JIHADHARI NA UONGO WA SHETANI UNAOKARIBIANA NA UKWELI.

JIHADHARI NA UONGO WA SHETANI UNAOKARIBIANA NA UKWELI.

Biblia inasema shetani ni Baba wa uongo Yohana 8:44, Maana yake kazi yake ni kusema uongo, na uongo sio wa kudanganya watumishi wake, hao siku nyingi tayari ni wa kwake…anachokifanya ni kuwafundisha watumishi wake uongo, ili wakadanganye wengine…Ndio maana anaitwa Baba wa uongo.

Na uongo wake unakaribia sana kufanana na ukweli…ili hela bandia iweze kuwadanganya wengi ni lazima ikaribiane sana kufanana na hela halali…kwahiyo jinsi uongo unavyozidi kukaribiana na ukweli ndivyo unavyokuwa na nguvu zaidi..

Kwahiyo shetani anajua kabisa Neno la Mungu ndio KWELI…Kwahiyo ili atengeneze uongo wenye nguvu kubwa ni lazima autengeneze unaokaribiana sana kufanana na Kweli ya Neno la Mungu…maana yake ni kwamba atatumia maandiko/biblia kuupotosha ukweli katika utashi wa hali ya juu kiasi kwamba ni ngumu kugundua kama Neno hilo limepotoshwa…Huo ndio uongo wa shetani unaozungumziwa katika biblia…

Kama unakumbuka wakati anamjaribu Bwana kule jangwani, utaona alikuwa anatumia maandiko yaani neno la Mungu…hakuwa anatumia kitabu cha sayansi au mithali za wahenga…bali alikuwa anatumia Neno la Mungu kwamba imeandikwa hivi au vile…kiasi kwamba kama Bwana asingekuwa mtu wa Rohoni wa kulielewa Neno sana, na kufananisha maandiko vyema angenaswa na mtego wa Ibilisi na angeusikiliza uongo wake.

Na hadi leo mbinu ya shetani ni hiyo hiyo, ya kuligeuza Neno la Mungu la kweli kuwa uongo….

Kama wengi wetu tunavyojua Mungu alimwagiza Musa kutengeneza “Yule nyoka wa shaba” ambaye aliambiwa amnyanyue juu ili kila amtazamaye ambaye kaumwa na nyoka aweze kupona, andiko hilo linapatikana katika kitabu cha Hesabu 21:6-9.

Sasa kupitia andiko hili shetani kawadanganya watu kuwa Ni halali kutengeneza sanamu ya nyoka, au ya mtu Fulani katika biblia, au ya kitu na kuitazama, na kuisujudia au kuiheshimu na hata kuiabudu ili kupata faida Fulani kutoka katika hiyo, labda uponyaji au Baraka.

Sasa tukirudi katika habari hiyo ya nyoka wa shaba..utaona kuwa Mungu hakuwaambia wana wa Israeli waiabudu, wala waiangukie, wala waipe heshima yoyote, wala haikuwekwa pale kama kitu kitakatifu…bali Mungu aliiweka pale kwa lengo la kuwatafakarisha upumbavu wao walioufanya na wanaoufanya wa kumnung’unikia Mungu..na hivyo Mungu akawaonyesha kwamba amewachapa kwa kiboko cha nyoka (Ndio maana utaona ni fimbo iliyozungushiwa nyoka)..Ili watafakari, na kutubia uovu wao…na waliotazama na kutafakari ndio waliopona.

Kama wewe ni msomaji wa biblia utakuja pia kuona kuna wakati wafilisti walilichukua sanduku la Agano kutoka Israeli na Mungu akawapiga kwa majipu mabaya na tauni…ndipo wafilisti wakatengeneza sanamu za majibu na za panya kuzipeleka Israeli kuonyesha kwamba wametambua wamefanya kosa na wametambua kwamba Mungu kawaadhibu kwa majibu na Tauni ambayo inatokana na panya..na hivyo wanatubu..na walipofanya hivyo ndipo Mungu akaacha kuwapiga….kasome 1Samweli 6:1-11.

Sasa wafilisti hawakutengeneza hizo sanamu kwa lengo la kuziabudu, wala kuzipa heshima, wala kuzitumikia…bali kwa lengo la kutubu (kwamba wametafakari makosa yao na kujua mkono wa Mungu umekua juu yetu kama mfano wa hayo majibu)..

Kwahiyo hata wana wa Israeli Mungu aliwaambia waitengeneze sanamu ile ili iwatafakarishe, na ili wamwogope Mungu..kwamba wakimuudhi Mungu wao..anaweza kuwachapa kwa fimbo ya kitu chochote kile, inaweza kuwa fimbo ya nyoka, fimbo ya wanyama wengine wakali, fimbo ya magonjwa au chochote kile, na hivyo wamweshimu na kuzishika amri zake. Na wachache waliotii na kuelewa ujumbe walipona lakini wengine walikufa…na hata baada ya janga hilo kuisha kuna wachache ambao bado walikuwa hawajamwelewa Mungu wakaihifadhi sanamu ile na kuanza kuiabudu na kuifanya ni chombo cha ibada…pasipo kujua kuwa wanamchukiza Mungu kwa kuiabudu ile fimbo ya nyoka wa shaba…Mungu akawa anawaadhibu kwa kuiabudu lakini bado wakawa na shingo ngumu kutoivunja vunja ile fimbo ya nyoka wa shaba. Sanamu ile ilikuja kuendelea kupata umaarufu, hadi kufikia Israeli wengi kuiabudu.

Mpaka siku ilipofika alipotokea mtumishi wa Mungu, Mfalme Hezekia, alipoona Taifa linapotea kwa ibada za sanamu, kwa kuiabudu hiyo sanamu ya nyoka wa shaba…ndipo aliponyanyuka na kwenda kuivunja vunja na kuitowesha kabisa, na Mungu akambariki kwa kufanya hivyo.. Tusome..

2Wafalme 18:1 “Ikawa katika mwaka wa tatu wa Hoshea, mwana wa Ela, mfalme wa Israeli, Hezekia, mwana wa Ahazi, mfalme wa Yuda, alianza kutawala.

2 Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka ishirini na kenda katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Abiya, binti Zekaria.

3 Akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana, mfano wa yote aliyoyafanya Daudi, baba yake.

4 Alipaondoa mahali pa juu, akazibomoa nguzo, akaikata hiyo Ashera; AKAIVUNJA VIPANDE VIPANDE ILE NYOKA YA SHABA ALIYOIFANYA MUSA; MAANA HATA SIKU ZILE WANA WA ISRAELI WALIKUWA WAKIIFUKIZIA UVUMBA; NAYE AKAIITA JINA LAKE NEHUSHTANI

5 Alimtumaini Bwana, Mungu wa Israeli; hata baada yake hapakuwa na mfano wake katika wafalme wote wa Yuda, wala katika hao waliomtangulia.

6 Maana alishikamana na Bwana, hakuacha kumfuata, bali alizishika amri zake Bwana alizomwamuru Musa”.

Umeona hapo mstari wa 4 ???…Aliivunja vunja maana yake ni kwamba, halikuwa agizo la Mungu kuiabudu, wala kuitolea uvumba, wala kuipa heshima yoyote ile…ni machukizo makubwa!.
Na sanduku la Agano ni hivyo hivyo, Mungu alitoa maagizo kwa Musa litengenezwe lakini hakuna mahali popote Mungu aliagiza liabudiwe…hata hivyo wana wa Israeli wakati Fulani walipojaribu kuligeuza kuwa ni chombo cha Ibada, liliwaletea laana badala ya Baraka kasome 1Samweli 4:1-11. Hakuna kitu chochote kile kwenye biblia nzima agano la kale wala agano jipya kinachoitwa sanamu ambacho Mungu alitoa maagizo kiabudiwe wala kitukuzwe. Ni uongo wa shetani ambao lengo lake ni kuugeuza ukweli wa Neno la Mungu.

Hivyo ndugu..usidanganywe na uongo wa shetani ambao unakaribia sana kufanana na ukweli..usidanganyike na kuabudu sanamu, usidanganyike na kuisujudia sanamu ya bikira Maria wala ya Petro, wala inayojulikana kama sanamu ya Bwana Yesu, wala usiisujudie misalaba, wala kitu chochote kile…Ni machukizo makubwa…biblia inasema..

Kutoka 20:4 “Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia.

5 Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,

6 nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu”.

Na pia inasema..

Ufunuo 21:7 “Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.

8 Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili”.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Je! Bwana Yesu alitumwa kwa Waisraeli tu peke yao?

NA ROHO NA BIBI-ARUSI WASEMA, NJOO!

WAKATI WA BWANA KUKUVUSHA, NI LAZIMA ARUHUSU JESHI LA ADUI KUNYANYUKA.

MIJI YA MAKIMBILIO.

NA MTU MMOJA AKAVUTA UPINDE KWA KUBAHATISHA, AKAMPIGA MFALME

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments