Je! Bwana Yesu alitumwa kwa Waisraeli tu peke yao?

Je! Bwana Yesu alitumwa kwa Waisraeli tu peke yao?

SWALI: Je! Bwana Yesu alitumwa kwa Waisraeli tu peke yao au kwa watu wote wa mataifa..Maana yeye mwenyewe alisema katika Mathayo 10:5, kwamba wasihubiri kwa watu wa Mataifa.


JIBU: Tusome..

Mathayo 10:5 “Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema, Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie.

6 Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli”

Ni kweli Bwana aliwaagiza wanafunzi wake wasiende kuhubiri Injili kwa watu wa mataifa kipindi yupo nao, bali wawaendee kwanza wayahudi (yaani waisraeli). Sasa kwanini awazuie wasiende kuwahubiria watu wa Mataifa?

Jibu ni rahisi: Ni kwasababu wakati wa Mataifa kwenda kuhubiriwa injili ulikuwa bado hujafika. Tunaweza kujifunza katika mfano wa kawaida wa Maisha. Unapotengeneza bidhaa yako mpya na kuipeleka sokoni, huwa huanzi na soko kubwa, badala yake utawaambia wale wasambazaji wako, msiende mbali kwanza, hakikisheni kwanza hapa mtaani kwetu au mkoani kwetu bidhaa zetu zimefika.

Kwa sentensi hiyo, haimaanishi kwamba..bidhaa yako huna mpango wa kuivukisha mipaka siku za mbeleni…

Bali ni umefanya hivyo ni kwasababu unataka kazi imalizike hapa kwanza, ndipo iende pengine…Mahitaji ya hapa yakishajitosheleza kwamba watu wameikubali au wameikataa ndipo utanue na kwenda kuitangaza mahali pengine mbali Zaidi.. hiyo ndiyo hekima na akili.

Ndicho Bwana alichowaambia wanafunzi wake, kwamba kwa wakati ule waanze Injili kwa WaIsraeli kwanza, na ndipo wengine watafuata, wasirukie kwenda pengine, muda wa kwenda huko bado.. Ili tuelewe vizuri zaidi hebu tukisome tena kile kisa maarufu tunachokijua cha yule mwanamke mkananayo ambaye hakuwa Mwisraeli.

Mathayo 15: 22 “Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo.

23 Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu.

24 Akajibu, akasema, SIKUTUMWA ILA KWA KONDOO WALIOPOTEA WA NYUMBA YA ISRAELI. 25 Naye akaja akamsujudia, akisema Bwana, unisaidie”.

Sasa tuishie hapo, na kisha twende tena tukakirudie kisa hiki hiki katika Injili ya Marko, ili tupate kuelewa Zaidi…

Marko 7:24 “Akaondoka huko, akaenda zake hata mipaka ya Tiro na Sidoni. Akaingia katika nyumba, akataka isijulikane na mtu; lakini hakuweza kusitirika.

25 Ila mara mwanamke, ambaye binti yake yuna pepo mchafu, alisikia habari zake, akaja akamwangukia miguuni pake.

26 Na yule mwanamke ni Myunani, kabila yake ni Msirofoinike. Akamwomba amtoe pepo katika binti yake.

27 Akamwambia, WAACHE WATOTO WASHIBE KWANZA; maana si vizuri kukitwaa chakula cha watoto, na kuwatupia mbwa.

28 Naye akajibu, akamwambia, Naam, Bwana, lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya Watoto”.

Ukiusoma hapo kwa makini huo mstari wa 27?…utaona Bwana Yesu anamwambia huyo Mwanamke ambaye sio mwisraeli, anamwambia waache Watoto washibe KWANZA… Sasa kama wewe unaelewa Kiswahili vizuri, utakuwa pia unaelewa nini maana ya neno “KWANZA”… Neno kwanza maana yake, kinaanza hichi, halafu ndipo kifuate kingine.

Ndicho Bwana alichomaanisha hapo, kwamba waache Waisraeli wale KWANZA(yaani wapokee baraka hizi za rohoni kwanza), ndipo nyie watu wa mataifa mtafuata baadaye..Ndio maana mwishoni kabisa

mwa Injili yake, siku ile baada ya kufufuka kwake, aliwapa wanafunzi wake ruhusa sasa ya kwenda kote ulimwinguni kuhubiri injili, kwasababu wakati wa mataifa umeshafika…

Luka 24:46 “Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu;

47 na kwamba MATAIFA YOTE watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, KUANZA TANGU YERUSALEMU.

48 Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya.

49 Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu”

Mstari huo wa 47, umehitimisha jibu la swali letu.. Kwahiyo Injili ni kwa watu wote na mataifa yote, Ilianzia Yerusalemu (yaani kwa waisraeli)..na sasa inahubiriwa kwenye mataifa yote..na imeshafika kila Taifa duniani, mpaka mataifa ambayo ni ngumu kufikiwa, lakini imeshapenya…anasubiriwa tu yule kondoo wa Mwisho kuingia ndani ya Neema, ule mwisho ufike, kama alivyosema..Marko 13: 10 “Na sharti Injili ihubiriwe kwanza katika mataifa yote” na Mathayo 24:14 “Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja”

Je umetubu dhambi zako na kumpokea Kristo?..Kama bado unasubiri nini..Ni wapi leo injili haihubiriwi?..unadhani tunaishi nyakati gani hizi?…Dunia inaisha na Zaidi ya yote ibilisi anafanya kazi kwa nguvu sana nyakati hizi za mwisho, kuwapotosha watu, na kuwaaminisha kwamba hakuna Mungu , wala mwisho wa dunia, Mkabidhi leo Kristo Maisha yako kama hujafanya hivyo bado, na ukabatizwe na kupokea Roho Mtakatifu, ili upate kuokoka.

Bwana akubariki

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

JINA LAKE KWA KIEBRANIA NI ABADONI, NA KWA KIYUNANI NI APOLIONI.

Tofauti kati ya Myunani, Farisayo na Sadukayo ni ipi?

JIEPUSHE NA UNAJISI.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments