USIJISIFIE KARAMA KWA UONGO.

USIJISIFIE KARAMA KWA UONGO.

Mithali 25:14 “Kama mawingu na upepo pasipo mvua; Ndivyo alivyo yeye ajisifiaye karama kwa uongo”.

Njia nyingine shetani anayoitumia kuwaangusha watu na kudanganya watu, ni kupitia “karama za uongo”.. Hii inatokea pale ambapo mtu anajipandikiza karama ambayo hana, na anajitangaza kuwa anayo kwa wote, jambo ambalo lina madhara makubwa sana kiroho.

Zifuatazo ni ishara za karama ya kweli ndani ya Mtu, maana yake mtu akikosa hizi ishara basi huenda hiyo karama hana au anayo lakini imeshambuliwa na kutumiwa na adui.

  1. KUWAKAMILISHA WATAKATIFU.

  Mtu mwenye karama ya kweli ya Mungu, ni lazima atakuwa na msukumo wa kuwafanya watu wazidi kukamilika katika Utakatifu, na kumcha Mungu…hata kufikia viwango ambavyo Mungu anataka (Waebrania 12:14), maana yake kila siku atakuwa anatafuta kutatua kasoro zinazofanya watu au yeye mwenyewe asiwe wakamilifu kwa Mungu..Lakini kama karama ya mtu inazidi kumfanya yeye mwenyewe asiwe mkamilifu, au kuwafanya watu wasiwe wakamilifu kwa Mungu, au wasihamasike kumtafuta Mungu zaidi, au kujitakasa… badala yake inawahamasisha kutafuta mambo ya kidunia, basi huyo mtu haijalishi anajiita Mchungaji au Mtume, au nabii kiuhalisia hana hiyo karama..

Utauliza tunalithibitisha vipi hilo kimaandiko… hebu tusome maandiko yafuatayo..

Waefeso 4:11  “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; KWA KUSUDI LA KUWAKAMILISHA WATAKATIFU….”

2. IPO KWA LENGO LA KUWAHUDUMIA WATU NA SI KUJIHUDUMIA YENYEWE.

Karama yoyote ya kweli ni lazima iwe na HUDUMA, na huduma maana yake ni kutoa msaada kwa wengine, na msaada tulioagizwa sisi wakristo tu utoe ni ule wa kiroho na usio na gharama.. Maana yake hatujaagizwa kuwatoza watu vitu ili wapokee kutoka kwetu.

Hiyo ikiwa na maana kuwa kama mtu yeyote anajiita Mchungaji, au Nabii, au Mwinjilisti au Mwimbaji, au Mwimbaji, halafu huduma yake anaitoa kwa malipo, ni wazi kuwa hana hiyo karama, haijalishi anajua kuimba kiasi gani au anajua kuhubiri kiasi gani, au anatoa unabii kiasi gani… Kama hatakuwa mtu wa kutoa Huduma bila kutazamia malipo, huyo atakuwa anahudumu kwa roho nyingine ya adui.

Utasema tulithibithisha vipi hili nalo  kimaandiko… Tuendelee na mstari ule wa 12..

Waefeso 4:11  “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu;

12  kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, HATA KAZI YA HUDUMA ITENDEKE….”

3. IPO KWA LENGO LA KUUJENGA MWILI WA KRISTO.

Mwili wa Kristo inajengwa kwa viungo vyote na si kimoja au viwili.. Kristo alipokuwa hapa duniani hakuwa mlemavu.. wala hata baada ya kufa hakuwa mlemavu (maandiko yanaonyesha mifupa yake haikuvunjwa pale msalabani).. Na sisi ni viungo vya Kristo, hivyo ili tuujenge mwili mkamilifu wa Yesu ni lazima tuwepo wote pamoja..

Mtu akijiona Nabii, au Mtume, au Mwalimu na hayupo katika ushirika na viungo vingine katika kanisa, ni yeye tu kama yeye, mtu huyo si kiungo cha Kristo, na hana hiyo karama anayojivunia..

1Wakorintho 12:14  “Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi.

15  Mguu ukisema, Kwa kuwa mimi si mkono, mimi si wa mwili; je! Si wa mwili kwa sababu hiyo?

16  Na sikio likisema, Kwa kuwa mimi si jicho, mimi si la mwili; je! Si la mwili kwa sababu hiyo?

17  Kama mwili wote ukiwa jicho, ku wapi kusikia? Kama wote ni sikio ku wapi kunusa?

18  Bali Mungu amevitia viungo kila kimoja katika mwili kama alivyotaka.

19  Lakini kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi?

20  Lakini sasa viungo ni vingi, ila mwili ni mmoja.

21  Na jicho haliwezi kuuambia mkono, Sina haja na wewe; wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu, Sina haja na ninyi”.

Tunazidi kulithibitsha hili katika mstari ule ule wa 12..

Waefeso 4:11 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu;

12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, HATA MWILI WA KRISTO UJENGWE”

Kama Karama haiujengi mwili wa Kristo ni karama ya uongo.

Kwahiyo ni lazima kila mtu mwenye karama Fulani ya Roho awe na sifa hizo, lakini kama hana hizo sifa basi huenda hana hiyo karama anayojivunia kuwa anayo au alikuwa nayo lakini sisi imeshambuliwa na inatumiwa na adui.

Na watu wote wanaojivunia karama za Uongo, biblia imesema ni kama mawingu yasiyo na maji.

Mithali 25:14 “Kama mawingu na upepo pasipo mvua; Ndivyo alivyo yeye ajisifiaye karama kwa uongo”.

Maana yake ni watu wanaotoa matumaini ya kusitawisha jambo lakini mwisho wao ni ukame tu.. Hivyo si wakuaminiwa.

Bwana atusaidie karama zetu ziwe za kweli.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

Karama ya pili inayozungumziwa katika 2Wakorintho 1:15 ndio ipi?

ICHOCHEE KARAMA YAKO.

Nini tofauti kati ya Kipawa na Karama?

JIHADHARI NA UONGO WA SHETANI UNAOKARIBIANA NA UKWELI.

NA VIUNGO VYETU VISIVYO NA UZURI VINA UZURI ZAIDI SANA.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Stephen kyalo
Stephen kyalo
1 year ago

Napenda sana neno la Mungu