ISHARA YA KANISA LA LAODIKIA

ISHARA YA KANISA LA LAODIKIA

Karibu katika mafunzo ya biblia.

Kwanini tunasema kuwa hili ni kanisa la Mwisho la Laodikia?, Je ni viashiria gani vinavyotutambulisha kuwa hali ya kanisa la Laodikia lile la saba ambalo Mtume Yohana alilonyeshwa kwenye Maono  katika kitabu cha Ufunuo ndio hali halisi ya kanisa letu la siku za mwisho?.

Awali ya yote hebu tujikumbushe historia ya yale makanisa saba, tunayoyasoma katika kitabu cha Ufunuo Mlango wa 2 na wa 3.

Makanisa saba tunayoyasoma katika kitabu cha Ufunuo ni makanisa ambayo yalikuwa katika miji 7 tofauti tofauti. (Efeso, Smirna, Pergano, Thiatira, Sardi, Filadelfia na Laodikia, Ufunuo 1:11).

Hivyo  na makanisa hayo yalijulikana kwa majina ya miji hiyo,  na Yote ilikuwa inapatikana katika eneo lijulikanalo kama “Asia Ndogo” ambapo kwasasa ni nchi ya “Uturuki”.

Sasa kila kanisa lilikuwa na tabia yake, kulingana na huo mji (unaweza kusoma tabia hizo katika Ufunuo 2-3). Na kanisa la Mwisho kabisa kutajwa ambalo ndio la saba lililoitwa Laodikia lilikuwa na tabia nyingine ya kipekee ambayo kwa hiyo ndiyo tutajua kuwa kanisa letu la sasa linafanana na kanisa la huo mji au la!.

Sasa kabla ya kwenda kusoma tabia za kanisa hilo katika kitabu cha Ufunuo, hebu kwanza tuweke msingi mwingine wa kuelewa jambo lingine, ambalo litatusaidia kuelewa hili vizuri.

Katika biblia maandiko yanatabiri kuwa dalili za siku za mwisho ni Maasi kuongezeka katika kiwango cha miji ya Sodoma na Gomora, au miji ya Nyakati za Nuhu (Soma Luka 17:26-28).

Maana yake ni kuwa kama hali ya maovu haijafikia kile kiwango cha maasi ya Sodoma na Gomora, basi bado ule mwisho utakuwa upo mbali, lakini kama hali ya mji itafikia kile kiwango cha maasi ya Sodoma na Gomora basi ni wazi kuwa ule mwisho umefika.

Kwahiyo ni sahihi kusema kuwa  Miji ya Sodoma na Gomora ni ishara au alama ya miji ya siku za mwisho, Hivyo tukitaka kujua kuwa tupo siku za mwisho basi tujilinganishe na miji ya Sodoma na Gomora. (2Petro 2:6 na Yuda 1:7).

Na sasa tunaona kabisa kuwa kizazi chetu ni kama kile cha Sodoma na Gomora na hata huenda kimepita, kwasababu katika miji ya Sodoma na Gomora kulikuwa na mwingiliano wa ndoa za jinsia moja..vile vile na sasa hali ni hiyo hiyo, ushoga upo kila mahali, mauaji, dhuluma n.k kwahiyo tupo siku za mwisho.

Vile vile na kanisa la Mji wa Laodikia, ambao ulikuwepo katika enzi  za kanisa la Kwanza,  lilikuwa ni Ishara ya kanisa la siku za mwisho. Maana yake ni kuwa tukitaka kujua kuwa tunaishi katika kanisa la mwisho, basi tunapaswa tujilinganishe kanisa letu na lile la Laodikia. Tukiona yanafanana kitabia basi tujue kuwa hili ndio kanisa la mwisho na unyakuo umekaribia.. lakini tukiona kuwa bado hatujafikia viwango vya kanisa lile basi tujue kuwa ule mwisho huenda bado sana.

Sasa hebu tusome tabia za kanisa la Laodikia katika biblia.

Laodikia 3:14 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.

15  NAYAJUA MATENDO YAKO, YA KUWA HU BARIDI WALA HU MOTO; INGEKUWA HERI KAMA UNGEKUWA BARIDI AU MOTO.

16  Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.

17  Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi”.

Umeona tabia za kanisa la Laodikia?..Biblia inasema ni kanisa ambalo lilikuwa vuguvugu, si moto wala si bariki.. mfano kamili wa kanisa la wakati huu. (Kumbuka hapa tunazungumzia kanisa na si watu wa ulimwengu, watu wa ulimwengu ishara yao ni miji ya Sodoma na Gomora na sisi kanisa ishara yetu ni kanisa la mji wa Laodikia).

Kanisa la wakati huu utaona mtu mguu mmoja nje mguu mmoja ndani, leo yupo kanisani kesho disco, leo anamwabudu Bwana kesho anasikiliza miziki ya kidunia, simu yake nusu ina nyimbo za injili nusu nyimbo za kidunia, kabati lake nusu lina nguo za kujisitiri nusu lina nguo za nusu uchi, maneno yake nusu ya heshima nusu ya kihuni, biashara yake nusu ni halali nusu si haramu, duka lake nusu lina bidhaa njema nusu lina bidhaa haramu (pombe, na sigara), leo atatoa sadaka kesho anaonga/ anaogwa.n.k

Hiyo ndiyo ilikuwa hali ya kanisa la Laodikia na ndio hali ya kanisa la Sasa tulilopo.

Hiyo ndiyo alama pekee inayotutambulisha siku si nyingi unyakuo wa kanisa utatokea. Kwasababu hakutakuwa na kanisa lingine litakalotokea lenye tabia nyingine, hili la Laodikia biblia imetabiri ndio kanisa la Mwisho baada ya hapo ni unyakuo ndio maana utaona pale, baada ya ujumbe wake kumalizika kilichofuata ni Yohana kuchukuliwa juu mbinguni.

Ufunuo 4:1 “Baada ya hayo naliona, na tazama, mlango ukafunguka mbinguni, na sauti ile ya kwanza niliyoisikia kama sauti ya baragumu ikinena nami, ikisema, Panda hata huku, nami nitakuonyesha mambo ambayo hayana budi kuwako baada ya hayo”.

Wakati kanisa hili la Laodikia limechafuka hivi, Bwana analiandaa kundi lake dogo, na kuliambia litoke huko, kama vile alivyowaokoa Nuhu na Luthu..Vile vile kanisa la Laodikia litaingia katika dhiki kuu kwasababu ni kanisa vuguvugu lakini kundi dogo ambalo litakuwa safi na litakuwa Moto na si Vuguvugu hilo litaenda na Bwana katika unyakuo.

Ndugu unyakuo umekaribia sana, Yesu yupo Mlangoni kurudi, ondoka katika uvuguvugu, wa kidunia, kuwa Moto.. Ukiamua kumfuata Kristo basi mfuate kwelikweli, usiige desturi za kiduni, ukiamua kuwa mtu wa kujisitiri fanya hivyo kikweli kweli usiwe nusu nusu, ukiamua kumfuata Yesu basi jikane kweli kweli.

Uvuguvu Kristo anauchukia kuliko hata Yule mtu aliye baridi kabisa.. kwasababu yeye mwenyewe anasema ni heri mtu awe moto au baridi kuliko vuguvugu..

Bwana atusaidie.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

AGENDA KUBWA YA SHETANI KWA KANISA HILI LA LAODIKIA.

SAUTI NI SAUTI YA YAKOBO, LAKINI MIKONO NI YA ESAU.

Babewatoto ni nani katika biblia?(Isaya 34:14).

Babeli ni nchi gani kwasasa?

JE NI KWELI SAMAKI NGUVA YUPO?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments