha kusomwa kwenu fanyeni kwamba usomwe katika kanisa la Walaodikia pia; na ule wa Laodikia usomwe na ninyi”.
Kumbe ulikuwepo waraka mwingine ulioandikwa wa kanisa la Laodikia ambao ungepaswa usomwe kwa Wakolosai, na huu wa Wakolosai ulipaswa ukasomwe kwa kanisa la Laodikia.
Ikiwa na maana kuwa nyaraka za Paulo, ijapokuwa alizipeleka katika kanisa husika lakini hakuzizuia zosisomwe katika makanisa mengine, kwasababu mambo aliyokuwa anayahubiri kanisa moja na kuyakemea ndio hayo hayo atakayoyafundisha na kuyakemea katika makanisa mengine, na ndio hayo hayo pia yanatufaa katika makanisa ya siku za mwisho.
Utaona pia salamu ya kwanza ya Paulo kwa Wagalatia, ilihusu makanisa yote yaliyopo Galatia na si kanisa moja tu….
Wagalatia 1:1 “Paulo, mtume, (si mtume wa wanadamu, wala kutumwa na mwanadamu, bali na Yesu Kristo, na Mungu Baba aliyemfufua kutoka kwa wafu),
2 na ndugu wote walio pamoja nami, kwa makanisa ya Galatia”.
Maana yake kama makanisa yaliyokuwepo Galatia yalikuwa mia (maana Galatia ilikuwa ni kubwa mno, tazama ramani)..basi makanisa yote yalisomewa huo waraka pasipo kujalisha tabia zao.
Pia utazidi kulithibitisha hilo katika kitabu cha waraka kwa Wakorintho, utaona Paulo anaelekeza kuwa si kwa Wakorintho peke yao bali na kwa watu wote wanaoliitia jina la Bwana kila mahali ikiwemo sisi..
1 Wakorintho 1:1 “Paulo, aliyeitwa kuwa mtume wa Yesu Kristo kwa mapenzi ya Mungu, na Sosthene ndugu yetu,
2 kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, wale waliotakaswa katika Kristo Yesu, walioitwa wawe watakatifu, pamoja na wote wanaoliitia jina la Bwana wetu Yesu Kristo kila mahali, Bwana wao na wetu”
Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba nyaraka zote za Mtume Paulo na biblia yote kwa ujumla yafaa kwa mafundisho kwa makanisa yote na vizazi vyote..
2 Timotheo 3:16 “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki”
Hivyo si sahihi kusema waraka huu waliandikiwa Wakorintho tu peke yao au Wagalatia bali unatuhusu hata sisi..
Mafundisho yaliyohusu utakatifu ikiwemo kujisitiri na kuishi maisha ya kuepuka dhambi yaliwahusu watu wa kanisa la kwanza na yanatuhusu sisi pia..
Mafundisho yanayohusu nafasi za wanawake na wanaume katika kanisa sawasawa na 1Wakorintho 14:34 na 1Timotheo 2:8-12, yanatuhusu hata sisi.
Kupunguza Neno lolote katika biblia ni kosa, Bwana atusaidie.
Shalom